Hesperian Health Guides

Dawa za wasiwasi, kukosa utulivu

Diazipamu (diazepam)


Diazipamu inaweza kutumika kulegeza misuli na kutuliza maumivu. Inaweza pia kutumika kusimamisha shambulio la mara moja. Kwa watu wenye mashambulizi ya mara kwa mara (kifafa), tumia dawa tofauti, dawa ambayo inaweza kutumika kila siku.


Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Kusinziasinzia.

MuhimuNBgrnimportant.png
  • Kuzidisha kiasi cha dawa ya diazipamu kinyume na maelekezo huweza kupunguza kasi ya kupumua au kusimamisha kupumua kabisa. Usitoe zaidi ya dozi ya dawa iliyoelekezwa na usitoe zaidi ya dozi 2.
  • Diazipamu ni dawa inayojenga kiu cha kuendelea kuitumia. Epuka matumizi ya muda mrefu au ya mara kwa mara.
  • Usitoe dawa hii kwa mjamzito au mama ambaye ananyonyesha isipokua tu kama amepata shambulio (kwa mfano kutokana na kifafa cha mimba).
  • Usichome sindano ya diazipamu isipokuwa tu kama una uzoefu au umepitia mafunzo ya kufanya hivyo. Ni vigumu kutoa dawa hii kwa njia ya sindano. Badala yake, wakati wa shambulio, unaweza kuiweka kwenye njia ya haja kubwa (angalia chini).


Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Kulegeza misuli na kumtuliza mtu

Toa vidonge vya diazipamu kwa njia ya mdomo dakika 45 kabla ya kutoa huduma yenye maumivu kama vile kunyoosha mfupa uliovunjika. Toa miligramu 0.2 hadi 0.3 kwa kila kilo. Kama huwezi kumpima mtu, toa dozi kuzingatia na umri:
Chini ya miaka 5: toa miligramu 1.
Zaidi ya miaka 5: toa miligramu 2.

Kwa ajili ya shambulio

Tumia dawa mchanganyiko wenye majimaji kwa ajili ya sindano, au saga kidonge 1 na kuchanganya na maji. Toa sindano kutoka kwenye bomba, halafu nyonya dawa na kuiingiza ndani ya njia ya haja kubwa. Au tumia diazipamu teketeke (gel) ambayo imetengenezwa kwa ajili ya matumizi kwenye njia ya haja kubwa. Mlaze mgonjwa upande na tumia bomba isiyo na sindano kuingiza dawa ndani kabisa ya njia yake ya haja kubwa. Halafu makalio yake yabaki pamoja kwa dakika 10 ili dawa iweze kubaki ndani.
Chini ya miaka 7: mpe miligramu 0.2 kwa kilo, mara moja.
Miaka 7 hadi 12: toa miligramu 3 hadi 5, mara moja.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 5 hadi 10, mara moja.

Kama shambulio halijadhibitiwa baada ya dakika 15 za kutoa dawa hii, rudia dozi. Usirudie zaidi ya mara moja.

Lorazipamu (lorazepam)


Lorazipamu inafanana sana na diazipamu. Inaweza kutumika kulegeza misuli na kumtuliza mtu. Inaweza pia kutumika kusimamisha shambulio la mara moja. Kwa watu wanaopatwa na mashambulio ya mara kwa mara(kifafa), tumia dawa tofauti, dawa ambayo inaweza kutumia kila siku.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Kizunguzungu.

MuhimuNBgrnimportant.png
  • Kuzidisha dozi ya dawa ya lorazipamu kunaweza kupunguza au kusimamisha pumzi kabisa.
  • Lorazipamu ni dawa inayojenga kiu ya kuendelea kuitumia. Epuka matumizi ya muda mrefu au ya mara kwa mara.
  • Usitoe dawa hii kwa mjamzito isipokuwa tu kama ana kifafa cha mimba au shambulio
  • Usichome diazipamu kwenye msuli au mshipa isipokuwa tu kama una uzoefu au umepitia mafunzo ya kufanya hivyo. Ni vigumu kutoa dawa hii kwa njia ya sindano. Badala yake, wakati wa shambulio, unaweza kuiweka kwenye njia ya haja kubwa (angalia sehemu inayofuata).


Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Kulegeza misuli na kumtuliza mtu

Toa vidonge vya lorazipamu kwa njia ya mdomo dakika 45 kabla ya kutoa huduma yenye maumivu kama vile kunyoosha mfupa uliovunjika.
Mwezi 1 hadi miaka 12: toa miligramu 0.05 kwa kilo, mara moja.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 1 hadi 2, mara moja.