Hesperian Health Guides
Kudhibiti utoaji mimba usiyo salama
HealthWiki > Pale ambapo Wanawake hawana Daktari > Sura ya 15: Utoaji mimba na matatizo yanayotokana na utoaji mimba > Kudhibiti utoaji mimba usiyo salama
Elimu ya uzazi wa mpango inaweza kupunguza haja ya kutoa mimba. |
Hapa chini ni baadhi ya mambo ambayo mwanamke yoyote au kikundi cha wanawake wanaweza kufanya kwenye jamii kupunguza magonjwa na vifo kutokana na utoaji mimba:
- Kutoa elimu kwa wanaume, wanawake, na jamii kwa ujumla juu ya namna uzazi wa mpango unavyosaidia kudhibiti matukio ya utoaji mimba. Ni vizuri zaidi kwanza kupata mafunzo ya utoaji wa huduma za uzazi wa mpango kwa wanawake kwenye jamii yako.
- Kutoa elimu kwa wanawake na wasichana kwenye jamii yako juu ya hatari ya utoaji mimba usiyo salama.
- Kuwatembelea watu kwenye jamii yako ambao wanajishughulisha na utoaji mimba ili kuhakikisha wanatoa huduma hiyo kwa usalama.
- Kujifunza juu ya matatizo ya kiafya yanayohusiana na utoaji mimba na jinsi ya kusaidia. Tafuta wapi unaweza kumpeleka mwanamke mwenye matatizo yanayohusiana na utoaji mimba kwenye jamii yako kwa ajili ya huduma za dharura.
- Tafuta fursa za usafiri wa haraka kwa mwanamke ambaye anahitaji huduma za dharura. Kama hakuna huduma ya usafiri wa dharura, mfano gari la wagonjwa, je kuna mtu yoyote kwenye jamii mwenye gari? Hifadhi chombo chenye petroli au dizeli ya akiba kwa ajili ya usafirishaji wakati wa dharura.
- Weka akiba ya dawa muhimu za dharura kwenye duka la dawa la kijiji au kliniki kutibu matatizo ya kiafya ya dharura yanayohusiana na utoaji mimba.
Kama wewe ni mfanyakazi wa afya, yafuatayo ni mapendekezo ya nyongeza:
Wahimize wanawake ambao wamepata matatizo baada ya kutoa mimba kutafuta msaada haraka, badala ya kuficha hali zao.
- Jitahidi kupata mafunzo ya kutoa huduma ya MVA - kusafisha tumbo la uzazi kwa kutumia vifaa vya unyonyaji au ufyonzaji, ili uweze kuwasaidia wanawake wenye matatizo yanayohusiana na utoaji mimba. Mafunzo kama haya yanaweza kutolewa kwa wafanyakazi wa afya hospitalini. Usitoe huduma ya utoaji mimba isipokuwa kama umepata mafunzo na unavyo vifaa safi na sahihi vya kutoa huduma hiyo kwa usalama.
- Saidia kuwezesha wafanyakazi wa afya kwenye jamii yako kuongea na viongozi wa idara ya afya juu ya hatari za utoaji mimba. Hata mahali ambapo utoaji mimba hauruhusiwi kisheria, huduma za matibabu kwa matatizo yanayohusiana na utoaji mimba zinapaswa kupatikana ili kuokoa maisha ya wanawake.