Hesperian Health Guides

Waelimishaji jamii wa afya wazuia kipindupindu

Katika sura hii:

Katika pwani ya nchi ya Ekueda, kawaida miezi 6 ni ya ukame na miezi sita mingine ni ya mvua. Hii hufanya hali kuwa ngumu kwa ajili ya kuotesha mazao. Kuna masoko machache na serikali haijafanya juhudi za kutosha kujenga shule, vituo vya afya na huduma nyingine za msingi kama vile maji safi na mifumo ya maji taka. Kipindupindu kilipopiga hodi mwaka 1991, karibu watu wote hawakuwa wamejiandaa na hivyo wengi waliugua. Siku hadi siku, watu walileta jamaa zao kwenye vituo vya afya, wakiwa wamedhoofu, wakitetemeka, wakiwa na homa kali, maumivu na upungufu wa maji mwilini kutokana na kuharisha sana. Wanaharakati wa afya waligundua kuwa ni kipindupindu na watu wengi wangefariki dunia kama wasingechukua hatua za haraka kudhibiti mlipuko huo.

Kwa sababu kipindupindu huathiri maji ya kunywa na kuenea haraka kutoka mtu mmoja hadi mwingine, wanaharakati wa afya walijua kuwa tiba kwa wagonjwa pekee haikuwa jawabu la kutosha. Ili kuzuia kipindupindu kuenea, ilibidi watafute njia ya kumwezesha kila mtu mjini hapo na vijiji vya jirani kupata huduma ya maji safi na vyoo salama.

Wanaharakati wa afya walianza kwa kuwahamasisha wana vijiji ambao walikuwa bado wana nguvu na kuomba vikundi mbalimbali katika jamii kusaidia. Walilishawishi shirika moja lenye uhusiano na mashirika mengine katika nchi za nje kuwapatia msaada wa fedha ili kuanzisha mradi wa dharura wa huduma ya maji safi na vyoo salama.

Waliuita mradi wao Afya kwa Jamii. Kupitia mradi huo, wanaharakati waliunda Kamati za Afya katika kila kijiji. Wajumbe wa kamati hizo waliwachagua Waelimishaji Jamii ambao walipewa mafunzo ya uelimishaji jamii juu ya maji na vyoo, hususan ujenzi na utunzaji wa vyoo, na kunawa mikono kuzuia kuenea kwa vijidudu visababishavyo magonjwa. Kwa njia hii wanaharakati wa afya waliwezesha wana vijiji wenyewe kuchukua sehemu muhimu ya mapambano dhidi ya kipindupindu, na kuboresha afya ya mazingira katika jamii zao.

 woman speaking
Fedha za kufanyia kazi lilikuwa hitaji muhimu, lakini tulihitaji zaidi ya fedha. Tulihitaji pia watu wa kufanya kazi ya kuzuia kipindupindu kisienee.

Kufanya kazi pamoja ili kuleta mabadiliko

Jambo la kwanza ambalo waelimishaji jamii wa kijiji walilofanya ni kuwaelimisha watu jinsi kipindupindu na magonjwa mengine ambayo husababisha kuhara yanavyoenezwa. Baadaye walisaidia kila kaya na kila kijiji kuhakikisha usafi na usalama wa mfumo wa maji yake. Waliwafundisha watu pia jinsi ya kuzuia tatizo la upungufu wa maji mwilini, ambalo ndio chanzo kikuu cha vifo kutokana na kuhara. Waliwafundisha jinsi ya kutengeneza kinywaji cha kuongeza maji mwilini. Kinywaji hiki hutengenezwa kwa kuchanganya chumvi na sukari katika maji yaliyochemshwa na kuwapa watoto au mwingine yeyote ambaye anaharisha. Waliwafundisha watu shuleni, misikitini, kanisani, kwenye vituo vya jamii na kupitia mikutano jinsi ya kuzuia kipindupindu kwa kunawa mikono yao, na kujenga na kutumia vyoo salama. Baada ya wiki chache, kipindupindu kilikaribia kutoweka kabisa.

 A group of men build a shelter over a pit toilet.

Lakini wanaharakati walijua kuwa bado walikua na kazi zaidi ili kuhakikisha kipindupindu hakitokei tena. Kwa kushirikiana na mafundi ujenzi, mafundi bomba na mafundi seremala, watu walijenga mifumo ya maji ya bomba, kuboresha vyoo vya shimo katika kila kijiji na kuhakikisha kila kaya ilikuwa na maji ya kutosha ya kuoga.

Wanavijiji wenyewe ndiyo walioifanya kazi hiyo na kujifunza jinsi ya kusafisha na kutunza mifumo ya maji na vyoo. Pia walihakikisha kuwa wanyama waliwekwa katika uzio, ili kuzuia kinyesi chao kuingia katika mfumo wa maji. Pia walihimiza vifaa vya maji kufunikwa ili kuzuia mbu waletao ugonjwa kuzaliana ndani.

Kadri kazi hii ilivyoendelea, watu kutoka vijiji vingine walijiunga na mradi huu ambao ulianza na vijiji 22 na baada ya muda mfupi kufikia vijiji 100. Mara baada ya hapo, kipindupindu kilidhibitiwa katika eneo lote na magonjwa mengine pia kupungua.

Mambo gani yalichangia kufanikisha jamii kujipanga kwa ajili ya afya yake?

Mradi wa Afya kwa Jamii ulifanikiwa sana katika kuzuia kipindupindu na kuendelea kupambana na matatizo mengine. Mafanikio haya yalitokana na Waelimishaji Jamii wa Afya:

  • Kufanya kazi na watu katika kaya zao: Waelimishaji Jamii wa Afya waliwafundisha watu nyumba hadi nyumba juu ya kulinda usafi na usalama wa vyanzo vyao vya maji. Shughuli hii ilisaidia pia vikundi vya waelimishaji jamii kujifunza juu ya matatizo mengine katika jamii, na jamii kuzidi kuwaamini zaidi.

 A health worker talks with a woman at her home.

  • Kuleta vikundi vingi pamoja: Vikundi vya kijamii, serikali za mtaa, mashirika yasiyo ya kiserikali ya kitaifa na kimataifa na Wizara ya Afya wote walifanya kazi kwa pamoja. Hii ilisaidia kuhakikisha kuwepo rasilimali na uzoefu wa wadau hao kwa ajili ya kuzuia mlipuko. Kwa vile walifanya kazi pamoja, waliepuka tatizo la asasi moja kufanya kazi inayofanywa na asasi nyingine, au kufanya kazi zinazokinzana.
 A large group of villagers and a health worker meet in a room with a sign reading "Community health depends on clean water."
  • Kuwathamini watu kama rasilimali muhimu kuliko rasilimali zingine zote: Hawakuwalaumu au kuwahukumu wanavijiji kwa matatizo ya afya yaliyowapata, wala kutegemea tu misaada kutoka nje ya jamii yao. Badala yake, walitumia uzoefu wa watu wenyewe kufanya kazi kwa lengo moja. Pia walitumia michezo, nyimbo, majadiliano na mbinu za uelimishaji walizopendelea wanajamii ili kuwakusanya pamoja na kubadilishana maarifa na ujuzi. Shughuli hizi zilizidi kujenga moyo wa kujiamini na hamasa, kadri wanavijiji walivyoendelea kuona jinsi maarifa yao na ushiriki wao ukichangia kutatua matatizo makubwa ya kiafya.

Jinsi dira ya afya ya mazingira ilivyoimarika

Baada ya muda, waelimishaji jamii juu ya afya walikuja kugundua pia kuwa wadudu wanaoeneza magonjwa walikuwa wakizaliana kwenye majalala na sehemu zingine za kutupia taka. Waliendesha mikutano ya kijamii kuhusu kusafisha mitaa na kuboresha maeneo ya kutupa taka. Kila kijiji kiliunda kikundi cha “Wanaharakati wa Afya ya Mazingira” ambao walipanga ratiba ya kila mtu kukusanya taka. Kwa msaada wa mhandisi, wanaharakati wa afya ya mazingira waligeuza majalala ya taka kuwa mashimo salama ya kukusanyia taka, kuzigandamiza katika matabaka kwa utaratibu, na kuzifukia pale shimo linapojaa. Baada ya miaka michache, wanaharakati hawa walianza kuzungumzia kuanzisha mradi wa urejesheaji thamani taka ili kupunguza kiasi kikubwa cha taka kwenye maeneo ya kutupa taka.

Taasisi moja ya kimataifa iliipatia Halmashauri gari kubwa la kuzolea taka na ndoto ya wahamasishaji hao ikatimia. Pesa zilizopatikana kutokana na urejeshaji thamani taka zilichangia kununua mafuta na matengenezo ya gari hilo.

Mwaka 1996, Mradi wa Afya ya Jamii tayari ulikuwa umekwisha jenga mamia ya vyoo na vituo vya maji ya bomba, kuchimba mashimo makubwa mawili ya kukusanyia na kuhifadhi taka, kuanzisha huduma ya urejeshaji thamani taka na kusaidia watu kuanzisha bustani.

 People using a recycling center.

Mnamo mwaka 1997 janga lilitokea: mvua kubwa za Elnino ziliathiri Pwani ya Ekueda. Kwa miezi 6 kulikuwa na pepo kali na mvua nyingi karibu kila siku. Pepo ziliangusha miti, mvua zikageuza vilima kuwa matope, mabonde kujaa na mito kugeuka rangi ya udongo.

Mito ilifurika na kubadili mielekeo, ikiangamiza vijiji vizima. Vyoo, vyanzo vya maji, na maendeleo ya miaka mingi yakaangamizwa na maji.

Kadri vilima vilivyoporomoka, kazi ya Mradi wa Afya ya Watu karibu iangamie navyo. Ili kuelewa vizuri kwa nini hali hii ilitokea, ni lazima tuangalie historia ya eneo hili.

Mlima bila miti ni kama nyumba isiyo na paa

 Rain over a thick forest.
KABLA
 A dry landscape where trees have been cut down.
BAADA

Miinuko na milima kwenye Pwani ya Ekueda hapo awali ilikuwa imefunikwa na misitu mizito ya Tropiki. Miti aina ya mikoko iliota pale ambapo maji ya mito yalipochanganyika na maji ya chumvi kutoka baharini. Misitu ya mikoko iliukinga ukanda wa pwani dhidi ya vimbunga na dhoruba na ilikuwa ni mazalia ya aina nyingi za samaki wa kawaida na viumbe hai vya bahari vingine. Miti ya mianzi pia iliota kando kando ya mito, huku ikizuia kingo za mito zisiliwe na mmomonyoko wa ardhi. Misitu ilikuwa imejaa miti mikubwa ambayo ilitoa vivuli. Mizizi yake ambayo ilishika chini sana ardhini ilisaidia kulinda maji na udongo. Aina nyingine ya miti iliota kwenye miteremko mikali ya milima, huku ikishikilia udongo mahali pale na kuzuia kingo za mlima kumomonyoka au kuanguka. Majani kutoka kwenye miti yalirutubisha ardhi yalipodondoka chini.

Misitu ilikuwa ni makazi ya watu na pia wanyama, ndege na wadudu; mijusi, na wanyama wengi. Watu walijenga nyumba zao kutokana na miti ya mianzi na makuti ya minazi. Kulikuwa na wanyama wa kuwindwa, matunda ya porini ya kula, maji na ardhi yenye rutuba iliyofaa kwa bustani na mashamba madogo.

Lakini zaidi ya miaka 100 iliyopita, miti hiyo mingi ilikatwa kwa ajili ya ujenzi wa reli na nyumba. Wakati huo, kampuni kutoka nchi ya kigeni ilifika na kukata miti iliyokuwa imesalia, na kwa kutumia reli hiyo kusafirisha magogo hadi bandarini kupelekwa nchi za nje. Kwa sababu miti kutoka misitu ya tropiki ni imara sana, iliuzwa kwa bei ya juu. Baada ya miti kwisha, kampuni nayo iliondoka. Reli ilikosa matengenezo na baadaye ilitelekezwa.

Sasa milima kwenye Pwani ya Ekueda huonekana kama jangwa. Vilima vinaonekana tupu, vyenye rangi ya udongo na hakuna kivuli. Wakati wa kiangazi, udongo hupeperushwa na upepo na hewa hujaa vumbi. Wakati wa masika ardhi hugeuka kuwa tope na kingo za milima humomonyoka. Mvua za Elnino zilipopiga mwaka 1997, hakukuwa na miti ya kuwakinga wanavijiji dhidi ya dhoruba zilizoambatana na mvua hizo.

Kutafuta mzizi wa tatizo

Walipoona jinsi mvua zilivyoangamiza vijiji vizima ……. pamoja na mifumo mipya ya maji na vyoo, watumishi wa Mradi wa Afya kwa Jamii waligundua haja ya kufanya kazi zaidi kuzuia majanga kama haya siku za usoni. Juhudi hizo ni pamoja na ujenzi wa mifumo ya maji na kuhimiza usafi wa mazingira, hususan ujenzi na matumizi sahihi ya vyoo.

Kuna usemi kwamba: “mlima bila miti ni kama nyumba isiyo na paa”. Hii ina maana miti hukinga milima dhidi ya mmomonyoko kutokana na upepo na mvua, kama vile ambavyo paa hukinga watu waliopo ndani ya nyumba. Wanaharakati juu ya afya ya mazingira hawa walianza kuliona swala la kuhimiza upandaji miti na kulinda mali asili lina umuhimu sawa na kuhimiza afya ya jamii. Ni mambo mawili yenye lengo na dhumuni moja. Kwa msingi huo, wanaharakati walianzisha mradi wa kupanda miti. Hata hivyo, baadhi ya wanavijiji hawakutaka kupanda miti. Mtu mmoja aliyeitwa Eduardo alikataa kujiunga katika mradi huu wa kupanda miti.

“Ni kazi kubwa mno”, alisema Eduardo. “Wanataka sisi tufanye kazi bila malipo!” Aliwashawishi wanavijiji kutowasikiliza wanaharakati.

 A man speaking.
Kupanda miti ni kazi kubwa. Hatuna mazao wala fedha. Tunahitaji kitu ambacho kitatupatia chakula sasa na siyo katika miaka 10 ijayo.

Mwanaharakati kwa jina la Gloria kutoka kijiji kimoja na Eduardo aliwakusanya watu pamoja na kuanzisha zoezi linaloitwa “Lakini kwa nini....?” ili kumsaidia kila mmoja kutafakari kwa makini, kwa nini walipoteza vyoo vyao na huduma yao ya maji ya bomba.

Kwa kuuliza maswali ya “lakini kwa nini?, Gloria aliwasaidia wanakijiji kuangalia, kwa njia mbalimbali, jinsi gani matatizo yao ya kiafya yalikuwa yanahusiana na mazingira. Mwisho wa majadiliano, wanakijiji wengi walikubali kuwa ni muhimu kupanda miti ili kuzuia mmomonyoko na kulinda ardhi. Lakini Eduardo alikuwa bado hajashawishika. div id=butwhy></div>

Kujifunza kuwa mwanaharakati makini wa afya ya mazingira

Gloria alirudi kwenye kituo chake akiwa amekata tamaa. “Ingawa walielewa umuhimu wa miti, walikataa kuipanda”, alitafakari. “Je nitawezaje kuwashawishi?” Wakati akiwaza jambo hili, nyuki aliruka chumbani na kumshtua. Gloria alimfukuza na baadaye akamwona akiruka kupitia dirishani na kutua nje kwenye maua mekundu ya mti wa karobi. Kitendo hiki kilimpa wazo jipya.

Siku iliyofuata, Gloria aliwakusanya wanakijiji tena. Aliwauliza swali jingine, na Eduardo alikuwa wa kwanza kujibu.

 Villagers speaking with a health worker.
Mnahitaji pesa ili kuboresha maisha yenu sasa -siyo miaka 10 ijayo. Pia mnaamini kuwa ni muhimu kupanda miti. Kuna njia yoyote ya kupata pesa kutokana na miti?
Haa! Bila shaka. Tunaweza kuvuna miti na kuuza mbao. Lakini baada ya miaka 10 kwa sababu miti huchukua muda mrefu kukomaa.

Wanavijiji wengine walifikiria sana na haya ndiyo yalikuwa mawazo yao:

 Villagers speaking with a health worker.
Tunaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali kutoka kwenye miti na kuziuza.
Tunaweza kufuga wanyama ambao watakula majani na mbegu za miti hiyo.
Tunaweza kutengeneza vinyago kutokana na miti hiyo.
Haya yote ni mawazo mazuri na yanatupa sababu zaidi za kupanda miti. Mimi pia nina wazo la kuchangia. Kuna mtu yoyote hapa ambaye anapenda asali?

Gloria aliendelea, “tukipanda miti inayozaa maua ambayo nyuki hupenda tunaweza kuanzisha mradi wa ufugaji nyuki na kuuza asali. Itachukua tu mwaka 1 kwa maua kuweza kuchanua”. Wanakijiji walilipenda wazo hilo. Hata Eduardo alikubali kujaribu kupanda miti kama angeweza kujifunza jinsi ya kurina asali.

Eduardo alimsimamisha Gloria wakati anaondoka. Akamwambia, “Mjukuu wangu alipokuwa anaumwa ugonjwa wa kuharisha, tulimtengenezea dawa kutokana na maua ya mti wa ‘karobi’. Ulimponya kuliko dawa nyingine yoyote ya kisasa. Nafikiri litakuwa wazo zuri kupanda miti. Baadaye tunaweza kutengeneza dawa na kutumia asali tutakayopata ili kuifanya iwe tamu.”

Gloria alirudi kwenye kituo chake akiwa na furaha kuhusu mradi huu mpya. Baada ya kutafakari jinsi mkutano ulivyokwenda, aligundua kuwa haifai yeye kuwaambia wanakijiji cha kufanya. Anatakiwa kujifunza kutokana na mtazamo wao, kusikia mawazo yao na kuelewa mahitaji yao iwapo anataka kuwa mwanaharakati makini wa afya ya mazingira.


Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022