Hesperian Health Guides

Namna ya kupata huduma bora

Katika sura hii:

Kuna maamuzi mengi ya kufanya unapokuwa na tatizo la kiafya. Uamuzi mmojawapo ni aidha kwenda kumwona mfanyakazi wa afya na aina gani ya mfanyakazi wa afya unahitaji. Kama kuna njia zaidi ya moja ya kuweza kutibu tatizo, unapaswa kufikiria faida na hasara za kila njia itakayotumika kabla ya kufanya uamuzi. Utaweza kufanya maamuzi mazuri na kupata huduma nzuri iwapo utashirikiana kwa karibu na daktari, muuguzi au mfanyakazi wa afya katika kutatua tatizo lako la kiafya.

Elewa unachotorajia

Utaweza kuwa mstari wa mbele kushughulikia tatizo lako la afya ikiwa umejiandaa na unajua unachotarajia unapokwenda kutafuta huduma ya afya.

Maswali kuhusu afya yako

Ni vizuri kujifunza kadri iwezekanavyo kuhusu tatizo lako la afya kabla ya kwenda kutafuta tiba. Ukisoma kitabu hiki,unaweza kuelewa tatizo lako la afya na hata mambo ambayo yanaweza kuwa yanalisababisha. kuelewa matatizo ya afya yako na uwezekano wa sababu zake.

Mara nyingi huwa inasaidia kufikiria mapema maswali ambayo ungependa kuuliza kabla ya kwenda kupata huduma za afya

Daktari, muuguzi au mfanyakazi wa afya atakayekuhudumia anapaswa kukuuliza kuhusu tatizo ulilo nalo sasa na kuhusu afya yako ya mwanzoni. Jaribu kutoa taarifa kamilifu, hata kama hutajisikia vizuri kufanya hivyo, ili anayekuuliza maswali aweze kuelewa kwa kiasi kikubwa kuhusu afya yako. Kila mara mweleze mfanyakazi wa afya dawa au tiba nyingine yoyote unayotumia, ikiwemo aspirini na njia za uzazi wa mpango.

Unapaswa pia kupata fursa ya kuuliza swali lolote ulilo nalo. Ni muhimu kuweza kuuliza maswali mengi kadri iwezekanavyo ili kukusaidia kufanya uamuzi mzuri kuhusu namna ya kushughulikia tatizo lako la afya. Ikiwa maswali yako yatakuwa bado hayajajibiwa, unaweza kujiuliza:

mwanamke akijiuliza maswali
  • Ni njia zipi tofauti ambazo zinaweza kutumika kutibu tatizo hili?
  • Je, tiba hii itakuwa na matokeo gani? Je, ina madhara yoyote?Je, nitapona? Au je, tatizo litajirudia?
  • Je, vipimo pamoja na matibabu vitagharimu kiasi gani?
  • Ni lini nitapata nafuu?
  • Kwa nini tatizo hili lilitokea na ninaweza kufanya nini kuzuia lisitokee tena?


Madaktari wengi na wauguzi wanaweza kushindwa kutoa taarifa nzuri, au wanaweza kubanwa na kazi nyingi kiasi cha kutoweza kuyajibu maswali yako. Hata hivyo endelea kuonesha heshima na kuwa na msimamo imara. Wanapaswa kuyajibu maswali yako mpaka uelewe. Ikiwa huelewi, siyo kwa sababu wewe ni mpumbavu, bali kwa sababu hawaelezi vizuri kiasi cha wewe kuelewa.

Uchunguzi

Ili kuweza kujua kinachokusibu na ukubwa wa tatizo, utahitaji kufanyiwa uchunguzi. Uchunguzi unajumwisha kuangalia, kusikiliza na kugusa eneo la mwili lenye tatizo. Kwa matatizo mengi utahitaji tu kuvua nguo sehemu inayohusika. Kama utaona ni vizuri zaidi, unaweza kumwomba rafiki yao mwanamke au muuguzi mwanamke naye awepo kwenye chumba unapokuwa unafanyiwa uchunguzi.

Vipimo

mfanyakazi wa afya akimfanyia uchunguzi mwanamke kwenye tumbo kwa kutumia mashine ya ultrasound
Mashini ya ultrasound

Vipimo vinaweza kutoa taarifa zaidi juu ya tatizo la afya. Vipimo vingi hufanyika kwa kuchukua sampuli kidogo ya mkojo, kinyesi au makohozi na kuipeleka kwenye maabara. Au sindano hutumika kutoa damu kidogo kutoka kwenye kidole au mkono kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi. Vipimo vingine vya kawaida ni pamoja na:

  • Kuchukua majimaji kutoka ukeni ili kuchunguza maambukizi ya magonjwa ya ngono.
  • Kukwangua seli za mlango wa mji wa mimba(kizazi) ili kuchunguza saratani (kipimo hiki huitwa pap test).
  • Kuchukua tishu kutoka kwenye uvimbe ili kuchunguza saratani (biopsy).
  • Kutumia eksirei au Ultrasound ili kuchunguza ndani ya mwili. Eksirei huweza kutumika kuangalia mifupa iliyovunjika, kuona maambukizo makubwa kwenye mapafu na baadhi ya saratani. Epuka kufanyiwa eksirei wakati wa ujauzito. Kipimo cha Ultrasound kinaweza kutumika wakati wa ujauzito kuchunguza mtoto aliye tumboni. Vipimo hivi havisababishi maumivu.

Kabla ya kufanyiwa kipimo chochote, kwanza ulizia kuhusu gharama. Mwulize daktari, muuguzi au mfanyakazi wa afya anachohitaji kujua kutokana na kipimo hicho na nini kitatokea iwapo kipimo hicho hakitafanyika.

Mlete rafiki au mwanafamilia

a woman speaking to a health worker while a younger woman lies in a bed
Mimi ni mama yake. Naweza kujibu baadhi ya maswali yako.
Kama mwanamke anaumwa sana, mtu mwingine anweza kwenda nae.

Watu wengi hupata hofu kwenda kutibiwa – hata kwa magonjwa ambayo si makubwa. Na mtu anapoumwa, inaweza kuwa vigumu zaidi kudai huduma ya afya anayohitaji. Kama atakuwepo mtu mwingine wa kumsindikiza mgonjwa, anaweza kutoa msaada mkubwa.

Rafiki anaweza:

  • Kusaidia kuwangalia na kuwatunza watoto wa mgonjwa.
  • Kusaidia kufikiria maswali ya kuuliza, kumkumbusha mgonjwa kuyauliza maswali hayo, na kuhakikisha kuwa yanajibiwa.
  • Kusaidia kujibu maswali kama mgonjwa anaumwa sana na hawezi kuongea.
  • Kukaa naye wakati anasubiri vipimo ili kumuondolea upweke
  • Kubaki na mgonjwa atakapokuwa anafanyiwa uchunguzi, kumfariji, na kuhakikisha kuwa daktari anamtendea kwa heshima.


Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Feb 2018