Hesperian Health Guides

Kuamua juu ya marafiki wa kiume na ngono

Katika sura hii:

wanaume vijana 2 wakiongea
msichana amesimama peke yake akifikiria juu ya mvulana
Nina wasiwasi, kweli ananipenda?

Vijana wengi huanza kupata hisia za mapenzi na kingono kadri wanavyoongezeka umri. Kufikiria kumshika mtu mwingine au wewe kushikwa kimahaba ni jambo la kawaida. Hata baadhi ya wasichana huweza kuwa na hisia hizo za kimahaba kwa wasichana wenzao. Lakini mara nyingi watu huwa na hisia za kimapenzi na kingono hata kabla ya kuwa tayari kuzifanyia kazi.

Fanya ngono tu pale utakapoamua uko tayari na unajua jinsi ya kujikinga dhidi ya madhara yake. Ngono inaweza kufurahiwa na wenzi wote 2, lakini pasipo hofu au aibu.

Vijana wa kike hufanya ngono kwa sababu mbalimbali. Baadhi hufanya ngono kwa sababu wanataka kupata mtoto. Wengine hufanya ngono kwa sababu huwafanya kujisikia vizuri au kwamba wanapendwa. Baadhi ya wanawake hufanya hivyo kwa kuamini kwamba ni wajibu wao kutimiza jambo hilo kama mke au mpenzi. Wengine hufanya ngono kama biashara kupata fedha au vitu vingine wanavyohitaji ili waweze kuishi kama vile chakula, mavazi au malazi.

Wengine hufanya ngono kwa kufikiri kwamba itamfanya mwenzi ampende zaidi. Wakati mwingine rafiki au mwenzi wa kiume anaweza kumfanya msichana ajihisi kwamba anapaswa kufanya ngono hata kama hajawa tayari kufanya hivyo.

Hakuna anayepaswa kufanya ngono kama hataki kufanya hivyo. Fanya ngono pale tu ambapo umeamua kwamba upo tayari kufanya hivyo. Ngono inaweza kufurahiwa na pande zote mbili, lakini ni vigumu kufurahia kitu kama unakuwa na hofu, aibu, au pale ambapo hujaridhia.

Kama upo tayari kwa ajili ya kufanya ngono, daima jikinge dhidi ya mimba zisizotakiwa na magonjwa. Kwa taariafa zaidi juu ya namna ya kujikinga, soma Sura kuhusu “uzazi wa mpango”, “maambukizi kupitia ngono”, VVU na “afya ya kingono”(sexual health).

Uhusiano wa kimapenzi bila kufanya ngono.

msichana na mvulana wamekaa kwenye benchi wakiwa wamekumbatiana

Kujenga uhusiano wenye upendo huhitaji muda, kujaliana, kuheshimiana na kuaminiana kutoka pande zote mbili. Ngono siyo njia pekee ya kumuonesha mtu mwingine kwamba unamjali. Kufanya ngono hakumaanishi kwamba unampenda.

Unaweza kutumia muda wako mwingi kukaa naye bila kufanya ngono. Kwa kuongea na kubadilishana uzoefu, unaweza kujifunza mambo muhimu juu ya mwenzio – mtazamo wa mwenzio juu ya maisha, maamuzi ambayo mnaweza kuyafanya pamoja, aina gani ya mwenzi au mzazi mwenzio anaweza kuwa, na kila mmoja anaionaje mipango ya maisha ya mwenzake. Kugusana au kupapasana (bila kufanya ngono) kunaweza kutosheleza na si hatari, ilimradi usipelekei kushindwa kujidhibiti na kuishia kufanya ngono wakati haupo tayari.

Ongea na mpenzi wako wa kiume. Kama una uhakika kwamba yeye ndiyo mtu sahihi kwako, lakini bado huna uhakika iwapo unataka kufanya ngono, zungumzia njia tofauti za kuweza kusubiri. Unaweza kukuta kwamba hata yeye pia hajawa tayari kwa ajili ya tendo la ngono. Kama mtaheshimiana mtaweza kufanya uamuzi pamoja.

Ongea na marafiki zako. Unaweza kugundua kuwa baadhi ya wasichana wenzako wenye marafiki wa kiume wanakabiliana na changamoto kama za kwako katika kufanya maamuzi juu ya maisha. Mnaweza kusaidiana kwa pamoja kutafuta njia za kuwa na mahusiano mazuri pasipo kufanya ngono. Lakini fikiria mara mbili juu ya ushauri kutoka kwa rafiki ambaye tayari yupo kwenye uhusiano wa kingono. Rafiki yako anaweza kukushawishi kufanya anavyofanya yeye ili ajisikie kwamba anachokifanya ni halali. Hii huitwa shinikizo la rika.

HAJA YA KUJIKINGA KAMA UKO TAYARI KUFANYA NGONO

msichana na mvulana wamekaa kwa kukaribiana moja akimkumbatia mwenzake
Kama kweli anakujali, atapenda kukulinda. Kama anakushinikiza kufanya ngono, huenda anajijali mwenyewe tu.

Wakati unapoamua kwamba upo tayari kuwa na uhusiano wa kimapenzi, unapaswa kujikinga dhidi ya mimba na magonjwa ambukizi. Zipo njia mbalimbali za kufanya mapenzi salama. Hii inamaanisha kwamba unapaswa kujiandaa kabla ya kujamiiana.

Ongea na mpenzi wako wa kiume kabla ya kufanya ngono. Mweleweshe umuhimu wa kujikinga. Kama itakuwa vigumu kwako kulizungumzia, pengine anza kwa kuwaongelea wenzi wengine.

msichana akimsikiliza mwanamke aliyemshika begani wakati wakitembea

Jamii nyingi zina watu ambao wamepewa mafunzo maalum ya kusambaza kondomu na kutoa njia zingine za uzazi wa mpango. Zungumza nao au waulize wafanyakazi wa afya mahali pa kupata huduma za kujikinga. Kama utapata aibu kuulizia, mtafute mtu unayemwamini ili akusaidie kuuliza. Baadhi ya kliniki zina huduma maalum za uzazi wa mpango kwa ajili ya vijana, na wanaweza kuwa na waelimishaji rika na washauri wa vijana waliopitia mafunzo ambao wanaweza kukusaidia kupatia taarifa.

Kwa vile huwezi kutambua iwapo mvulana ana maambukizi ya ngono au VVU, basi ngono inakuwa salama tu pale unapotumia kondomu kila unapofanya ngono. Kama mwanaume anatokwa na majimaji yasiyo ya kawaida uumeni mfano usaha, au ana kidonda kwenye uume, basi ana maambukizi na bila shaka atakuambukiza!

Kama ulifanya ngono na baadaye ukagundua majimaji yasiyo ya kawaida yakitoka ukeni, vidonda kwenye via vya uzazi au maumivu sehemu ya chini ya tumbo, huenda una maambukizi ya ngono. Kwa taarifa zaidi, soma zaidi sura kuhusu “Maambukizi Yanayopitia Ngono”.


Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Feb 2018