Hesperian Health Guides

Wanawake wapo katika hatari kubwa zaidi ya magonjwa na afya duni

Katika sura hii:

Kwa sababu mwili wa mwanamke ni tofauti na mwili wa mwanaume, na kwa sababu ya tofauti za msingi kati ya wanaume na wanawake, wanawake wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya maradhi na afya duni. Yafuatayo ni baadhi ya matatizo ya afya yanayowaathiri wanawake zaidi:

Ukosefu wa lishe ya kutosha unaweza kumfanya msichana asikue vizuri na kusababisha matatizo makubwa ya afya.

Lishe duni

Lishe duni ndio tatizo kuu linalokwaza afya za wanawake katika nchi maskini. Kuanzia utotoni, mara nyingi msichana anapewa chakula kidogo kuliko mvulana. Matokeo yake, anaweza kukua polepole sana na mifupa yake inaweza isikue vizuri (jambo ambalo baadaye linaweza kusababisha matatizo wakati wa kujifungua). Tatizo huwa kubwa zaidi anapoingia umri wa kuzaa kwa sababu mahitaji yake ya lishe huongezeka kadri kazi zake zinavyongezeka, anapoanza kupata hedhi, kubeba mamba na kunyonyesha.

Bila ya lishe bora, afya yake inaweza kuanza kudorora, pamoja na kukumbwa na uchovu, mwili kukosa nguvu, na upungufu wa damu. Iwapo mwanamke ambaye tayari an utapiamlo atabeba mimba, anakabiliwa na hatari zaidi wakati wa kujifungua kama vile kutokwa na damu nyingi, maambukizo au kuzaa mtoto mdogo mno.

Wanawake wakiongea
Mfanyakazi wa afya aliniambia natakiwa kunywa maziwa na kula mboga za majani kwa wingi. Lakini huwa natenga maziwa yote kwa ajili ya mume wangu na mtoto wangu wa kiume, na hatuna pesa za kununua mboga za majani.

Afya ya mwanamke haiwezi kutenganishwa na hadhi yake kijamii. Wanawake wengi wa vijijini huko India, hunywa maziwa kidogo kuliko waume zao na vijana wa kiume, na huwa wanakula baada ya wanaume kuhudumiwa. Jambo hili kwa kawaida huwaachia wanawake milo midogo na pia linaelezea jinsi gani wanavyothaminiwa


— CHETNA, Ahmedabad, India

Matatizo ya afya ya uzazi

Magonjwa yaenezwayo kwa ngono (STDs), vikiwemoVVU na UKIMWI. Kimaumbile mwanamke yupo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizo ya ngono na VVU kuliko mwanaume. Hii ni kwa sababu mbegu za mwanaume hubakia ndani ya mwili wa mwanamke na vijidudu vilivyomo vinaweza kupenya ute laini ukeni na kuingia kwenye damu. Na kwa vile mara nyingi mwanamke haoneshi dalili za maambukizo, anaweza asipate matibabu.

Kwa vile wanawake mara nyingi hulazimika kufanya ngono bila ya ridhaa yao, maambukizi kupitia ngono ni suala la kijamii.

Lakini tatizo hasa ni la kijamii. Mara nyingi wanawake hawana uwezo wa maamuzi kuhusu mahusiano ya kingono na hawawezi kukataa ngono isiyo salama. Matokeo yake, mamilioni ya wanawake hupata maambukizo kwa njia ya ngono kila mwaka na zaidi ya milioni 17 tayari wana VVU. Bila ya kupatiwa matibabu, maambukizo ya ngono (STDs) huweza kusababisha maumivu makali kiasi cha kushindwa kufanya kazi, magonjwa ya nyonga (PID), ugumba, matatizo wakati wa kujifungua na ongezeko la hatari ya saratani ya shingo ya kizazi. VVU visipotibiwa husababisha UKIMWI na hatimaye kifo.

mwanamke mjamzito akiwa na watoto wengine 6

Mimba za mara kwa mara

Sehemu nyingi duniani, theluthi moja hadi nusu ya wasichana hujikuta wamekuwa wamama kabla ya kufikisha umri wa miaka 20. Bila uzazi wa mpango, wengi wao hawawezi kupata muda wa kupumzika kati ya uzao mmoja na mwingine ili kujenga afya zao. Hili linamweka mwanamke katika matatizo makubwa ya kiafya na matatizo mengine wakati wa ujauzito na kujifungua. Kuzaa mara kwa mara pia humaanisha kwamba anao uwezo mdogo kujikimu, kujipatia elimu na kujifunza stadi za kumsaidia katika maisha yake.

Kila dakika, mwanamke mmoja hufariki kutokana na tatizo linalohusiana na ujauzito.

Matatizo kuanzia ubebaji mimba hadi kujifungua

Miaka 40 iliyopita, idadi ya vifo vya watoto imepungua kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo idadi ya wanawake wanaokufa kutokana na mimba na kujifungua bado haijapungua . Kila dakika moja, mwanamke mmoja hufa kutokana na tatizo linalohusiana na ujauzito. Na kwa mwanamke moja ambaye anafariki wakati wa kujifungua, wanawake 20 hupata matatizo ya afya ya kudumu kutokana na majeraha makali na maambukizo. Hii inamaanisha kwamba baada ya muda, takribani robo ya wanawake wote wanaoishi katika nchi maskini wataathirika zaidi kutokana na matatizo yanaohusiana na ujauzito na kujifungua.

Kila mwaka wanawake 70,000 hufariki kutokana na utoaji mimba usio salama.

Utoaji mimba usio salama

Mwanamke anapojaribu kutoa mimba kwa njia isiyo salama anakuwa anahatarisha maisha yake. Lakini kila siku takribani wanawake na wasichana 60,000 hujaribu kutoa mimba kwa njia zisizo salama kwa sababu hawana njia nyingine iliyo salama. Wengi hubakia bila uwezo wa kupata watoto tena, au na maumivu makali ya kudumu, maambukizo na matatizo mengine ya afya.

Ukeketaji

Kitendo katili cha ukeketaji, ambapo baadhi ya sehemu au sehemu yote ya uke wa msichana hukatwa na kuondolewa, husababisha matatizo makubwa ya afya. Matatizo haya ni pamoja na maambukizo kwenye nyonga na kwenye njia ya mkojo, matatizo ya kingono na kihisia, na matatizo wakati wa kujifungua. Licha ya matatizo haya, bado ukeketaji unaendelea kwa kiasi kikubwa. Kila mwaka takribani wasichana milioni 2 hukeketwa, wengi wao kutoka Afrika lakini pia Mashariki ya Kati na Asia.

Wanaume na wanawake hupata magonjwa mengi yanayofanana, lakini wanawake huweza kuathirika tofauti.

Matatizo ya kiafya kwa ujumla

Wanawake wako katika hatari kubwa ya kuathiriwa na baadhi ya matatizo ya afya kuliko wanaume kutokana na kazi wanazofanya, lishe duni, au kwa sababu ya kuchoka sana. Ugonjwa unaweza pia kusababisha madhara tofauti kwa mwanamke ikilinganishwa na mwanaume. Kwa mfano, mwanamke anayeugua ugonjwa unaodhoofisha mwili wake, au kuharibu umbile au sura yake unaweza kusababisha akataliwe na mumewe.

Wanawake wanapougua, huwa na uwezekano mdogo kutafuta na kupata tiba hadi pale wanapozidiwa. Kwa mfano, ugonjwa wa kifua kikuu (TB) huwaambukiza wanaume na vile vile wanawake, lakini ni wanawake wachache kuliko wanaume wanaopata matibabu. Takribani wanawake 3000 hufa kila siku kutokana na ugonjwa wa kifua kikuu (TB) — kwa uchache theluthi moja (⅓) ya hao hawakupata tiba sahihi, au hata hawakujua kamwe iwapo walikuwa na ugonjwa huo. Matatizo mengine ya afya ambayo zamani yaliwaathiri zaidi wanaume sasa yamekuwa hatari kwa wanawake pia. Kwa mfano, wanawake wengi wanaathirika sana kutokana na uvutaji wa sigara au matumizi ya pombe kupita kiasi.

Mwanamke hukumbana na hatari ya afya akiwa kazini kwake, ndani na nje ya nyumbani kwake. Kufanya kazi saa nyingi na kazi nyingi hudhoofisha miili yao kiasi cha kushindwa kupambana na magonjwa.

mwanamke akifanya kazi kwenye shamba la mpunga

Madhara kazini

Wanawake hukabiliana na matatizo ya afya kila siku kutokana na kazi wanazofanya. Wakiwa nyumbani, magonjwa ya mapafu kutokana na moshi au kuungua kwa moto ya kupikia, ni mambo ya kawaida kiasi kwamba huchukuliwa kuwa matatizo makuu yanayohusiana na kazi ya wanawake. Magonjwa yanayoambukizwa kupitia maji nayo yanaonekana ya kawaida kwa sababu ya muda mwingi wanawake wanaotumia kufua nguo, kukinga/kuteka maji au kusimama ndani ya maji wakati wa kilimo.

Mamilioni ya wanawake wanaofanya kazi mbali na nyumbani huathirika kutokana na matatizo ya afya kwa sababu ya mazingira yasiyo salama sehemu za kazi. Na wanaporudi nyumbani kutoka kazini, hulazimika kuendelea kufanya kazi nyumbani, na hivyo huishia kufanya kazi mara mbili tofauti na wanaume. Jambo hili husababisha uchovu zaidi na hatari ya magonjwa.

Matatizo ya kiakili yanaweza kufikia hali tete kama yalivyo matatizo mengine ya afya.

Matatizo ya afya ya akili

Wanawake na wanaume wanakaribia kuwa na kiwango sawa cha hatari ya kuwa na matatizo ya akili. Hata hivyo, msongo mkubwa wa mawazo huwaathiri wanawake wengi zaidi kuliko wanaume. Mara nyingi huwaathiri wanawake maskini, ambao wamekumbwa na upotevu mkubwa kimaisha, au vurugu, au wale ambao jamii zao zimeharibiwa au kukumbwa na mabadiliko makubwa. Lakini wanawake wanaokumbwa na tatizo lolote la kiakili wana uwezekano mdogo wa kupata msaada ikilinganishwa na wanaume.

Mara nyingi wanawake wanapofanyiwa vitendo vya ukatili, huwa ni kutoka kwa wanaume wanaowajua. Lakini mara nyingi vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya wanawake haviripotiwi, na ni mara chache wanaume husika kuadhibiwa.

mwanaume akimpiga mwanamke wakati watoto 2 kwa woga mkubwa wakiangalia

Ukatili wa kijinsia

Mara nyingi ukatili wa kijinsia hauchukuliwi kama tatizo la kiafya. Lakini ukatili wa kijinsia unaweza kusababisha majeraha makubwa, matatizo ya afya ya akili, ulemavu na hata kifo. Wasichana wengi hufanyiwa ukatili wa kingono na wanafamilia au hata rafiki zao. Wanawake wengi hulazimishwa kufanya ngono au hata kufanyiwa ukatili wa kimwili na wapenzi wao. Vitendo vya ubakaji na ukatili wa kijinsia kwa jumla vimekuwa mambo ya kawaida wakati wa vita. Ingawa aina hizi za ukatili wa kijinsia hutokea karibu sehemu zote duniani, mara nyingi vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake haviripotiwi na hatua zinazostahili kuchukuliwa. Hii ni kwa sababu polisi na wengine huwalaumu wanawake badala ya wanaume kwa kusababisha vitendo hivyo.




Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Feb 2018