Hesperian Health Guides

Kushinikizwa au kulazimishwa kufanya ngono

Kushinikizwa au kulaghaiwa na mpenzi wa kiume kufanya ngono

msichana akimsukuma kumtoa mvulana ambaye anataka kumlazimisha kufanya ngono
Mtu akikulazimisha kufanya ngono kama hutaki ni ubakaji.

Duniani kote, wasichana wenye umri mdogo na wanawake hulazimishwa kufanya ngono hata wanapokuwa hawataki. Mara nyingi, hulazimishwa na wapenzi wao wa kiume ambao wanadai kuwapenda. Anaweza kutotumia nguvu za kimwili. Lakini unaweza kuhisi shinikizo hilo kutokana na maneno makali au hisia zake. Anaweza kukutishia au kusema “leo nitajua kama unanipenda au la” au kukufanya ujisikie mwenye hatia au aibu kama hutafanya ngono. Hii siyo sahihi. Mtu yoyote hapaswi kulazimishwa kufanya ngono kama hataki.

Kuzuia kitendo cha kulazimishwa au kulaghaiwa kufanya ngono na mpenzi wa kiume:
  • Kama anataka mfanye ngono na wewe hutaki, unaweza kumwambia kuwa umeguswa sana na ombi lake lakini hupo tayari. Kama unaogopa kuwa peke yako ukiwa naye, jitahidi kuwa na mtu mwingine, au omba mtu mwingine aongee naye.
msichana akimsukuma mvulana ambaye anataka kumshikashika
Hapana!
  • Sema"HAPANA" kwa sauti kama unalazimishwa kufanya ngono. Endelea kusema "HAPANA" kama itabidi ufanye hivyo. Pia sema hapana kwa kutumia mwili wako. Kama unasema "HAPANA," lakini ukalegeza mwili wako, atafikiria unamaanisha "ndiyo."
  • Toka, jiondoe kama unashikwashikwa au kuguswa tu kwa njia ambayo hupendi. Hisia au fikra zako ni onyo au tahadhari kwamba jambo baya zaidi linaweza kutokea. Piga kelele sana na kuwa tayari kukimbia kama itabidi.
  • Usinywe pombe au kutumia madawa ya kulevya. Pombe na madawa ya kulevya hukufanya upungukiwe uwezo wa kuamua kwa usahihi na kudhibiti chochote kitakachokutokea.
  • Tembea katika makundi. Katika sehemu nyingi, vijana hutafuta wapenzi au kukutana nao wakiwa katika makundi. Unaweza kujenga uhusiano na mvulana, lakini usishinikizwe kufanya ngono kwa sababu hutakuwa peke yako.
  • Tembelea tu sehemu ambazo ni salama mahali wengine wanaweza kukuona.
  • Panga kabla hamjakutana. Amua kiwango cha kushikanashikana au kuguswa ambacho hutavumilia. Usinaswe na hisia zako mwenyewe na kuruhusu jambo lolote ambalo hukukusudia kukupata au kukutokea.

Kama mwanafamilia atajaribu kufanya ngono na wewe

Daima siyo sahihi kwa mtu yoyote kukugusa kama hutaki kuguswa. Wanafamilia, kama vile watoto wa baba au mama mdogo, mkubwa au shangazi; wajomba, kaka zako au baba hapaswi kugusa sehemu zako za siri au sehemu yoyote ya mwili wako kwa lengo la kuamsha hisia za ngono. Kama hili litatokea, unahitaji kupata msaada. Hata kama mwanaume atakutishia kukuumiza kama utasema, unahitaji kumwambia mtu mzima unayemwamini haraka iwezekanavyo. Wakati mwingine ni bora zaidi kumwambia mtu nje ya familia yako kama vile mwalimu wa kike au kiongozi wa dini katika jamii yako.

Wasichana wadogo na mwanaume mwenye umri mkubwa

mwanaume akiongea na wasichana 2 waliosimama pembeni ya gari lake

Baadhi ya wasichana huvutiwa na wanaume wenye umri mkubwa. Kuwa na uhusiano wa mapenzi na mwanaume mwenye umri mkubwa kunaweza kuonekana jambo lenye raha sana, hususan kama ni mtu maarufu kwenye jamii yako, au kama ana fedha na anaweza kukununulia vitu mbalimbali ambavyo vinavutia. Katika baadhi ya sehemu mwanaume anayemnunulia mpenzi wake wa kike zawadi nyingi huitwa ‘Suga Dadi ’. Hata hivyo, mara nyingi msichana ambaye anatembea na mwanume mwenye umri mkubwa huishia na hisia mbaya kwamba alitumiwa kwa ajili ya ngono au kutumiwa vibaya, hasa kama mwananume ameoa au ana wanawake wengine.

Wakati mwingine mwanaume mwenye umri mkubwa anaweza kumweka mwanamke mwenye umri mdogo katika shinikizo kubwa la kufanya ngono kuliko vijana au wavulana wenye umri wake, hasa kama ana mamlaka juu yake.

wasichana 2 ndugu wakiongea pamoja na baada ya hapo kuongea na wazazi wao; na baadaye wazazi wanaongea na mwanaume anayetuhumiwa
Usimruhusu Bw. Chifeve kukuingiza katika jambo hilo, Tarisai. Unamkumbuka Alice? Alimpa ujauzito na kulazimika kuacha shule. Nitakusaidia kuwambia Mama and Baba.
Kaa mbali na binti yetu !

Kuwatumia wasichana kupata fedha na mahitaji mengine

Wakati mwingine familia yenye hali duni inaweza kumtoa binti yao kwa mwanaume mwenye umri mkubwa kulipia deni la familia. Au wanaweza kumtumia kibiashara kupata fedha au kitu kingine ambacho familia inakihitaji.

mwanaume na mwanamke wakimtoa binti yao kwa mwanaume mwenye umri mkubwa

Wakati mwingine wasichana hupelekwa kwenye mji au jiji lingine. Huwa wanafikiri wanakwenda kufanya kazi kwenye viwanda, au kama wahudumu, lakini mara nyingi hulazimishwa kufanya biashara ya ngono.

Kama unadhani wewe au msichana mwingine katika jamii yako anakwenda kuuzwa kama mke kwa mwanaume, au kupelekwa mbali kufanya kazi, jaribu kupata msaada kutoka kwa mtu mzima mwingine anayeaminika. Shangazi au mjomba, au mwalimu mwanamke anaweza kusaidia.

Iwapo utapata ujauzito bila kukusudia

mwanamke mwenye umri mdogo akilia

Unaweza kuwa na ujauzito kama ulifanya ngono na sasa hedhi yako ya mwezi imechelewa, maziwa yako yanauma, unakojoa mara kwa mara au unahisi kutapika. Pata ushauri kutoka mfanyakazi wa afya au mkunga unayemwamini haraka iwezekanavyo kupata uhakika kama ni mjamzito.

msichana akiongea na mwanamke mwenye umri mkubwa
Ongea na mtu mwenye umri mkubwa kukuzidi unayemuamini.
Maisha yako yana thamani kubwa sana na hayapaswi kupotea.

Wasichana wengi wenye umri mdogo hupata ujauzito bila kutaka. Baadhi yao huweza kupata msaada wanaohitaji kutoka kwa familia na marafiki. Kwa wengine, siyo rahisi kiasi hicho.

Kama unahisi kunaswa na mtego wa mimba ambayo hukupanga na unataka kuisitisha, tafadhali kuwa mwangalifu na maamuzi utakayoyafanya. Duniani kote, maelfu ya wasichana na wanawake hupoteza maisha wakijaribu kutoa mimba kwa kutumia njia hatari. Kuna njia salama za kusitisha ujauzito.Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Feb 2018