Hesperian Health Guides
Mabadiliko ambayo yanaweza kuleta maisha bora zaidi
HealthWiki > Pale ambapo Wanawake hawana Daktari > Sura ya 5: Masuala ya afya yahusuyo wasichana > Mabadiliko ambayo yanaweza kuleta maisha bora zaidi
Katika sehemu nyingi, jamii zinamjenga na kumwaminisha msichana kujiona kuwa ana thamani ndogo kuliko mvulana. Hufundishwa kuona aibu juu ya miili yao na hali ya kuwa mwanamke, na hujifunza kukubali elimu ndogo, chakula kidogo, kunyanyasika zaidi, na kufanya kazi zaidi kuliko kaka zake. Hali hii siyo tu huathiri afya zao moja kwa moja, bali pia huwafanya kujisikia vibaya kwa kuwa wanawake na kushindwa kufanya maamuzi sahihi juu ya afya zao kwa ajili ya maisha bora ya baadaye. Wasichana wanapolelewa hivi, huonesha kwamba jamii zao haziwajali kwa usawa kama zinavyowajali wavulana.
Lakini kama jamii ya msichana itamtambua na kumthamini kila mtu kwa usawa – awe ni mwanaume au mwanamke, itamfanya msichana akue akijiona kwamba anao uwezo wa kuboresha maisha yake na familia yake, pamoja na majirani zake.
Namna jamii inavyowatendea wanawake huathiri pia namna familia zinavyotendea watoto wao wa kike. Kwa mfano, iwapo jamii inaamini kwamba wasichana wanahitaji kujifunza stadi za kujikimu, familia inayoishi kwenye jamii hiyo itataka binti zake waende shule na kujiendeleza kadri iwezekanavyo. Lakini kwenye jamii ambapo wanawake huruhusiwa tu kufanya kazi ziitwazo za “kike”, na wanawake hawaruhusiwi kushiriki na kuongea katika mikutano ya hadhara, familia huenda zisione umuhimu wa kuwasomesha wasichana.
Zipo njia nyingi za kumsaidia msichana ajisikie vizuri na kusaidia familia yake na jamii ziweze kuelewa kwamba msichana anaweza. Kurasa zinazofuata zinaelezea jambo hili.
Njia ambazo wasichana wanaweza kufuata kuboresha maisha yao
Tafuta mtu wa kuongea naye ambaye unadhani ataweza kukusikiliza na kukuelewa – rafiki, dada, au ndugu mwingine wa kike. Zungumzia hofu na matatizo uliyo nayo. Kwa pamoja mnaweza kuzungumzia wanawake wengine jasiri na wenye mifano katika jamii yenu, malengo na ndoto zako za baadaye.
Fanya mambo ambayo wewe na rafiki zako mnafikiri ni muhimu. Ikiwa utaona tatizo katika jamii yako, kutana pamoja na rafiki zako na kufanya jambo lolote linalostahili kusaidia kuleta mabadiliko. Nyote mtajisikia furaha na kujivunia mtakapoona kwamba juhudi zenu zimechangia kuboresha jamii yenu.
Maamuzi kwa ajili ya maisha bora ya baadaye.
Kuna maamuzi muhimu unayoweza kufanya pamoja na familia yako ili kutengeneza fursa mpya za baadaye.
Elimu. Elimu inaweza kukusaidia kujivunia nafsi yako, kuishi maisha yenye furaha na afya zaidi. Kwa wasichana wengi, elimu hufungua mlango wa maisha bora ya baadaye. Hata kama huwezi kwenda shule, bado zipo njia zingine za kujifunza kusoma na kujiendeleza. Kwa mfano, unaweza kujifunza ukiwa nyumbani, kujiunga na programu ya kujifunza kusoma na kuandika, au kujifunza stadi mpya chini ya mtu mwenye ujuzi na uzoefu.
Kusubiri kuolewa. Ongea na familia yako kuhusu kuvuta subira kuolewa hadi pale utakapojisikia kuwa tayari na kumpata mwenzi sahihi. Wasichana wengi wameweza kumaliza shule na kuanza kufanya kazi kabla ya kuanzisha familia zao. Hii inaweza kukusaidia kupata fursa ya kujielewa zaidi na kile utachotaka. Kama utasubiri unaweza hata kumpata mwenzi mwenye fikra na mtazamo unaofanana na wako kuhusu maisha.
Kusubiri kupata watoto.
Ni rahisi kulea mtoto mwenye furaha na afya bora zaidi iwapo wewe pamoja na mwenzi wako mtasubiri hadi pale mtakapokuwa tayari kuanzisha familia. Kama unafikiria kupata mtoto, yafuatayo ni baadhi ya mambo muhimu ya kujiuliza:- Je, utaweza kuendelea na elimu yako?
- Utampatiaje mtoto wako mahitaji yake ya msingi ? – chakula, mavazi, malazi, n.k?
- Je, upo tayari kumpatia mwanao mahitaji yake ya kisaikolojia-upendo, ukaribu, kucheza nk, ili aweze kukua akiwa mwenye afya ?
- Je, mwenzi wako yuko tayari kusaidiana katika kumlea mtoto?
- Je, familia yako itakusaidiaje?