Hesperian Health Guides

Mfumo wa uzazi wa mwanaume

Katika sura hii:

Viungo vya uzazi vya mwanaume ni rahisi kuonekana kuliko vya mwanamke kwa sababu kwa sehemu kubwa vipo nje ya mwili. Mapumbu, korodani au makende ndio hutengeneza homoni kubwa ya kiume kwenye mwili iitwayo testosteroni. Mvulana anapopita katika kipindi cha balehe, huanza kutengeneza homoni ya testosteroni kwa wingi. Homoni hii ndiyo huleta mabadiliko yanayomfanya mvulana azidi kuonekana kama mwanaume.

KUPATA MTOTO – JE ATAKUWA WA KIKE AU WA KIUME?

mwanaume akirusha shilingi hewani
Wa kike au wa kiume? Ni suala la bahati tu — sawa na kurusha shilingi.

Kiasi cha nusu ya mbegu zote za mwanaume zinaweza kutengeneza mtoto wa kiume na nusu nyingine iliyobaki yaweza kutengeneza mtoto wa kike. Ni mbegu moja tu itakayoungana na yai la mwanamke. Ikiwa ni mbegu ya kiume ilitakayoungana na yai la mama basi mtoto atakuwa wa kiume Ikiwa ni mbegu ya kike iliyoungana na yai, basi mtoto atakuwa wa kike.

Kwa sababu jamii nyingi huthamini zaidi mtoto wa kiume kuliko wa kike, baadhi ya familia hupendelea kuwa na watoto wa kiume kuliko wa kike. Jambo hili siyo haki kwa sababu watoto wa kike wanapaswa kuthaminiwa sawa na wa kiume. Pia siyo haki kwa sababu katika baadhi ya sehemu, mwanamke ndiye anayelaumiwa ikiwa hajazaa watoto wa kiume. Lakini ukweli ni kwamba ni mbegu ya mwanaume ambayo hutengeneza aidha mtoto wa kiume au wa kike.

Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Feb 2018