Hesperian Health Guides

Tathmini ya athari kwa mazingira (TAMA)

Katika sura hii:

Kwa sababu viwanda na miradi ya maendeleo vimesababisha kiasi kikubwa cha uharibifu wa mazingira, serikali nyingi, viwanda na wakala wa maendeleo hivi sasa wanatakiwa kisheria kutumia nyenzo muhimu ya kupanga na kufanya maamuzi kuhusu maswala ya mazingira. Nyenzo hii hujulikana kama Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAMA).

TAMA huonyesha jinsi gani mradi kama vile ujenzi wa barabara, migodi, viwanja vya ndege, au viwanda vitakavyoathiri watu, wanyama, ardhi, maji na ubora wa hewa katika eneo husika. TAMA pia inaweza kuchunguza matatizo ya kijamii ambayo yanaweza kusababishwa na mradi huo kama vile watu kuhamishwa, na upotevu wa raslimali za kiutamaduni kwa mfano ajira za jadi, maeneo ya kihistoria, au yenye umuhimu wa kiroho. TAMA pia ni lazima ipendekeze njia mbadala zenye madhara na athari kidogo iwapo itabidi mradi huo kuendelea.

TAMA inaweza kufanywa na shirika au kampuni husika yenyewe, au pamoja na jamii na maafisa wa serikali.

Jinsi Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAMA) zinavyofanya kazi

TAMA huhusisha shughuli 2 za msingi:

  1. Uchunguzi wa athari za mradi na maandalizi ya taarifa katika maandishi inayoelezea athari hizi. Kawaida huu ni wajibu wa kampuni au shirika linalosimamia mradi na inaweza kuishirikisha au kutoishirikisha jamii.
  2. Mikutano ya hadhara ili kuruhusu jamii zitakazoathiriwa na mradi huo kuutathmini kabla haujaanza.

TAMA hufanya kazi vizuri zaidi pale inapoongozwa na misingi ya tahadhari. Pale TAMA inapoonyesha kuwa madhara yanaweza kutokea kutokana na mradi, inabidi mpango huo wa kuanzisha mradi usitishwe au kubadilishwa. Lakini mara nyingi tathmini hizo hutumika kuhalalisha mradi kwa kuufanya uonekane kutokuwa na madhara, hata kama unaweza kusababisha madhara makubwa kwa watu na mazingira; sasa au hata baadaye.

At a long table, a group of people in suits face a group of people in work clothes.

Makampuni mengi huandika ripoti ya TAMA hata kabla ya kualika jamii kushiriki katika tathmini hiyo, badala ya kuiandika kwa kushirikisha jamii. Mara kwa mara makampuni hayatangazi mikutano kuhusu zoezi la TAMA au hufanya mikutano kuwa migumu kwa watu kuweza kuhudhuria. Mchakato wa TAMA, usio shirikishi na wala wenye uwazi, ukiharakishwa na kampuni au wakala wa serikali mara nyingi husababisha mradi kuanza lakini wakati huo huo jamii ikiendesha kampeni ya kuusimamisha. Hata hivyo, pamoja na mapungufu hayo, TAMA ni nyenzo muhimu kwa jamii na serikali ili kuweza kutathmini na kuboresha miradi ya maendeleo iliyopendekezwa.

Jinsi jamii zinavyoweza kuishawishi Tathmini ya Athari kwa Mazingira - TAMA

4 people point of information on 2 papers to a man.

Kupata taarifa nyingi kutoka vyanzo tofauti (siyo tu kutoka kampuni husika), na kupata muda wa kutosha kuelewa athari zote ambazo zinaweza kutokea, ni sehemu muhimu ya kutumia haki yako kushiriki katika TAMA. Kawaida maamuzi mengi hufanyika kabla wale watakaoathirika zaidi na mradi kutoa mawazo yao.

Kushiriki katika zoezi la TAMA husaidia kuielimisha na kuiandaa jamii yako kulinda afya na rasilimali zake vizuri zaidi, na kwa muda mrefu. Ingawa haiwezekani kila mara kusimamisha mradi wenye madhara makubwa kuendelea, elimu na maandalizi ya jamii inayotokana na zoezi la TAMA husaidia kuimarisha msingi wa ulinzi wa jamii.

Jamii idai kushirikishwa

Jamii zinaweza kudai kushirikishwa katika TAMA. Wakati mwingine mahakama, serikali, au wakala wa maendeleo wanaweza kuruhusu wawakilishi wa jamii kushiriki katika zoezi la TAMA. Wanajamii wanaweza kushiriki, au kuomba mdau kama vile shirika lisilo la kiserikali au wakili kuwawakilisha. Iwapo wawakilishi wa jamii watashiriki katika zoezi la TAMA, wanapaswa kutoa mrejesho kwa jamii kupitia mikutano ya jamii, hasa kuhusu kampuni ilichopanga na inachofanya. Ushiriki wa jamii unaweza kusaidia kujenga uelewa juu ya haki za jamii na wajibu wao, na njia ambazo wanaweza kutumia kuzuia madhara kutokana na mradi, au kuzuia kabisa mradi usiendelee.

Jamii idai kupata nakala ya ripoti kamili ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira- TAMA

Jamii zina haki ya kuiona ripoti kamili ya tathmini hiyo na siyo tu muhtasari au sehemu yake. Ripoti za TAMA mara nyingi zinajumuisha “Hadhari za kiusalama”, “Hadhari za kijamii”, “Hadhari za kiafya” na “Gharama za usafishaji”. Sehemu hizi zinaweza kuelezea matatizo ambayo kampuni pengine isingependa yajulikane hasa katika mikutano ya hadhara.

Matatizo yanayoelezewa katika TAMA, pamoja na matatizo yanayoachwa na tathmini hiyo, yanaweza kufikishwa kwenye vyombo vya habari, maafisa wa serikali na wananchi kujadiliwa ili kujenga upinzani mpana dhidi ya miradi yenye madhara. Yanaweza pia kufikishwa kwenye vyombo vya kitaifa na kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa, na kusababisha shinikizo kwa makampuni au serikali kutekeleza matakwa ya jamii.

Tathmini ya athari kwa mazingira (TAMA) yenye misingi ya kijamii

TAMA yenye misingi ya kijamii inaweza kusaidia watu katika kijiji, mji au mkoa kufikia mwafaka kuhusu njia wanazotumia katika maisha yao ya kawaida, ulinzi, na matumizi ya rasilimali kama vile hewa, chakula, maji, wanyama, mazao ya misitu, mitishamba, maeneo yenye umuhimu wa kiroho nk. Hii inaweza kuanzisha mchakato wa usuluhishi wa migogoro na kutokuelewana ndani ya jamii kuhusu matumizi ya rasilimali. Hali hii huchangia kujenga umoja unaotakiwa dhidi ya mashirika au serikali. Inaweza pia kuchangia kuhamasisha jamii kupinga viwanda vinavyotumia mgawanyiko miongoni mwa watu kupora maji yao, mbao, ardhi au rasilimali nyingine.

TAMA yenye misingi ya kijamii kwa urahisi inaweza kuwa zoezi tu la kujadili rasilimali ambazo jamii inatumia na kukubaliana kuhusu njia bora za kulinda rasilimali hizo dhidi ya wanyonyaji. Lakini TAMA yenye misingi ya kijamii madhubuti inaweza kuhusisha uandaaji wa ramani ambazo zinaonyesha mambo mengi, kufanya tafiti, na kujenga mahusiano na jamii jirani na taasisi nyingine zinazotoa misaada.

TAMA ya misingi ya kijamii ni tofauti na TAMA inayoendeshwa na mashirika au serikali. Huenda isikidhi mahitaji ya TAMA rasmi au ya kisheria kwa sababu hutoa umuhimu zaidi juu ya mawazo ya jamii, afya ya watu na tamaduni zao kuliko uchimbaji au uendelezaji wa rasilimali hizo. TAMA ya kijamii hutambua kuwa muundo ambao ni mgumu kueleweka na lugha ya ‘kisayansi’ inayohitajika katika TAMA, siyo tu huwachanganya watu wa kawaida, lakini hufanywa hivyo kwa makusudi kabisa ya kuwatenga. TAMA ya kijamii ni njia ya kusema: “INAWEZEKANA KUTATHMINI ATHARI KWA MAZINGIRA KWA KUTUMIA NJIA NYINGINE”.

Soma Uchoraji ramani ya jamii, Tamthilia, Matembezi ya kiutafiti katika jamii kujua hali ya taka.

Jamii yapinga mradi wa uchimbaji madini

Jamii ndogo ya wakulima ya Junin ina makazi yake katika eneo zuri la misitu katika mteremko wa milima ya Andes nchini Ekueda, Amerika ya Kusini. Watu katika jamii hii ni masikini lakini wameishi kutokana na kilimo kwa mamia ya miaka. Hivi karibuni, watu wa Junin walikabiliwa na changamoto kubwa zaidi katika historia yao. Kampuni moja ilipanga kuanzisha katika eneo hilo mgodi mkubwa wa shaba ambao ungekuwa miongoni mwa migodi mikubwa zaidi, Amerika ya Kusini.


Kampuni ya Kijapan ilipokuja kuchunguza eneo hilo, watu wa Junin walijua uchimbaji madini ungeleta uchafuzi mkubwa. Lakini kampuni ya uchimbaji iliahidi kujenga barabara, vituo vya afya na shule. Hivyo watu wa Junin ilibidi waruhusu uchunguzi wa madini ufanyike. Baada ya muda mfupi, kampuni iligundua kuwepo kwa kiasi kikubwa cha shaba, na watu wa Junin wakagundua mfumo wao wa usambazaji maji ukianza kuchafuliwa na taka kutokana na uchimbaji. Watu walianza kuugua magonjwa ya ngozi na matatizo mengine ya afya.

A woman speaks.
Tuliendelea na harakati. Baadhi ya wanakijiji walianzisha kijarida kueneza habari na kujenga mshikamano juu ya mapambano yetu.


Jamii iliiomba kampuni ya uchimbaji kuacha uchafuzi. Kampuni haikuacha, hivyo jamii ya Junin ikachukua hatua. Wachimbaji walipokuwa hawapo wakati wa likizo, mamia ya wanakijiji waliingia kwenye kambi ya machimbo na kuondoa vifaa, fenicha, na vitu vyenye thamani vingi, na kuviacha kwa viongozi wa serikali. Halafu waliteketeza kwa moto kambi nzima ya wachimbaji. Kampuni ilipata ujumbe na kuondoka eneo hilo, lakini baadaye waliuza mgodi huo kwa kampuni kutoka Kanada.


Kampuni kutoka Kanada ilianza kazi kwa kutaka kuigawa jamii. Kampuni ilitoa kiasi kikubwa cha fedha kwa wakazi wa Junin ili wauze ardhi yao. Baadhi ya watu waliweza kuuza, lakini wengine walikataa. Kampuni ilijua hali hii ingesababisha mgogoro. Kampuni pia ilituma daktari kutoa huduma za afya, lakini kwa watu waliosaini karatasi kukubali kuwepo kwa machimbo eneo hilo. Baada ya ukiukwaji huu wa haki kujulikana nje ya nchi ya Ekueda, wadau wa kimataifa walituma daktari kuwahudumia watu wote waliohitaji kutibiwa.

Kwa vile sheria nchini Ekueda huhitaji TAMA kabla ya mradi wa maendeleo kuanza, watu wa Junin walitumia TAMA kama silaha mojawapo ya kulinda ardhi yao. Wanakijiji walijua kwamba iwapo TAMA haitafanyika vizuri, serikali isingeruhusu mgodi kujengwa. Walijua pia TAMA ya ukweli ingeonyesha kuwa mgodi ungelazimisha watu kuhamishwa, uchafuzi wa hali ya hewa, mmomonyoko wa ardhi, njia za maji kujaa tope, na maji kuchafuliwa na vinyesi, madini ya chuma yanayodhuru afya, na kemikali zingine zenye sumu.


Watu wa Junin walikuwa wamejifunza kutumia sheria kulinda maslahi yao. Baada ya Kampuni kudai kuwa ilikwisha fanya TAMA, serikali ilikataa kwa kutokuwa kamilifu.


Watu wa Junin pia walitumia hatua za moja kwa moja au za wazi, kama vile kutoruhusu kampuni kuingia eneo hilo kwa kuziba njia zote. Viongozi wa jamii walitamka eneo zima kuwa marufuku kwa ajili ya shughuli za uchimbaji. Kwa kutumia njia mbalimbali, watu wa Junin walizuia chimbo la wazi la shaba kuharibu makazi yao, misitu yao mikubwa na vyanzo vya maji.


Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022