Hesperian Health Guides

Sura ya 3: Mfumo wa utoaji huduma za afya

HealthWiki > Pale ambapo Wanawake hawana Daktari > Sura ya 3: Mfumo wa utoaji huduma za afya


mfanyakazi wa afya akiongea na mama mwenye mtoto ofisini

Pale wasaidizi wa afya waliopitia mafunzo nao watakapoanza kutoa huduma za afya za msingi kwenye jamii,kila mtu atapata tiba bora kwa gharama nafuu.

Maeneo mengi duniani yana mifumo ya huduma ya afya tofauti. Kwa mfano, kuna wafanyakazi wa afya wa jamii au wasaidizi wa afya, wakunga na watalaam wa tiba za jadi, madaktari na wauguzi. Wote hao wanaweza kufanya kazi zao wakiwa nyumbani kwao, kwenye kliniki au vituo vya afya au hospitalini. Wanaweza kuwa katika sekta binafsi (wakitoza ada kwa huduma zao) au wanaweza kuwa wanagharamiwa na jamii zao, serikali, taasisi za kidini na nyinginezo. Wakati mwingine huwa wamefundishwa vizuri na huwezeshwa kutoa huduma vizuri, na wakati mwingine sivyo. Wote hao kwa pamoja ni sehemu muhimu ya mfumo wa utoaji huduma za afya.

Watu wengi hutumia tiba mchanganyiko wa dawa za kisasa na dawa za asili ili kujitibu wenyewe. Mara nyingi hiki tu ndicho wanachokifanya. Lakini wakati mwingine, hujikuta wakihitaji huduma kutoka mfumo rasmi wa huduma za afya.

Ni bahati mbaya kuwa wanawake wengi hawapati huduma bora za afya. Wakati mwingine hawana fedha za kutosha kwenda katika kliniki nzuri au kununua dawa. Au wakati mwingine, kunakuwa hakuna wafanyakazi wa afya katika maeneo yao. Hata kama wanaweza kwenda kliniki, inaweza kuwa vigumu kuongea na wafanyakazi wa afya kuhusu matatizo yao. Wakati mwingine kliniki au hospitali hazina huduma wanazohitaji.

Sura hii inatoa mawazo kuhusu jinsi wanawake wanavyoweza kupata ushauri na huduma bora za kiafya. Pia inapendekeza njia ambazo wanawake wanaweza kuzitumia kwa pamoja kuchangia mabadiliko katika mfumo wa utoaji huduma za afya ili uweze kukidhi mahitaji yao.


Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Feb 2018