Hesperian Health Guides

Kufanya kazi kuleta mabadiliko

Hali ya sasa siyo lazima iwe kama ilivyo

Namna ambavyo jamii zimejipanga hulazimisha wanawake wengi kuishi katika umaskini na afya duni. Lakini jamii zingeweza kujipanga kwa namna ambayo huchangia afya badala ya maradhi. Kwa vile sababu za afya duni zimo ndani ya familia, jamii na taifa, mabadiliko ya kuboresha afya ya wanawake lazima yafanyike katika kila hatua mojawapo iliyotajwa.

Kufanya kazi kuleta mabadiliko kwenye familia yako

Unaweza kuboresha afya yako kwa kujifunza kuhusu matatizo ya afya ya wanawake na kwa kufanya mabadiliko kwenye maisha yako mwenyewe na katika familia yako. Ongea na mwenzi wako kuhusu kile ambacho kila mmoja anahitaji ili kuwa na afya bora, ikijumuisha kuzingatia ngono salama na kusaidiana kazi kwa usawa. Unaweza pia kufanya juhudi kuboresha afya na maisha ya baadaye ya watoto wako. Yafuatayo ni baadhiya mawazo:

Kufanya kazi ili kuleta mabadiliko katika jamii.

Unaweza kuboresha afya yako na afya ya wanawake wengine kwenye jamii yako kwa kuwaazima wanawake wenzio kitabu hiki na kwa kuongea nao juu ya matatizo ya afya ya wanawake.

Kwa sababu mazingira ya kijamii huwaathiri kwa njia tofauti, wanawake na wanaume wanaweza kuhitajika kutafuta suluhisho tofauti kwa tatizomoja la kiafya.

Kuongea na wengine inaweza kuwa vigumu. Mara nyingi wanawake hujisikia aibu (kwa mfano, kuongelea sehemu mbalimbali za mwili) au huogopa kwamba wengine watafikiriaje. Hata hivyo kuongea na watu wengine bado ndio njia pekee ya kujifunza zaidi kuhusu matatizo ya afya na kugundua sababu zake. Mara nyingi utaona kwamba wanawake wengine wanayo hofu juu ya matatizo kadhaa na kwamba wako tayari kuyajadili.

Tafuta kikundi kidogo cha wanawake katika jamii yako ili kujadili matatizo ya afya katika jamii yako. Jaribu kuwakaribisha wanawake ambao ni marafiki wa marafiki zako, majirani, au wanawake unaofanya nao kazi pamoja. Mara utakapo ainisha tatizo la afya linalowakumba wanawake wengi, ni rahisi kuweza kukutana tena na kuwaalika wengine ili kulijadili na kujifunza zaidi. Wakati mnapokutana, fikiria kuhusu sababu za msingi za tatizo la afya husika, na kupanga mabadiliko ambayo yanaweza kufanyika katika familia na jamii zenu.

Njia mbalimbali za kufanya kazi na kikundi, kupanga na kutekeleza kwa vitendo ili kuleta mabadiliko, angalia Harakati za kuleta mabadiliko.

a small group of women talking together in a village
Kwa kukutana na kikundi kidogo cha wanawake, unaweza kujifunza zaidi kuhusu tatizo la afya na jinsi ya kuweza kulitatua, kutokana na mawazo ya watu tofauti kama ifuatavyo.
Naumwa mgongo sana siku hizi kwa sababu ya kubeba maji na kuyapandisha mlima hadi nyumbani kwangu. Wahudumu wa afya walishauri kuwa sipaswi kubeba vitu vizito nikiwa mja mzito — hivyo ndivyo mimba ya Mari ilivyoharibika. Lakini bila kubeba maji familia yangu itapataje maji ?
Siyo tatizo tu la wanawake waja wazito! Mimi pia huwa naumwa mgongo. Hatimaye nimefanikiwa kumshawishi mume wangu kuwa ananisaidia kubeba maji kila siku.
Nilimtembelea dada yangu siku moja, na kwenye mtaa wanapoishi, mamlaka ya jiji iliwawekea bomba la maji karibu na nyumbani kwao. Ni msaada mkubwa, kwani hawezi kubeba maji tena kutoka mbali. Kila mtu amelifurahia jambo hilo.
Pengine tungeweza kupata watu wa kutosha kushawishi mamlaka ya mji kutufanyia jambo kama hilo. Lakini tunapaswa kuwa watu wengi. Na tutahitaji kujua ni nani wa kuongea naye, na kuamua mabomba ya maji yawekwe wapi.
Naam, tunaweza kuongea na mwalimu Yusuf. Yeye ni mwalimu na kila mtu anamheshimu. Pengine anaweza kusaidia.


kikundi kidogo cha wanawake na wanaume wakiwa wamesimama pamoja, wakitabasamu

Fikiria pia kuhusu namna ya kuwashirikisha wanaume na wanawake kwenye majadiliano kuhusu afya ya wanawake. Inaweza kuonekana vigumu kuongelea matatizo ya afya ya wanawake mbele ya wanaume, kwa sababu baadhi ya mambo huchukuliwa kama mwiko au siri za wanawake. Lakini kwa vile wanaume kawaida ndio wapo kwenye nafasi za maamuzi, msaada wao ni muhimu sana. Tafuta wanaume wanaounga mkono haki za wanawake, ambao ni mifano mizuri kwa wavulana kuiga, au ambao huaamini katika usawa kati ya wanawake na wanaume.

Yafuatayo ni mambo mengine ambayo yanaweza kuboresha afya kwenye jamii:

  • Kushirikishana taarifa.Tafuta njia za kusambaza taarifa kuhusu matatizo ya afya yaliyoenea katika jamii yako ili kila mmoja aweze kuyaelewa.
  • Kunda vikundi vya kusaidiana Wanawake wenye matatizo yanayofanana — kama vile wanawake waliowahi kubakwa au kunyanyaswa, wanawake wanaonyonyesha, wanawake wenye ulemavu, au wanaojishughulisha na biashara ya ngono — wanaweza kuunda vikundi vya kusaidiana na kufanya kazi pamoja kupambana na matatizo wanayokabiliana nayo.

wanawake wakiwa na watoto wadogo wakitembea kuelekea kwenye nyumba, wakiwa wabeba mifuko

Huko Zimbabwe, mradi wa Musasa ulianzishwa ili kusaidia wanawake ambao waliathirika kutokana na ukatili, hususan ukatili nyumbani ukiwemo ukatili wa kingono. Mradi wa Musasa uligundua kwamba wanawake walikuwa wakipigwa na wenzi wao, na walikuwa hawalindwi na sheria. Watu wengi walisema wanaume wanastahili kuwa na mamlaka juu ya wanawake kwa sababu hivyo ndivyo ilivyokuwa tangu zamani za kale na sasa imekuwa sehemu ya imani ya jamii. Pia walisema kuwapiga wanawake husaidia kuwakumbusha nafasi yao kijamii.

Lengo la Mradi wa Musasa ni kubadili mtizamo huu kwa njia ya elimu kwa jamii na utoaji nasaha kwa wale waliopitia ukatili huu. Kwa njia hii, wanawake, wanaume, walimu, wanafunzi, polisi na wafanyakazi wa afya hujifunza kwamba ukatili ni matumizi mabaya ya madaraka. Mradi wa Musasa ulipanga kutenga nyumba maalum mahali ambapo wanawake na watoto wataweza kukaa wanapokuwa katika hatari.

  • Kufanya kazi kwa bidii ili uweze kuwa na uwezo zaidi wa kujitegemea . Miradi ambayo huwasaidia wanawake kujipatia pato na kuboresha mazingira yao ya kazi, pia huwasaidia kuanza kufanya maamuzi juu ya maisha yao na hivyo kujiongezea hadhi na heshima.

mwanamke akifanya ufumaji
Katika kijiji kidogo huko Mayan Guatemala, wanawake waliunda kikundi cha ufumaji. Waliuza bidhaa zao kupitia duka la ushirika kwa ajili ya bidhaa za sanaa zinazotengenezwa na wanawake katika mji huo. Sasa wanawake hao wana pato kubwa zaidi kuliko wanaume wengi katika eneo hilo. Matokeo yake, wanawake wameweza kujipatia hadhi mpya katika familia zao na jamii, na wana fursa zaidi katika maisha yao.

  • Kuanzisha miradi ya jamii. Kwa mfano, jaribu kutafuta njia kwa kila familia katika jamii kuweza kujipatia chakula cha kutosha, au kuboresha hali ya usafi wa mazingira katika jamii, na kupata maji safi na salama.

miti iliyopandwa katika msitari karibu na nyumba ndogo

Shirika la wanaharakati wa mazingira la Ukanda wa Kijani huko Kenya limewashirikisha wanawake wengi katika kupanda na kulinda miti ambayo huzuia mmomonyoko wa udongo na kutoa nishati. Mafanikio ya wanawake katika kutunza mazingira na kutoa nishati kwa familia zao yawamesaidia kuwajengea moyo wa kujiamini na pia kujikimu.


Kama alivyosema mwanachama mmoja wa shirika hilo la Ukanda wa Kijani, "Misitu yetu ilikuwa ikitoweka kwa sababu ya mahitaji yetu ya kila mara ya kuni. Tuliamua kuwa tunakutana kila wiki ili kupanda mbegu kwenye vyombo, kutengeneza vitalu na kuzungusha uzio, na kuhudumia miche iliyopo kwenye bustani. Pia huwa tunaongea na vikundi vya kijamii na mashule kuhusu mazingira. Kwa njia hii, tunajisaidia sisi wenyewe na pia kuboresha mazingira."

Juhudi ndogo ndogo za gharama nafuu zinaweza kuleta tofauti

Kwa mara ya kwanza unapolitazama tatizo hili, mara nyingi inaonekana ni vigumu sana kuleta mabadiliko. Lakini kwa kweli, jamii zinaweza kufanya maboresho mengi ambayo hayagharimu kiasi kikubwa sana. Kwa mfano, yafuatayo ni mapendekezo yaliyomo kwenye kitabu hiki ya kuzuia au kusaidia kutatua matatizo ya afya ya wanawake.

a woman speaking
Matatizo mengi ya wanawake yanaweza kuepukika au kutibika mapema kama wafanyakazi wengi wa afya wangepewa mafunzo ya kushughulikia matatizo ya msingi ya afya ya wanawake.
  • Kuanzisha mradi wa jamii wa majiko salama. Mara nyingi wanawake huathirika kutokana na maambukizo ya mapafu, kuungua moto, na maumivu ya mgongo. Majiko salama yenye bei nafuu,ambayo ni salama zaidi nayanayotumia nishati kidogo na kutoa moshi kidogo, yanaweza kuzuia matatizo mengi kama haya.
  • Kuanzisha huduma ya usafiri wa dharura. Wanawake wengi hufariki kutokana na matatizo yanayohusiana na ujauzito, kujifungua, na utoaji mimba usio salama. Hivi vifo vingeweza kuzuilika kwa kupata huduma za afya mapema.
  • Uchunguzi wa saratani wenye gharama nafuu unaweza kuepusha vifo vingi vya wanawake kuhusiana na saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti. Saratani inaweza kutibika iwapo itagundulika mapema.
  • Kurahisisha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango na huduma kwa wajawazito wote kabla ya kujifungua. Kufanya hivyo kutaweza kuzuia vifo vingi kutokana na matatizo yanayohusiana na ujauzito, kujifungua, na utoaji mimba usio salama
  • Kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya wote juu ya afya ya wanawake. Wanapaswa kufundishwa jinsi ya kufanya uchunguzi kwenye nyonga, uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi na kutumia vipimo vya Pap na MVA, uchunguzi wa matiti, na jinsi ya kutoa huduma ya unasihi. Pia wanapaswa kufundishwa jinsi ya kutumia dawa kwa ajili ya afya ya wanawake

Kufanya kazi ili kuleta mabadiliko katika nchi yako

Unaweza kuboresha afya yako na afya ya wanawake katika nchi yako, kwa kufanya kazi pamoja na vikundi au wadau katika sehemu tofauti za nchi. Kwa kufanya kazi pamoja, unaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa namna ambavyo serikali inawatendea wanawake na afya zao. Kwa mfano, vikundi vya jamii na mashirika yasiyo ya kiserikali yanaweza kushinikiza serikali kuwadhibu vikali wanaume wanaobaka au kudhalilisha wanawake, au kuwezesha upatikanaji wa huduma ya utoaji mimba salama. Au unaweza kushinikiza kupitishwa kwa sheria zinazowawezesha wanawake kurithi mali — ili wasilazimike kuwategemea wanaume.

Kushika hatamu ya afya zetu

Kama "afya ya wanawake" ilivyo na maana pana zaidi ya afya ya uzazi, pia ina maana zaidi ya upatikanaji wa huduma za afya. Ili kuwa na afya bora, wanawake wanahitaji fursa ya kufanya maamuzi muhimu kwa lengo la kuwa na afya bora. Na pia wanahitaji mgao wao wa raslimali zilizopo kwenye jamii zao na duniani, kwa kuzingatia haki na usawa.

Kwa kuungana na wanawake na wanaume wengine katika harakati za kuboresha afya, tunaweza kudai kwa nguvu zaidi fursa za kuishi maisha yenye afya bora, furaha na kamilifu zaidi — pasi na magonjwa, maumivu, na woga wa mara kwa mara.Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Feb 2018