Hesperian Health Guides
Iwapo unahitaji kwenda hospitali
HealthWiki > Pale ambapo Wanawake hawana Daktari > Sura ya 3: Mfumo wa utoaji huduma za afya > Iwapo unahitaji kwenda hospitali
- Mtafute mtu wa kukusindikiza ambaye atakusaidia kupata huduma unayohitaji na pia kukusaidia kufanya maamuzi.

- Watu tofauti wanaweza kukuchunguza. Kila mmoja anapaswa kuandika matokeo au taarifa zake kwenye kadi ambayo unapaswa kubaki nayo. Kwa njia hii anayefuatia kukuhudumia ataweza kujua ni kipi kimekwisha fanyika juu yako.
- Kabla mtu yeyote hajaanza kukuchunguza au kukutibu, ni muhimu sana kuliza ni nini wanachokwenda kufanya na kwa sababu gani. Kwa njia hii unaweza kuamua kama unataka waendelee na kusaidia kuzuia makosa yasitokee.
- Jaribu kujenga urafiki na wafanyakazi wa hospitali. Wanaweza kukusaidia kupata huduma nzuri.
- Kama unapaswa kupata aina fulani ya upasuaji, uliza iwapo inawezekana sindano ya ganzi kuchomwa eneo lile husika tu ili kuzuia maumivu. Ni salama zaidi na utapata unafuu haraka kuliko kupewa dawa itakayokulaza kwa kipindi chote cha operesheni.
- Uliza kujua dawa gani unapewa na kwa nini.
- Wakati wa kuondoka omba upewe nakala ya ripoti yako ya matibabu.
Baada ya kufanyiwa operesheni.
![]() |
Kuweka mapafu yako salama na kuepusha nimonia, tembea tembea kama unaweza. Ukiwa kitandani, vuta pumzi nzito na jaribu kukaa mara nyingi. |
Kabla ya kuondoka hospitalini, uliza:
- Nifanye nini ili kulinda usafi wa kidonda?
- Nifanye nini juu ya maumivu?
- Je, ninapaswa kupumzika kwa muda gani?
- Je, ni lini tena ninaweza kushiriki tendo la ngono? Iwapo unajisikia aibu kuzungumzia jambo hili pengine daktari au mfanyakazi wa afya anaweza kuongea na mwenzi wako.
- Je, ninapaswa kumuona daktari tena, Kama ndiyo, lini?
Kula vyakula laini vyepesi ambavyo vinaweza kuchakatwa tumboni kwa urahisi.
Pumzika kadri uwezavyo. Ikiwa upo nyumbani, waombe wanafamilia wenzio wakusaidie kufanya kazi zako za kawaida za kila siku. Siku chache utakazotumia kujihudumia na kujitunza zitakusaidia kupata nafuu mapema.
Chukua tahadhari juu ya dalili za maambukizo. Usaha au majimaji ya kinjano, harufu mbaya, homa, ngozi na sehemu karibu na uliokatwa ‘kuwaka moto’ au maumivu zaidi. Mwone mfanyakazi wa afya iwapo utaona dalili mojawapo.
Iwapo operesheni yako ilikuwa maeneo ya tumbo, jaribu kuepuka kukaza au kuvuta eneo lililokatwa. Shikilia eneo hilo kwa uangalifu kwa kitambaa kilichokunjwa vizuri, blanketi au mto kila unapotembea au kukohoa.