Hesperian Health Guides

Sura ya 1: Afya ya wanawake ni suala la jamii

HealthWiki > Pale ambapo Wanawake hawana Daktari > Sura ya 1: Afya ya wanawake ni suala la jamii

Nini maana ya "afya ya wanawake"?
wanawake 4 wakijadili taarifa iliyomo kwenye karatasi


Mwanamke anapokuwa na afya nzuri, anakuwa na nguvu na uwezo wa kufanya kazi zake za kila siku, huweza kutimiza majukumu mengi aliyonayo katika familia na jamii, na huweza kujenga mahusiano ya kuridhisha na wengine. Kwa maneno mengine, afya ya mwanamke huathiri kila eneo la maisha yake. Hata hivyo kwa miaka mingi, huduma za afya ya wanawake, mara nyingi, zimeishia kwenye huduma za ujauzito na kujifungua. Huduma hizi ni muhimu lakini zinaishia tu kugusa mahitaji ya wanawake kama mama. Licha ya uwezo wa kuzaa mtoto, mahitaji ya afya ya mwanamke yamekuwa yakichukuliwa sawa na ya mwanaume.

Kitabu hiki kinatoa picha tofauti kuhusu afya ya wanawake. Kwanza, tunaamini kwamba kila mwanamke anayo haki ya kupata huduma za afya kamilifu kwa kipindi chote cha maisha yake. Huduma ya afya ya mwanamke inapaswa kumsaidia katika nyanja zote za maisha yake — na siyo tu kulenga majukumu yake kama mke na mama. Pili, tunaamini kwamba afya ya mwanamke huathiriwa siyo tu na jinsi mwili wake ulivyoumbika, bali pia na hali halisi ya kijamii, kiutamaduni na kiuchumi pale anapoishi.

Afya nzuri ni zaidi ya kutokuwa na maradhi. Afya nzuri humaanisha ustawi wa mwili mzima wa mwanamke, akili na roho yake.

Wakati ambapo afya ya wanaume pia huathiriwa na mambo hayo, wanawake kwa ujumla wao, hutendewa tofauti. Kwa kawaida wana uwezo mdogo na raslimali chache, na hadhi ya chini katika familia na jamii. Ukosefu huu wa usawa kimsingi humaanisha kwamba:

  • Wanawake wengi zaidi kuliko wanaume wanakabiliwa na umaskini.
  • Wanawake wengi zaidi kuliko wanaume wananyimwa fursa ya kupata elimu na stadi za kuwasaidia kujikimu.
  • Wanawake wengi zaidi kuliko wanaume hawapati taarifa muhimu za afya na huduma za afya kwa ujumla.
  • Wanawake wengi zaidi kuliko wanaume wanakosa uwezo wa kuamua masuala ya msingi kuhusu huduma ya afya.
mama na binti yake wamesimama mlangoni wakati mwanaume akilima na trekta karibu nao

Mtizamo huu mpana zaidi unatusaidia kuelewa sababu za msingi za afya duni ya wanawake. Uboreshaji wa afya ya wanawake unajumuisha kutibu matatizo yao ya afya, pamoja na kubadilisha hali zao za maisha ili waweze kupata uwezo zaidi wa kusimamia afya zao.

Hili litakapotokea, kila mmoja —mwanamke, familia yake na jamii yake wote watanufaika. Mwanamke mwenye afya bora anayo fursa nzuri ya kutumia uwezo wake. Zaidi ya hayo, atakuwa na watoto wenye afya bora zaidi, uwezo zaidi wa kuhudumia familia yake na anaweza kuchangia zaidi katika maendeleo ya jamii yake. Mtizamo wa namna hii unatusaidia pia kutambua kuwa matatizo ya afya ya mwanamke hayamhusu mwanamke peke yake. Afya ya wanawake ni suala la jamii nzima.Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Apr 2018