Hesperian Health Guides

Mzunguko wa hedhi wa kila mwezi

Katika sura hii:

Takribani mara moja kila mwezi wakati wa umri wa kuzaa, mwanamke huwa na siku chache ambapo majimaji yenye damu hutoka kwenye tumbo lake la uzazi yakitoka nje ya mwili wake kupitia ukeni. Tendo hili hujulikana kama hedhi, au hedhi ya kila mwezi, au mwanamke kuwa katika siku zake. Wanawake sehemu tofauti duniani huwa na majina tofauti ya jambo hili. Ni mchakato chanya wa kiafya kwani ni sehemu ya maandalizi ya mwili katika kujiweka tayari kwa ajili ya ujauzito.

Wanawake kutoka tamaduni tofauti wakielezea hedhi
Sehemu nyingi duniani, wanawake wana majina tofauti kwa ajili ya tukio la hedhi ya kila mwenzi.
Nimeuona
mwezi.
Tabia yangu ya
kila mwezi
imewadia.
Nimepata
mgeni kutoka
Urusi.
Niko kwenye
hedhi.
Niko kwenye
siku zangu.
Maria
analia.
Rafiki
ameni-
tembelea.

Wanawake wengi huchukulia jambo hili la hedhi kama sehemu ya kawaida ya maisha yao. Lakini mara nyingi hawajui kwa nini hutokea au wakati mwingine kwa nini hubadilika.

MZUNGUKO WA HEDHI WA KILA MWEZI

Mzunguko wa hedhi hutofautiana kati ya mwanamke mmoja na mwingine. Huanza na siku ya kwanza ya mwanamke ya kutokwa damu. Wanawake wengi hutokwa damu kila baada ya siku 28. Lakini baadhi hutokwa damu kila baada ya siku 20 au kwa uchache kila baada ya siku 45 kwa wengine.

Kiasi cha homoni za estrojeni na projesteroni kinachozalishwa na ovari hubadilika kila mwezi. Katika nusu ya kwanza ya mzunguko, ovari hutengeneza zaidi homoni ya estrojeni ambayo husababisha utando mzito wa damu kuota kwenye kuta za tumbo la uzazi au kizazi. Mwili hutengeneza utando huu ili mtoto apate sehemu laini ya kukulia kama kiota iwapo mwanamke atabeba ujauzito mwezi huo.

Mwanamke anaweza kugundua kuwa muda kati ya hedhi moja ya kila mwezi na nyingine hubadilika kadri umri wake unavyoongezeka, baada ya kujifungua, au kwa sababu ya msongo.

Takriban siku 14 kabla ya mzunguko wa hedhi kumalizika, wakati utando laini uliotengenezwa ni tayari, yai hutolewa kutoka kwenye ovari. Kitendo hiki huitwa ovulesheni (Ovulation). Kisha yai hili husafiri likishuka kwenda kwenye mji wa mimba. Kwa wakati huu mwanamke anakuwa na rutuba na anaweza kutunga mimba. Kama mwanamke huyu atakuwa amefanya ngono siku za karibuni, mbegu ya mwanaume inaweza kuungana na yai hili. Tendo hili, yaani kuungana kwa mbegu na yai huitwa urutubishaji na ndio mwanzo wa ujauzito.

Katika siku 14 za mwisho za mzunguko wa hedhi- hadi anapoona damu ya hedhi ya mwezi unaofuata- mwanamke pia huzalisha homoni ya projesteroni. Homoni hii ya projesteroni husababisha utando unaofunika kizazi kwa ndani kuanza kujiandaa kwa ajili ya ujauzito.

Kwa miezi mingi, yai huwa halirutubishwi, kwa hivyo lile tabaka la utando ndani ya mji wa mimba halihitajiki. Ovari husitisha kuzalisha homoni za estrojeni na projesteroni, na lile tabaka huanza kuvunjika na kudondoka. Wakati utando huu unapotoka nje pamoja na hedhi, yai pia hutoka nje. Na huu ndio mwanzo wa mzunguko mpya wa hedhi. Baada ya hedhi ya mwezi, ovari huanza tena kutengeneza estrojeni na hivyo tabaka lingine la utando huanza kuota tena.

Mzunguko wa kila mwezi
michoro 4 inayoonesha mabadiliko katika sehemu za uzazi za mwanamke wakati wa mzunguko wa hedhi ya kila mwezi
Wakati wa hedhi ya kila mwezi, utando hukatika
damu
Mara baada ya kumaliza hedhi ya kila mwezi
mirija ya mayai ya kike ya uzazi
ovari
utando unaozunguka kuta za tumbo la uzazi
tumbo la uzazi au kizazi
uke
Ovari inapoachia yai...
...utando huzidi kuwa mzito
egg
siku 5 baada ya yai kuachiwa,
utando huzidi kuwa mzito zaidi
Kwa wanawake wengi, mzunguko wa hedhi mzima huchukua takriban siku 28-sawa na mzunguko wa mwezi wa kawaida

MATATIZO YANAYOHUSIANA NA HEDHI YA KILA MWEZI

Iwapo unapata matatizo kuhusiana na hedhi, jaribu kuongea na mama yako, dada zako au marafiki zako. Unaweza kugundua kwamba hata wao wanayo matatizo yanayofanana na wanaweza kukusaidia.

Mabadiliko ya hedhi

Wakati mwingine ovari hazitoi yai. Hili likitokea, mwili hutengeneza homoni ya projesteroni kidogo, ambayo inaweza kusababisha mabadiliko ya lini hedhi itatokea na kiasi cha damu. Wasichana ambao ndiyo wameanza kupata hedhi, au wanawake ambao wameacha kunyonyesha siku za karibuni – wanaweza kupata hedhi kwa miezi michache au kupata damu ya hedhi kidogo au kupata damu nyingi kupita kiasi. Mizunguko yao hutulia taratibu na hatimaye kurudia hali ya kawaida baada ya muda.

Wanawake wanaotumia njia za uzazi wa mpango za homoni wakati mwingine hujikuta wanapata hedhi katikati ya mwezi.

Wanawake wenye umri mkubwa ambao bado hawajafikia hatua ya hedhi kukomaa wakati mwingine hutokwa na damu nyingi zaidi, na wakati mwingine mara nyingi zaidi kuliko walivyokuwa wakati wa ujana. Wanavyokaribia umri wa hedhi kukomaa, wanaweza kutopata hedhi kwa miezi kadhaa, na baadaye kurudia kupata hedhi tena kama kawaida.

Maumivu wakati wa hedhi ya kila mwezi

Wakati wa hedhi, tumbo hujikamua kusukuma utando ili uweze kutoka nje. Kujikamua kwa tumbo kunaweza kusababisha maumivu eneo la chini ya tumbo au mgongo. Maumivu yanaweza kuanza kabla ya hedhi au punde mara baada ya hedhi kuanza.

Jambo la kufanya:
dole gumba likibonyeza sehemu laini kwenye kiganja
Kubonyeza kwa nguvu sehemu laini kati ya dole gumba lako na kidole cha pili kunaweza kusaidia kutuliza aina nyingi za maumivu
  • Pangusa sehemu ya chini ya tumbo. Hii itasaidia kulegeza misuli.
  • Jaza chupa ya plastiki au chombo kingine maji ya moto na kukiweka juu ya sehemu ya chini ya tumbo lako au sehemu ya chini ya mgongo. Au tumia kitambaa kizito ambacho kimelowekwa kwenye maji ya moto.
  • Kunywa chai ya tangawizi. Wanawake wa eneo lako wanaweza kufahamu aina zingine za chai na njia zingine za kutuliza maumivu kama haya.
  • Endelea kufanya kazi zako za kila siku.
  • Jaribu kufanya mazoezi na kutembea.
  • Unaweza kutumia dawa baridi za kutuliza maumivu kama Ibuprofen.
  • Iwapo pia unatokwa na damu nyingi na hakuna njia inayosaidia, kutumia dozi ndogo ya vidonge vya uzazi wa mpango kwa muda wa miezi 6 hadi 12 kunaweza kusaidia.

Dalili za awali za hedhi

mwanamke akionekana kutojisikia vizuri, akiwa ameshikilia paji la uso na tumboni

Baadhi ya wanawake na wasichana hujisikia vibaya siku chache kabla ya kuingia kwenye mzunguko wao wa hedhi ya kila mwezi. Huweza kupata kundi moja au zaidi ya dalili zifuatazo, ambazo hujulikana kama dalili za awali:

  • Maumivu ya matiti.
  • Kujisikia tumbo la chini kujaa.
  • Shida katika kupata choo.
  • Kusikia uchovu usiyo wa kawaida.
  • Maumivu ya misuli kwenye tumbo la chini au mgongoni.
  • Mabadiliko katika unyevu ukeni.
  • Uso kutoa mafuta mafuta na chunusi.
  • Hisia zenye nguvu au ambazo ni ngumu kuzidhibiti.

Wanawake wengi hupata angalau dalili mojawapo kila mwezi na baadhi ya wanawake hupatwa na dalili zote. Mwanamke anaweza kupata dalili tofauti kutoka mwezi mmoja kwenda mwingine. Kwa wanawake wengi, siku zinazotangulia hedhi huwa ni siku zisizo na utulivu. Lakini wanawake wengine husema kwamba hujisikia vizuri zaidi kwa maana ya ubunifu na utendaji wao kwa ujumla.

Jambo la kufanya:

Kinachomsaidia mwanamke kukabiliana na dalilia za awali za hedhi hutofautiana kati ya mwanamke mmoja na mwingine. Ili kuweza kujua ni njia ipi itakusaidia, mwanamke anapaswa kujaribu njia tofauti kuona ni ipi inampa unafuu zaidi.

Wanawake 4 wakicheza mpira wa kapu
Mazoezi wakati mwingine husaidia kupunguza dalili mbaya za awali za hedhi.

Yafuatayo ni mawazo mengine ambayo yanaweza kukusaidia:

  • Punguza matumizi ya chumvi. Chumvi hufanya mwili ulimbikize maji mengi ndani, hali inayokufanya kuhisi tumbo lako sehemu ya chini kujaa.
  • Epuka vinywaji vyenye kemikali ya kafeini vikiwemo kahawa, chai, na soda za aina ya kola.
  • Jaribu kula nafaka ambazo hazijachakatwa, karanga, samaki wabichi, nyama, maziwa au vyakula vingine vyenye protini. Mwili wako utakapotumia vyakula hivi, utaondoa maji ya ziada tumboni na kupunguza hali ya kujaa.
  • Jaribu pia kutumia dawa za mitishamba. Ulizia kwa wanawake wenye umri mkubwa na uzoefu zaidi juu ya dawa za mitishamba zinazosaidia.


Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Feb 2018