Hesperian Health Guides
Nini cha kutarajia katika utoaji mimba salama?
HealthWiki > Pale ambapo Wanawake hawana Daktari > Sura ya 15: Utoaji mimba na matatizo yanayotokana na utoaji mimba > Nini cha kutarajia katika utoaji mimba salama?
Kunywa vinywaji kwa wingi siku inayotangulia huduma ya utoaji mimba. Hii itakusaidia kupona haraka.
Unapokwenda kwenye kituo cha afya au hospitali kwa ajili ya kutoa mimba, unapaswa kupokelewa vizuri na kwa heshima. Mshauri nasaha anapaswa kuongea na wewe juu ya uamuzi wako na kuelezea jinsi mimba itakavyotolewa na madhara yanayoweza kutokea.
Taarifa zifuatazo zinaelezea nini cha kutarajia katika utoaji mimba salama. Utoaji mimba ambao ni tofauti na njia zilizoelezewa hapa unaweza kuwa hatari.
- Unapaswa kuulizwa lini ulipata hedhi yako ya mwisho na iwapo una maambukizi ya ngono.
- Mfanyakazi wa afya anapaswa kufanya uchunguzi wa kitabibu. Hii inajumuisha kuchunguza ndani ya uke wako na juu ya tumbo kwa ajili ya ukubwa wa mji wa mimba.
- Wakati wa utoaji mimba kwa vifaa vya ya unyoyaji au ufyonzaji na ukwanguaji, utasikia maumivu makubwa sehemu ya chini ya tumbo. Lakini mara baada ya mimba kutoka, maumivu yatapungua.
- Baada ya kutoa mimba, sehemu zako za uzazi zinapaswa kusafishwa, na baada ya hapo kupelekwa kupumzika. Mfanyakazi wa afya anapaswa kuwepo kuangalia hali yako angalau kwa saa moja.
- Mfanyakazi wa afya au daktari anapaswa kukueleza nini cha kufanya baada ya kutoa mimba, dalili za hatari ambazo unapaswa kuangalia, na nani wa kuwasiliana naye iwapo matatizo yatatokea.
Vilevile, mfanyakazi wa afya anapaswa kuongea na wewe juu ya njia za uzazi wa mpango. Unaweza kuanza kutumia njia moja wapo inayofaa siku hiyo ya utoaji mimba. Unapaswa kupangiwa tarehe ya kurudi kufanyiwa uchunguzi ndani ya wiki 1 au 2.