Hesperian Health Guides

Utoaji mimba salama na usiyo salama

Katika sura hii:

Utoaji mimba salama una uwezekano mdogo wa kusababisha madhara kuliko kuibeba mimba hiyo na kupata mtoto.

Utoaji mimba unakuwa salama kama:
  • Utafanywa na mfanyakazi wa afya ambaye amepitia mafunzo na mwenye uzoefu.
  • Utafanyika kwa kutumia vifaa sahihi.
  • Utafanyika katika mazingira masafi. Kila kinachoingizwa ukeni na kwenye kizazi (tumboni) lazima kiwe kimetakaswa ili kuua wadudu wote.
  • Hauzidi miezi 3 (wiki 12) baada ya hedhi ya mwisho.
Utoaji mimba unakuwa siyo salama kama utafanyika:
  • Na mtu ambaye hajapitia mafunzo ya utoaji mimba.
  • Kwa kutumia vifaa au dawa zisizo sahihi.
  • Katika mazingira yasiyo masafi.
  • Ujauzito ukiwa umezidi miezi 3 (wiki 12), isipokuwa kama utafanyika katika kituo cha afya au hospitali ambayo ina vifaa maalum.

Vifo kutokana na utoaji mimba usiyo salama

WWHD10 Ch15 Page 241-2.png Kati ya wanawake
100,000 wanaopata
huduma ya utoaji
mimba salama, ni
1 tu ambaye
hupoteza maisha.
WWHD10 Ch15 Page 241-1.png
Lakini kati ya wanawake
100,000 ambao wanatoa
mimba kwa njia zisizo
salama kati ya 100 na
1000 watapoteza maisha.

Duniani, inakadiriwa vitendo vya utoaji mimba milioni 46 hufanyika kila mwaka na mara nyingi wanawake hunusurika, hata kama sehemu kubwa ya vitendo hivyo haviruhusiwi kisheria. Lakini utoaji mimba usiyo salama unaweza kusababisha kifo, au matatizo mengine kama vile maambukizi, maumivu ya kudumu, na ugumba.

Wanawake wanapokata tamaa mara nyingi hujaribu kutafuta njia za kukatisha ujauzito. Epuka njia zifuatazo. Ni hatari sana.

Epuka utoaji mimba usiyo salama. Jaribu kuzuia mimba isiyotakiwa kabla haijatokea.

  • Usiingize vifaa vyenye ncha kali kama vile vijiti, waya au mirija ya plastiki ukeni au kwenye kizazi (tumboni). Vitu hivyo vinaweza kutoboa au kujeruhi tumbo na kusababisha kuvuja damu na maambukizi hatari.
  • Usiweke dawa za mitishamba au mimea ukeni au tumboni. Vitu hivyo vinaweza kuunguza au kukudhuru vibaya, na kusababisha uharibifu wa viungo vya ndani, maambukizi, na uvujaji damu.
  • Usiweke vitu kama vile vinavyobabua, majivu, sabuni, au mafuta ya taa ukeni au tumboni. Pia kamwe usinywe vitu hivyo.
  • Usitumie dawa au tiba za asili katika vipimo vikubwa ili kutoa mimba (iwe kwa njia ya mdomo au kupitia ukeni). Kwa mfano, kutumia dawa nyingi ya malaria (krolokwini) au dawa za kusimamisha damu kutoka baada ya kujifungua (ergometrine, oxytocin) kunaweza kusababisha kifo hata kabla mimba haijatoka.
  • Usipige tumbo lako au kujirusha chini kwenye ngazi. Hii inaweza kusababisha majeraha na uvujaji damu ndani ya mwili wako, lakini usisababishe mimba kutoka.
MUHIMU! Kamwe usiweke kitu chochote ndani ya tumbo lako au kuruhusu mtu ambaye hajapitia mafunzo kufanya hivyo. Hii inaweza kusababisha kifo.

Upatikanaji wa huduma salama ya utoaji mimba

Mwanamke anapokabiliwa na mimba isiyotakiwa, anapaswa kuwa na fursa ya kupata huduma salama na ya kisheria ya utoaji mimba. Lakini sheria juu ya utoaji mimba hutofuatiana kati ya nchi moja na nyingine.

Hata kama utoaji mimba hauruhusiwi kisheria, mwanamke kwa kawaida anaweza kupata msaada wa daktari kwa ajili ya matatizo ambayo hutokea baada ya jaribio la kutoa mimba. Mara nyingi ni vigumu kutofuautisha kati ya utoaji mimba wa makusudi au mimba kuharibika kwa bahati mbaya, isipokuwa kama kuna kitu au vitu ambavyo viliachwa tumboni.

Utoaji mimba kisheria. Kama utoaji mimba utaruhusiwa kisheria, mwanamke anaweza kuingia, bila kikwazo, kwenye kiliniki au hospitali, kulipa ada, na kupata huduma salama ya utoaji mimba. Katika nchi mahali ambapo utoaji mimba unaruhusiwa kisheria, ni mara chache mwanamke kuugua au kufariki kutokana na matatizo yanayosababishwa na utoaji mimba.

Utoaji mimba kisheria katika baadhi ya nchi. Katika baadhi ya nchi, utoaji mimba huruhusiwa kisheria tu kwa sababu kadhaa, kama vile:

  • Kama mwanamke amepata ujauzito kutokana na kubakwa au amefanya ngono na mwanafamilia wa karibu (ndugu wa damu wa karibu).
  • Kama daktari atasema mimba hiyo itahatarisha afya ya mama.

Lakini huduma ya utoaji mimba salama mara nyingi haipatikani kwa urahisi, hata kwa sababu zilizoelezwa juu. Madaktari na wafanyakazi wa afya wanaweza kutokuwa na uhakika sheria inasema nini. Wanaweza kutokuwa tayari kutoa huduma hiyo kwa uwazi, au wanaweza kudai fedha nyingi. Na wanawake wanaweza kutojua iwapo utoaji mimba unaruhusiwa kisheria katika nchi yao au kama huduma salama inapatikana.

Utoaji mimba usiyoruhusiwa kisheria. Kama utoaji mimba hauruhusiwi kisheria, wote-wanawake wanaotoa mimba na wale wanaosaidia kuzitoa wanaweza kushitakiwa. Katika sehemu nyingi hili halifanyiki. Lakini mahali ambapo utoaji mimba hauruhusiwi kisheria, wanawake wengi hufariki kutokana na utoaji mimba usiyo salama na mimba zisizo salama. Fedha ambayo ingetumika kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa wanawake badala yake hutumika katika kutibu matatizo makubwa ya kiafya yanayohusiana na utoaji mimba usiyo salama.

Kamwe usichukulie moja kwa moja kwamba utoaji mimba hauruhusiwi kisheria katika jamii yako. Jaribu kutafuta ukweli -sheria zinasema nini katika nchi yako. Inaweza kuwa rahisi zaidi kuzizunguka sheria hizo hizo kuliko kujaribu kuzibadili. Hata kama utoaji mimba hauruhusiwi kisheria, huenda kukawa na watu wanaotoa huduma salama ya utoaji mimba. Huduma salama ya utoaji mimba inaweza kukusaidia kuokoa maisha na kukuepusha kifo.


Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Mei 2017