Hesperian Health Guides

Njia za kujifunza na kuhamasisha jamii

Katika sura hii:

Njia ya vikundi inaweza kusaidia watu kuelewa mizizi ya matatizo yao ya kiafya na kufanya mipango ya kuyatatua. Njia utakayoitumia itategemea unacholenga na raslimali zilizopo. Njia hizo ni muhimu zisaidie:

  • Kuwaleta watu pamoja na kujadili matatizo yanayowasibu.
  • Kugundua fikra za watu juu ya mahitaji yao.
  • Kukusanya taarifa juu ya visababishi vya tatizo la afya husika.
  • Kufanya uchambuzi wa matatizo ili kugundua sababu zake za haraka na sababu za muda mrefu za matatizo hayo.
  • Kukusanya mawazo ya makundi yote katika jamii. Mradi hautafanikiwa iwapo baadhi ya makundi au mawazo hayatazingatiwa. Baadhi ya watu huenda wakashindwa kuchangia kwa kuhisi kuwa mawazo yao hayathaminiwi.


Daima, afya ya mazingira ni suala la jamii nzima na huhitaji watu kufanya kazi pamoja ili kuleta maboresho. Hata kama lengo ni kudhibiti mlipuko wa kipindupindu, kuanzisha bustani ya umma, kuboresha afya na usalama wa watu wanaoishi karibu na viwanda, au wanaofanya kazi kwenye migodi, au kuzungumzia suala lolote linalohusu afya ya mazingira, kadri watu wengi zaidi wanapolielewa tatizo na kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu ufumbuzi, ndivyo watakavyofanikiwa.

Majadiliano katika vikundi mahsusi

Katika baadhi ya jamii, wanawake na wasichana wanaweza kushiriki vizuri zaidi kupitia vikundi vyao mahsusi tofauti na kuwachanganya na wanaume. Kundi mahsusi la wanawake baadaye linaweza kuwasilisha mawazo yao katika hadhara ya watu wote. Kwa njia hii, wanawake na wasichana hupata nafasi ya kuongea kwa sauti yenye nguvu na umoja mbele ya jamii nzima. Kwa kuimarisha sauti ya wanawake na wasichana na kuwajengea stadi za uongozi, jamii nzima huimarika.

 illustration of the below: 5 women gather for a group discussion next to a sign reading, "Toilets too far from my house. Safer to go in the bush. No way to wash."
Vyoo siyo salama kwa watoto
Hata sisi tunapokuwa katika hedhi, haturuhusiwi kutumia vyoo.
Kama unataka kutatua tatizo, washirikishe wale wanaoathirika kutokana na tatizo hilo.

Majadiliano yanayoongozwa na mtu maalum

Ili kubadilishana maarifa juu ya matatizo ya kiafya, watu wanahitaji kuongea na wenzao. Majadiliano yanayoongozwa na mtu maalum ni njia ambayo watu wanaweza kuongea pamoja wakiwa katika kikundi, kuulizana na kujibu maswali mahsusi. Zoezi la kutumia swali la Lakini kwa nini? ni mfano wa aina ya majadiliano yanayoongozwa na mtu maalum.

Mwongozaji wa majadiliano wakati mwingine huitwa mwezeshaji. Mazoezi mengi katika moduli hii yanahitaji mwezeshaji ili kuhakikisha kila mtu anashiriki kadri ya uwezo wake na kusaidia zoezi au mjadala kuzaa matunda.

Uchoraji ramani ya jamii

 A group of men and women bend over to make a map.
Chora ramani kwa kutumia kalamu, au rangi kwenye karatasi, au chini kwenye sakafu au udongo kwa kutumia vijiti na vifaa vingine vilivyopo.

Zoezi la uchoraji wa ramani ya jamii (mtaa au kijiji) ni zoezi ambalo huwezesha watu kwa pamoja kuchora ramani kulingana na yale ambayo wanaona na kufahamu kuhusu eneo lao. Kwa kutengeneza ramani ya afya ya jamii tunaweza kujifunza:

  • Wapi matatizo ya afya yalipo.
  • Nani huathiriwa na matatizo hayo.
  • Namna gani matatizo hayo ya afya yanaweza kutokea kwa sababu ya hali ya mazingira.

Zoezi la uchoraji ramani linaweza kusaidia watu kuangalia mwenendo wa matatizo ya kiafya katika jamii yao, kuanza utambuzi wa mizizi ya matatizo hayo na kuangalia jinsi gani hali katika jamii imekuwa ikibadilika. Ramani inaweza pia kusaidia watu kutambua raslimali muhimu katika jamii yao na fursa zingine zilizopo ambazo pengine zilikuwa hazijabainishwa. Pia uchoraji ramani unaweza kutumika kama hatua muhimu katika kulinda maeneo muhimu au nyeti katika jamii husika.

Uchambuzi shirikishi wa mahitaji ya jamii

Watu kawaida wana maoni tofauti kuhusu matatizo katika jamii zao na njia bora za kuyatatua. ‘Uchambuzi shirikishi wa mahitaji ya jamii’ ni mchakato wa kuongeza uelewa wa wanajamii juu ya matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii yao na sababu zake, na kuwasaidia kuamua ni yapi yanayofaa kushughulikia kupitia mipango ya muda mfupi na yapi kushughulikia kupitia mipango ya muda mrefu. Mchakato mzuri wa uchambuzi shirikishi wa mahitaji ya jamii unaweza kuhakikisha kuwa mahitaji ya kila mtu na uwezo wao vinazingatiwa wakati wa uandaaji mipango.

Men, women and children walk together through a village of thatched huts.

Matembezi ya kiutafiti

Wakati wa matembezi ya kiutafiti, watu huichunguza jamii yao kwa karibu zaidi kugundua vitu ambavyo vinaweza kuwa vinasababisha matatizo ya kiafya kwa jamii, kama vile vyanzo vya maji visivyo salama, biashara zinazochafua mazingira n.k. Matembezi ya kiutafiti yanapofanyika katika kikundi, watu hupata fursa zaidi ya kubadilishana mawazo juu ya matatizo wanayogundua katika zoezi hilo. Baadaye wanaweza kushirikiana zaidi kutafuta ufumbuzi. Kadri matembezi ya kiutafiti yanavyowashirikisha watu wengi zaidi ndipo matokeo yanapokuwa bora zaidi.

Ulinganishi wa hali ya jamii ya sasa na vipindi vilivyopita

Njia nyingine ya kuelewa matatizo na mahitaji ndani ya jamii ni kulinganisha hali ya sasa na ilivyokuwa siku za nyuma. Halafu fikiria jinsi ungependa hali iwe siku za usoni. Njia mojawapo ya kuifanya kazi hii ni kukusanya hadithi kutoka kwa wazee katika jamii husika.

Pia kuwawezesha vijana katika jamii husika kuongoza zoezi hili husaidia kujenga heshima na maelewano kati ya marika. Husaidia pia kuhifadhi mila zenye manufaa kwa jamii ambazo kila mtu angependa kuzitunza.

Kumbukumbu za matukio muhimu katika jamii husaidia watu kuelewa jinsi gani mabadiliko yametokea kutoka kizazi hadi kizazi, na kuzingatia matukio muhimu kama vile barabara ilipojengwa, kiwanda kilipozinduliwa, bwawa lilipojengwa, n.k. Kuandaa kumbukumbu za mabadiliko ya mazingira ni njia nyingine ya kubadilishana maarifa juu ya historia ya jamii kupitia picha au ramani za mabadiliko katika vipindi tofauti kwenye mashamba, misitu, makazi, mito na maziwa.

Uchoraji

Men and women make drawings. Kuchora na kuangalia michoro kunaweza kusaidia kupata ufumbuzi wa matatizo ambao pengine tusingeweza kuupata. Michoro inaweza kutumika kuanzisha majadiliano yanayoongozwa na mtu maalum au mwezeshaji. Michoro pia inaweza kuwa njia, kwa watu ambao hawawezi kusoma au kuandika vizuri, kujieleza vizuri na kushiriki katika uongozi wa kikundi (soma namna magonjwa ya kuhara yanavyosambazwa).

Baadhi ya jamii zinaweza kushirikiana kuchora picha za rangi kwenye kuta za nyumba au majengo, ambazo zinaonyesha matatizo yao na matarajio yao ya maisha na afya bora ya baadaye.

Uchunguzi shirikishi jamii

Uchunguzi shirikishi jamii ni njia mojawapo ya kukusanya taarifa. Tafiti za aina hii zinaweza kutumika kuchunguza masuala muhimu ya kiafya katika jamii husika, kuangalia yale yanayofanana au kutofautiana katika fikra au imani za watu na hata kupima kwa kiwango gani watu wanaunga mkono mipango na shughuli zinazotekelezwa katika jamii.

A female survey worker visits at the doorway of a home and listens to a woman as two other women watch.

Katika zoezi la uchunguzi shirikishi jamii, maswali yale yale huulizwa na watu tofauti wanaoshiriki kwa njia ile ile. Uchunguzi huu unaweza kufanyika nyumbani, sehemu za kazi, shuleni, sehemu za ibada, sehemu nyingine zenye mikusanyiko ya watu au hata kwa njia ya simu au posta.

Uchunguzi shirikishi jamii huruhusu watu kubadilishana mawazo yao kwa faragha bila kulazimika kukusanyika kwenye mikutano au sehemu nyingine za wazi. Hii inaweza kuwa njia nzuri kwa watu waoga au wale ambao hawapewi fursa kushiriki katika maamuzi ya kijamii kuwasilisha kero na mawazo yao.

Maigizo

Maigizo ni njia ya kuchunguza matatizo na kupendekeza ufumbuzi wakati watu wakiendelea kuburudika na kucheka. Watu wanaweza kuigiza masuala yanayowahusu na pia kuhusisha watu wengine. Baadhi ya mambo na mifarakano inaweza kutazamwa kwa makini zaidi ikionyeshwa wakati na katika mazingira tofauti.

Tamthilia

Tamthilia huruhusu watu kuigiza tatizo na kuonyesha baadhi ya sababu na athari zake. Tamthilia hutoa kila aina ya msisimko. Baadhi ya waandaaji wa shughuli za jamii hupenda kuhitimisha tamthilia kwa kuwawezesha watu kuimba pamoja, au kufanya zoezi lingine la pamoja.

Hadithi yoyote inaweza kugeuzwa kuwa tamthilia ili mradi wawepo waigizaji wa tatizo ambalo linatafutiwa ufumbuzi.
illustration of the above: People watch as 2 men and a woman act out a drama.

Tamthilia shirikishi ni aina ya tamthilia ambapo watu wote hutazama na pia kushiriki. Mtu yeyote miongoni mwa watazamaji anaweza kuwaambia waigizaji kusimamisha igizo na kuchukua nafasi ya mmojawapo wa waigizaji kuigiza ufumbuzi mbadala kwa tatizo husika. Hii hasa husaidia katika hali mbalimbali ambapo watu tofauti kwa zamu, huigiza nafasi ya mtu mwenye uwezo kidogo au asiye na uwezo kabisa.

Igizo dhima

Igizo dhima halihitaji sana maandalizi kama tamthilia na linaweza kusaidia kuelezea njia mbalimbali za kutafuta ufumbuzi kwa migogoro au matatizo. Watu huchukua nafasi mbalimbali katika hali halisi ya maisha na kuonyesha jinsi ambavyo wangeweza kufanya. Mnaweza kujadili na kulirudia igizo dhima ili kuelewa kwa nini watu wana tabia hizo walizo nazo.

Kubadili mienendo na utendaji wa watu wenye uwezo jukwaani ni rahisi lakini katika maisha ya kawaida ni kazi ngumu sana. Kwa kutumia tamthilia tunaweza kufanya zoezi la kukabiliana na watu wenye mamlaka juu yetu, uzoefu ambao unaweza kuwasaidia watu kupata njia mbalimbali za kukabiliana na mamlaka katika maisha ya kawaida.

A child behind a table on its side performs a puppet show for 2 other children.

Onyesho la vikaragosi

Onyesho la vikaragosi hutumia vikaragosi badala ya watu katika kuigiza hadithi juu ya migongano ya kijamii. Vikaragosi huwafanya watu kucheka na pia kuona vitu kupitia mtazamo ambao si wa kawaida. Baadhi ya watu hupata urahisi kuongea kupitia vikaragosi kuliko kuigiza wao wenyewe kwenye jukwaa.


Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022