Hesperian Health Guides

Sababu za afya duni kwa wanawake

Katika sura hii:

Ni rahisi kutaja moja kwa moja sababu nyingi za matatizo ya afya ya wanawake. Kwa mfano, tunaweza kusema kwamba magonjwa ya ngono husababishwa na vijidudu tofauti; lishe duni hutokana na kutokula chakula kizuri cha kutosha; na matatizo kuhusiana na ujauzito husababishwa na ukosefu wa huduma za kutosha za mama wajawazito. Lakini nyuma ya sababu hizi za moja kwa moja, kuna sababu mbili za msingi — umaskini na hadhi ya chini ya wanawake kijamii — ambazo huchangia matatizo mengi ya afya ya wanawake.

Umaskini

Kwa kila wanawake 3 duniani, 2 ni maskini. Siyo tu kwamba wanawake wana uwezekano mkubwa wa kuwa maskini kuliko wanaume, lakini mara nyingi wao ni miongoni mwa maskini wa kupindukia. Mamilioni ya wanawake hujikuta kwenye mzunguko wa umaskini unaoanza hata kabla ya kuzaliwa. Watoto wanaozaliwa na akina mama ambao walikosa lishe borakabla na wakati wa ujauzito, wana uwezekano mkubwa wa kuzaliwa wakiwa wadogo na kudumaa. Katika familia maskini, wasichana wana uwezekano mkubwa wa kupata chakula kidogo kuliko kaka zao, na hii huchangia udumavu zaidi. Wasichana mara nyingi hupatiwa elimu kidogo au hukosa elimu kabisa, hali ambayo huwalazimika kufanya kazi zisizo na utaalam na kupokea ujira mdogo kuliko wanaume (hata kama wanafanya kazi ya aina moja). Wakiwa nyumbani, kazi zao za kila siku hazina malipo. Uchovu, lishe duni na ukosefu wa huduma nzuri wakati wa ujauzito humweka mwanamke na watoto wake katika hatari ya kuwa na afya duni. Umaskini humlazimisha mwanamke kuishi katika mazingira ambayo huweza kumsababishia matatizo makubwa ya kimwili na kiakili. Kwa mfano, mara nyingi wanawake wenye hali duni:

mwanamke mwenye hali duni akiwa amekaa nje ya kibanda chake
  • huishi kwenye nyumba duni, zenye huduma duni za usafi wa mazingira au bila huduma hizo (hususan choo) au maji safi.
  • hawana chakula cha kutosha na hulazimika kutumia muda mwingi na nguvu nyingi kutafuta chakula wanachoweza kumudu.
  • hulazimika kukubali kazi hatarishi au kufanya kazi kwa muda mrefu.
  • hawawezi kutumia huduma za kiafya hata kama ni za bure kwa sababu hushindwa kuacha kazi zao au majukumu ya familia.
  • Hutumia muda wao mwingi katika mihangaiko ya kujitafutia chakula na riziki, na hivyo kukosa muda na nguvu za kuweza kushughulikia mahitaji yao, kupanga kwa ajili ya maisha yao,au kujifunza stadi mpya za kujikimu
  • hulaumiwa kwa umaskini wao na kuwafanya kujihisi kuwa wao sio muhimu wakilinganishwa na wale wenye hali nzuri zaidi.


Mara nyingi umaskini huchangia wanawake kuingia kwenye mahusiano tegemezi ili waweze kuishi. Iwapo mwanamke anamtegemea mwanaume kiuchumi au kwa ajili ya matunzo ya watoto, anaweza kufanya mambo yanayohatarisha afya yake ili kumfurahisha mwanaume. Kwa mfano, anaweza kuruhusu mwanaume kumfanyia ukatili wa kijinsia au kumfanyisha ngono isiyo salama kwa sababu ya kuogopa kupoteza msaada wake wa kiuchumi.

mwanamke mwenye huzuni akiwa amesimama peke yake katika hali ya  upweke wakati wenzake wakimnyoshea kidole

Hadhi ya chini ya wanawake kijamii

Hadhi ya mtu katika jamii ni umuhimu wa mtu alionao kwenye familia au jamii yake. Hadhi huathiri namna mwanamke anavyotendewa, jinsi anavyojithamini mwenyewe, aina ya kazi anazoruhusiwa kufanya, na aina ya maamuzi anayoruhusiwa kufanya. Katika jamii nyingi duniani, wanawake wana hadhi ya chini kuliko wanaume. Hadhi ya chini ya wanawake husababisha ubaguzi — yaani kutendewa au kunyimwa baadhi ya vitu kwa sababu tu ni wanawake. Ubaguzi huweza kujitokeza kwa namna tofauti katika jamii mbalimbali lakini daima huathiri afya ya mwanamke.

Kupendelea watoto wa kiume kuliko wakike. Familia nyingi huthamini watoto wa kiume kuliko wasichana kwa kudhani wavulana wanaweza kuchangia zaidi kwenye utajiri wa familia, kusaidia wazazi wakati wa uzeeni , kusimamia mila na taratibu zingine baada ya wazazi kufariki dunia, na kuendeleza jina la familia. Matokeo yake, wasichana hunyonyeshwa kwa muda mfupi, hupewa chakula na matunzo ya afya kidogo zaidi kuliko wa kiume, na hupatiwa elimu kidogo au huikosa kabisa.

Kwa sababu ya kazi nyingi wanazofanya wanawake hazitambuliwi kisheria, mara nyingi wanakosa ulinzi wa kisheria sehemu za kazi.

Ukosefu wa haki za kisheria au uwezo wa kufanya maamuzi. Katika jamii nyingi, mwanamke hawezi kumiliki au kurithi mali, kujitafutia pesa au kupata faida. Iwapo mwanamke amepata talaka, haruhusiwi kwenda na watoto wake au mali zake. Hata kama mwanamke anayo haki ya kisheria, mila za jamii yake zinaweza kumruhusu kuwa na udhibiti mdogotu juu ya maisha yake. Mara nyingi mwanamke hawezi kuamua jinsi gani mali ya familia itumike au ni lini apate huduma ya afya. Mwanamke hawezi kusafiri au kushiriki katika maamuzi ya jamii bila ruhusa ya mume wake.

Mwanamke anaponyimwa mamlaka kwa njia hizi, hulazimika kuwategemea wanaume ili kuishi. Matokeo yake, hawawezi kudai kwa urahisi mambo muhimu yanayochangia afya njema , kama vile uzazi wa mpango, ngono salama, lishe bora, huduma za afya, na kutofanyiwa ukatili.

Wanawake ni nusu ya idadi ya watu wote duniani, lakini hufanya kazi saa 2 kwa kila saa 3 za kazi duniani, huambulia asilimia 10 tu ya mapato yote duniani, na humiliki theluthi tu ya mali zote duniani.

Kuwa na watoto wengi au kuzaa bila kupanga uzazi. Ubaguzi dhidi ya wanawake unaweza pia kuwasababishia kupata mimba mara kwa mara kwa kudhani watoto wengi ndio njia pekee ya wao au wenzi wao kupata hadhi.

Katika mazingira haya, wanawake hujikuta wakiwa na afya duni na kupata huduma duni za afya. Mara nyingi pia huikubali hadhi yao ya chini kwa sababu wamelelewa kujiona wenye hadhi ya chini kuliko wanaume. Wanawake huweza kukubali kushi na hali duni ya afya kama sehemu ya maisha yao ya kila siku, na kutafuta msaada tu pale matatizo ya afya yanapozidi, au kuhatarisha maisha yao.

Mfumo wa matibabu haukidhi mahitaji ya wanawake

Umaskini na ubaguzi katika familia na jamii siyo tu husababisha matatizo ya afya zaidi kwa wanawake, bali pia husababisha uwezekano wa mfumo wa afya kutoa huduma pungufu zisizolingana na mahitaji ya wanawake. Sera za serikali na mfumo wa uchumi kidunia unaweza kuchangia kukuza tatizo hili.

Katika nchi maskini, watu wengi hawawezi kupata huduma za afya za aina yoyote. (Kwenye jedwali hapo chini, inaelezwa sababu moja kwa nini tatizo hili limekuwa baya zaidi miaka hivi karibuni.) Na kwa sababu ya ubaguzi dhidi ya wanawake, kiasi kidogo cha fedha kilichopo huenda hakitatumika kwa mahitaji ya afya ya mwanamke. Kwa hivyo, mwanamke anaweza asipate huduma nzuri za afya hata kama atakuwa na uwezo wa kumudu huduma hizo. Baadhi ya huduma za afya ya uzazi zinaweza kuwa zinatolewa, lakini ili kupata huduma zote anazohitaji, atalazimika kusafiri hadi mijini au hata nje ya nchi.

Katika nchi nyingi, utaalam unaohitajika kuwahudumia wanawake huchukuliwa kama “utalaam maalum” na huduma hutolewa tu na madaktari. Hata hivyo, sehemu kubwa ya huduma hizi ingeweza kutolewa kwa gharama nafuu na wafanyakazi wa afya wa kawaida waliopewa mafunzo.

Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Feb 2018