Hesperian Health Guides

Uhamasishaji kwa ajili ya afya ya mazingira

Katika sura hii:

Baada ya miaka mingi ya umasikini na kukosa huduma, wakazi wa maeneo ya vilima vyenye matope kwenye pwani ya Ekueda walikata tamaa. Hawakujua jinsi gani ya kuboresha maisha yao. Kila siku maisha yalikuwa magumu, na haikuwa rahisi kuamini au hata kupanga kwa ajili ya maisha bora ya baadaye.

Kwa kulifanyia kazi tatizo la Kipindupindu ambalo lilihitaji ufumbuzi wa haraka, Gloria na wafanyakazi wa afya waliokoa maisha ya watu wengi. Mafanikio ya waelimishaji jamii wa afya, vikundi vya kijamii, na wanakijiji, kwa kufanya kazi pamoja kuzuia mlipuko huo, walipata hamasa na uzoefu pia wa kukabiliana na matatizo mengine. Mvua za Elnino zilipoharibu kazi zao nyingi, waliweza kujipanga na kukabiliana na athari ya maafa hayo. Baadaye, waliweza kuendelea kutatua matatizo mengine. Kazi yao ya kuboresha afya ya jamii inaendelea, kadri wanavyozidi kuboresha mazingira ya sasa na kupanga kwa ajili ya baadaye.

Fanya juhudi kuelewa sababu za msingi

 Man and women asking and answering questions.

Kwa nini watu wengi waliugua kipindupindu?
Kwa sababu maji yalikuwa na vijidudu vya ugonjwa huo.
Hiki ndicho kitendo kilicho sababisha ugonjwa
Lakini kwa nini maji yalikuwa na vijidudu vya ugonjwa?
Kwa sababu hatuna vyoo ili kuzuia vijidudu hivyo visiingie kwenye maji.
Hii ndiyo sababu ya kimazingira iliyosababisha ugonjwa
Lakini kwa nini hatuna vyoo bora?
Kwa sababu hatuna fedha za kujenga vyoo.
Hii ndiyo sababu ya kiuchumi iliyosababisha ugonjwa

Matatizo ya afya yanaweza kusababishwa na mambo mengi, kama vile vijidudu au bakteria, kemikali za sumu, ajali, njaa, madhara ya baridi au joto kali n.k. Hii ni mifano ya haraka ya sababu za magonjwa. Magonjwa yana visababishi vingi vya haraka lakini zipo pia sababu za msingi.

Kutambua mzizi wa tatizo kunaweza kusaidia kupata ufumbuzi wa muda mrefu. Kwa mfano, kwa kutumia njia ya kuuliza maswali ya “Lakini kwa nini ……?”, kama alivyofanya Gloria, tunaweza kusaidia watu kuelewa jinsi tatizo moja linaweza kuwa na sababu kadhaa za msingi.

Mabadiliko huchukua muda

Maboresho ya afya ya mazingira kawaida si rahisi kupatikana haraka. Katika eneo la Mradi wa Afya kwa Jamii, wafanyakazi wa afya kwanza walitibu wagonjwa kwa kuwaongezea maji mwilini. Pia walijitahidi kuzuia ueneaji wa ugonjwa kwa kuhimiza usafi na usalama wa maji. Halafu walihamasisha jamii kujenga mifumo mipya ya maji na vyoo ili kuzuia milipuko zaidi ya kipindupindu siku za usoni. Lakini ni baada tu ya tufani ya Elinino kuangamiza mifumo mipya waliokuwa wameijenga ndipo walielewa athari za mmomonyoko wa ardhi na mafuriko kutokana na uharibifu wa misitu au ukataji miti hovyo. Walihitaji uelewa wa kiini cha matatizo hayo ili kuweza kufanya mabadiliko ya kudumu.

 woman speaking
Mafanikio haya yote hupatikana hatua kwa hatua. Kuweni na subira. Wakati mwingine mafanikio hupatikana haraka lakini hutoweka haraka pia.

Wakati mwingine, inabidi kujitahidi na kushindwa mara kadhaa kabla ya kufanikiwa. Kawaida ni baada ya kuona njia moja ikishindikana ndipo tunapojifunza njia ipi inafaa na kwa nini.

Uboreshaji wa afya ya mazingira huchukua muda kwa sababu, kawaida huhitaji aina 4 za mabadiliko:

  • Miundo mbinu: mabadiliko kwa ajili ya kuboresha mifumo ya maji, makazi na miundo mbinu mingine ambayo huwa tunajenga wenyewe.
  • Ulaji na manunuzi yetu ya kila siku: mabadiliko katika manunuzi yetu kama vile kuacha kununua vyakula na bidhaa vilivyofungashwa kwenye plasitiki, bidhaa za kufanyia usafi nyumbani zenye kemikali zinazodhuru afya nk.
  • Tabia: mabadiliko katika tabia zetu, kama vile kunawa mikono mara kwa mara, kutumia choo kila mara na kwa usahihi, kutenganisha taka ili taka zinazofaa ziweze kurejeshewa thamani na kutumika tena, au kutumia mbinu mpya za kilimo.
  • Siasa na sera za nchi: mabadiliko katika kiwango cha mamlaka na ushiriki wa watu wa kawaida, mashirika, serikali kuu na vyombo vingine katika kufanya maamuzi ambayo yanahusu mazingira.

Fanya kazi na vijana

Njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa mabadiliko yanadumu kwa muda mrefu ni kuwashirikisha vijana, kwa sababu wataendeleza kile walichojifunza katika maisha yao ya baadaye. Kila mtu, hata awe wa umri gani, anaweza kujifunza na kujaribu mambo mapya.


Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022