Hesperian Health Guides

Jitihada za kuleta mabadiliko

Mamilioni ya watu duniani huteseka na kufariki kutokana na magonjwa ambayo yangeweza kuzuilika au kutibika iwapo wangepata huduma bora za afya. Na hata pale ambapo huduma za afya zinapatikana, kuna vikwazo vingi vinavyowafanya hasa wanawake wenye hali duni kushindwa kuzipata huduma hizo.

Lakini kwa pamoja, wafanyakazi wa afya na vikundi vya wanawake wanaweza kuchangia kuleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa utoaji wa huduma za afya. Wanaweza kuiona changamoto hiyo kama fursa badala ya kikwazo katika kutatua matatizo yao ya kiafya. Mfumo wa utoaji huduma za afya hauwezi kujibadili wenyewe. Utaweza kubadilika pale watu watakapodai mabadiliko na kutoa njia bunifu za kufikisha huduma za afya zinazohitajika kwa watu wote.

Hatua moja nzuri ya kuanzia ni kujadili-wanawake na wanaume- matatizo ya afya yanayoikabili jamii yako, likiwemo tatizo la ukosefu wa upatikanaji wa huduma bora za afya.

kikundi cha wanawake wakiwa na watoto wadogo, wamekaa kwenye benchi na
Ninaishi mbali sana. Kama kungekuwepo na mfanyakazi wa afya karibu, tungeokoa pato la familia la wiki 2 ambalo huwa natumia kila mara ninapokuja hapa.
Natamani wasingeishiwa nyezo za uzazi wa mpango(majira). Nilipata ujauzito mwaka jana kwa sababu kliniki iliishiwa nyenzo hizo, na siwezi kumudu gharama ya kununua nyingi kwa mpigo mara wanapokuwa nazo.
Hawa madaktari wa mjini hutudharau sana.Heri ningejisikia vizuri iwapo watu wetu wa kijijini wangesaidia kuendesha kliniki hii.
Natamani wangetufanyia kipimo cha saratani ya shingo ya kizazi (pap test) hapa. Nimesikia kipimo hicho ni muhimu sana lakini siwezi kumudu gharama ya kukifuata jijini.
Ningependa viwepo vyumba tofauti mahali ambapo tunaweza kufanyiwa uchunguzi bila watu wengine kusikiliza.
Sitaki mwanaume kunifanyia uchunguzi. Natamani kungekuwa na wafanyakazi wa afya wanawake kuifanya kazi hiyo.
Ningependa kiliniki iwe wazi jioni, baada ya kumaliza kazi zangu.
Natamani wangenieleza tatizo ni nini. Hii ni mara ya 4 mwaka huu kukojoa damu. Kwa nini tatizo hili linajirudia?
Kawaida tunatumia muda mrefu kusubiri.Kama kila mtu angeulizwa moja kwa moja anataka nini, basi wale ambao ni wagonjwa hasa wangehudumiwa mapema.

Wanawake wanaweza pia kufanya kazi pamoja ili:

  • Kusaidia kila mwanajamii kujifunza kuhusu matatizo ya afya ya wanawake. Kwa mfano, unaweza kuandaa kampeni kuelezea umuhimu wa huduma bora kwa wanawake wajawazito kabla ya kujifungua. Ikiwa wanawake na familia zao wataelewa mahitaji ya afya ya wanawake, wanawake watakuwa na uwezekano zaidi wa kutumia huduma za afya zilizopo. Pia watakuwa na uwezekano wa kudai kupatiwa huduma zingine mpya – kama vile matibabu na uchunguzi bora zaidi wa saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti.
wanawake 3 wakibandika bango ambalo linawaalika wanawake wajawazito kwenda kupata huduma
  • Angalia namna ya kuweza kuboresha huduma ambazo tayari zipo. Kwa mfano, kama tayari kuna mkunga kwenye jamii, atapaje mafunzo ili kuongeza utaalam wake?
  • Tafuta njia mpya za kuongeza upatikanaji wa huduma za afya. Ni muhimu kufikiria aina za huduma za afya mnazohitaji na siyo tu zile zilizopo tayari. Hivyo, kama hakuna mfayakazi wa afya kwa sasa, mtawezaje kupata mtu mmoja, kumpatia mafunzo na kumwezesha kutoa huduma? Ikiwa tayari kuna kliniki, je, inaweza kutoa huduma zingine kama vile warsha na ushauri?
  • Wezesha kila mwanamke kuwashirikisha wenzake maarifa na uzoefu alionao juu ya huduma ya afya. Wanawake tayari wanafanya kazi kubwa ya utoaji huduma kwenye jamii. Kwa mfano, kawaida wanawake ndiyo huwahudumia wagonjwa, huwafundisha watoto kuwa na afya nzuri, huandaa au kutayarisha chakula, hufanya mazingira ya nyumbani na jamii yawe safi na salama, na huwasaidia wanawake wengine kujifungua. Kupitia kazi hii, wamejifunza maarifa na mbinu nyingi ambazo wanaweza kuzitumia kuwahudumia wanawake wengine na kila mwanajamii.Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Feb 2018