Hesperian Health Guides

Kufungua kesi mahakamani

Katika sura hii:

Njia mojawapo inayoweza kufanikisha haki na sheria za mazingira ni kufungua kesi mahakamani dhidi ya makampuni ambayo yanakiuka sheria za kitaifa na kimataifa. Kesi itakayofanikiwa dhidi ya kiwanda kinachochafua mazingira au kampuni siyo tu itasaidia kulinda watu wanaoathirika moja kwa moja kutokana na uchafuzi huo, bali itawalinda watu katika maeneo mengine na hata kizazi kijacho.

A man with a briefcase and a woman speak.
Lazima tutumie sheria kulinda haki zetu.
Lakini ili sheria iweze kufanya kazi,lazima tupiganie haki zetu!

Je, kufungua kesi mahakamani kutasaidia jamii yako?

Kupeleka kesi mahakamani ni njia ambayo imetumika sana kwa mafanikio katika mapambano mengi kwa ajili ya haki za kimazingira. Lakini kuendesha kesi mahakamani ni ghali sana na mara nyingi huchukua miaka mingi.

Hata pale ambapo nchi ina sheria zinazolinda afya na mazingira, inaweza kuwa vigumu kushinda kesi mahakamani. Kama sheria hazitumiki mara kwa mara, majaji na wanasheria wanaweza kutokuzijua. Na katika nchi nyingi, hasa pale ambapo mashirika yana nguvu sana, rushwa miongoni mwa majaji na wanasiasa huifanya kazi ya jamii maskini kudai haki zao kuwa ngumu. Kwa bahati mbaya, idadi ya kesi ambazo hazifanikiwi ni nyingi kuliko zile zinazofanikiwa.

Kabla ya kufungua kesi dhidi ya shirika, kiwanda au serikali, kuna mambo ya kuzingatia.

Fikiria malengo yako

Ni muhimu kujua hasa nini unachotaka kesi hiyo kufanikisha. Halafu amua kama kufungua kesi mahakamani ndiyo njia bora zaidi ya kulifikia lengo hilo. Je, unataka kampuni:

  • Kusafisha mafuta waliyomwaga hovyo au kuvujisha, au uchafuzi mwingine wenye sumu?
  • Iwalipe watu fidia kwa ajili ya madhara waliopata ya kiafya, kuhusiana na ardhi au raslimali zingine?
  • Kusitisha kazi zao na kuondoka katika eneo au nchi hiyo?


Mapambano ya kisheria yanaweza kuhamasisha na kuielimisha jamii. Lakini vitendo kama vile migomo ya aina mbalimbali, na kampeni za kueneza habari zinaweza kusababisha kuwepo majadiliano au mwafaka wa kisiasa haraka, na kwa urahisi zaidi, kuliko mapambano ya kisheria ambayo huchukua muda mrefu. Fikiria iwapo vitendo vya aina hii vinaweza kuwa rahisi na kuifaa jamii yako kuliko kufungua kesi mahakamani. Fikiria pia iwapo njia zote mbili: njia ya kisheria na ile ya vitendo vya moja kwa moja zitasaidia jamii yako kupata ushindi.

Je hatua ya kufungua kesi mahakamani itakuwa na manufaa yoyote hata kama haitafanikiwa?

Bila shaka ungependa kushinda kesi yako mahakamani; lakini kama huna uhakika wa kushinda, fikiria faida na hasara kama hutashinda. Wakati mwingine kesi mahakamani, hata ikishindwa, husaidia kuongeza uelewa na hamasa ya watu juu ya matatizo ya jamii. Iwapo kesi juu ya uharibifu wa mazingira na haki za binadamu itashindwa katika mahakama za nchi yako, unaweza kukata rufaa kwenye vyombo vya kimataifa vya haki za binadamu. Hii pia inaweza kutotatua tatizo, lakini itatangaza zaidi swala lako. Hata hivyo, inaweza kuchukua muda na raslimali.

Wakati mwingine kesi isipofanikiwa hufanya hali kuwa mbaya zaidi. Matokeo mabaya yanaweza kufanya majaji na wanasheria kufikiri kwamba hata kesi zijazo kama hizo hazipaswi kushinda. Upotoshaji wa habari kutokana na kesi hiyo unaweza kuwafanya watu kufikiri kwamba jamii inadai fedha au fidia isiyostahili. Kama vile juhudi yoyote ya jamii kujipanga kuanzisha kitu fulani inaposhindikana, vivyo hivyo kesi isipofanikiwa huweza kuwavunja watu moyo na kuigawa jamii.

Nani atafungua kesi mahakamani?

Waathirika kutokana na madhara ya uharibifu wa mazingira, awe mtu mmoja, familia yake au jamii nzima lazima iwe tayari kubeba jukumu hilo pamoja na gharama za aina yote zinazoambatana. Kawaida shirika lisilo la kiserikali haliwezi kufungua kesi dhidi ya kampuni kwa niaba ya mtu aliyeathiriwa lakini ambaye hayuko tayari kuwa sehemu ya kesi hiyo.

Je kuna ushahidi wa madhara?

Ili kesi iweze kufanikiwa mahakamani, ni lazima uwe tayari kuthibitisha:

  • Waathirika walipata madhara ya kimwili, au kiuchumi.
  • Shirika au kampuni ndiyo ilisababisha au inahusika na madhara hayo.


Kama hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha haya, kesi inaweza kuleta hasara zaidi kuliko faida. Hata kama ni wazi kampuni imevunja sheria, bila kuwa na ushahidi kwamba wamesababisha madhara, mnaweza msiruhusiwe kufungua kesi mahakamani, na kama itafunguliwa basi huenda mkashindwa.

Je upo ushahidi wa kuthibitisha hayo?

Ushahidi wa maana ni ule ambao unaweza kuletwa mbele ya mahakama. Watu wanaofungua kesi mahakamani kwa sababu wamedhurika ni lazima wawe tayari kuongea mahakamani, na lazima wawe na mashahidi ambao watakuwa tayari pia kuzungumza. Lazima wawe tayari kuonyesha kupitia picha, tafiti, kumbukumbu za hospitali au ushahidi mwingine kwamba shirika wanalolishtaki liliwadhuru. Madhara yanaweza kuwa jambo gumu kuthibitisha. Kwa mfano, kampuni inaweza kuajiri daktari kusema kwamba kemikali kampuni ilizotumia hazikuwasababishia wafanyakazi saratani, lakini ni tabia mbaya za wafanyakazi zikiwemo uvutaji wa sigara, kula vyakula visivyofaa au ni bahati mbaya tu. Inaweza kuwa vigumu kuthibitisha “chanzo na madhara” hata kama hali ikiwa inaonyesha wazi.

Nani au nini kilisababisha madhara?

Kesi zinaweza kufunguliwa mahakamani dhidi ya watu, kampuni, mashirika na katika nchi nyingi dhidi ya serikali kwa kusababisha uharibifu wa mazingira.

Je kesi inaweza kufunguliwa dhidi ya shirika au kampuni ya kimataifa?

Mashirika au kampuni za kimataifa mara nyingi huwa na ofisi katika nchi nyingi. Ili kuweza kufungua kesi dhidi ya shirika au kampuni ya kimataifa ni muhimu kufanyakazi katika nchi mahali madhara yalipotokea na vilevile, katika nchi- mama ya shirika au kampuni hiyo. Hii inaweza kuwa aghali na ngumu lakini inawezekana. Makampuni ya kimataifa mara nyingi yana matawi katika nchi yanapofanyakazi. Inaweza kuwa rahisi kuishtaki kampuni tanzu kuliko kumshtaki mmiliki wa kigeni. Kwa mfano, wakati kampuni ya uchimbaji mafuta ya Marekani ilipochafua eneo la Delta la mto Niger huko Nigeria, kuliko kuishtaki kampuni ya Kimarekani, wanaharakati wa Nigeria waliishtaki kampuni tanzu iliyopo Nigeria. Wakati huohuo, wanaharakati wa kimataifa walianzisha kampeni ya kuelimisha watu dunia nzima kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na kuishinikiza kampuni hiyo chafuzi kubadili utendaji wake.

Mambo mengine ya kuzingatia

(Je madhara au uharibifu umefanywa hivi karibuni? Kesi lazima ifunguliwe ndani ya kipindi cha miaka fulani baada ya madhara kufanyika (kawaida siyo zaidi ya miaka 10.) Hivyo ni vigumu kushinda kesi kuhusiana na maradhi ambayo huchukua muda mrefu kujitokeza, kama vile saratani.

  • Je watu wanaofungua kesi, mashahidi wao na wanasheria wao wako tayari kwa lolote kuhusu usalama wao? Mashirika mengi na serikali wako tayari kutumia njia yoyote ile kulinda madaraka yao, kama vile matumizi ya nguvu na hata kuua. Hivyo wale wanaopinga mamlaka hayo wanaweza kuweka maisha yao hatarini.
3 protesters link arms; 1 holds a sign reading "Environmental rights are human rights."
  • Je kuna fedha kwa ajili ya kulipia gharama za uendeshaji wa kesi hiyo mahakamani? Gharama ambazo huongezeka haraka ni pamoja na ada za mahakama, wanasheria, gharama za safari za ndani na nje, simu, ushahidi na gharama nyingine.
  • Je mko tayari kuendesha kesi hiyo kwa miaka mingi? Kesi inaweza kuchukua miaka 3-10 na zaidi. Mara nyingine waathirika wanakuwa tayari wamefariki kesi inapofikia kuamuliwa.


Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022