Hesperian Health Guides

Matatizo ya kiafya kwa watoto wachanga ambao ndiyo wanatoka kuzaliwa

Katika sura hii:

Mtoto mchanga mwenye afya hupumua kwa urahisi, bila msukumo. Anapaswa kunyonya kila saa 2 hadi 4 na kuamka peke yake bila kuamshwa anaposikia njaa au kujilowesha. Ngozi yake inakuwa safi au inakuwa na wekundu mdogo kwa mbali au na upele mdogomdogo ambao hutoweka baada ya siku chache. Mtoto ambaye haonyeshi mambo hayo anaweza kuwa na matatizo na anahitaji msaada wa haraka.

Magonjwa ambayo huchukua siku au wiki kadhaa kuua watu wazima yanaweza kumuua mtoto ndani ya saa chache.

Maambukizi

Maambukizi kwa mtoto mchanga ambaye amezaliwa siyo muda mrefu uliopita yanweza kuwa hatari sana na huhitaji tiba kwa kutumia antibiotiki mara moja (angalia Antibiotiki hupambana maambukizi). Kwa kutegemea umbali wako kutoka kwenye kituo cha afya na dawa ulizonazo, unatakiwa kutafuta msaada mara moja au kutoa tiba wewe mwenyewe-hata kama njiani utapata msaada.

Dalili za hatari
  • Kupumua haraka haraka: zaidi ya pumzi 60 kwa dakika wakati amelala au akiwa amepumzika.
  • Kupata hewa kwa shida: Kifua kuvuta ndani, mtoto kukoroma, pua kulazimika kutanuka na kufunguka wakati wa kulala au kupumzika.
NWTND Newb Page 12-1.png
kifua kinavuta kwa ndani
pua kutanuka
  • Homa, zaidi ya nyuzi joto 37.5º sentigredi, au joto la mwili kushuka chini ya nyuzi joto 35.5º sentigredi.
  • Upele mkali ukiandamana na vipele vikubwa vingi au malengelenge (upele mdogo ni jambo la kawaida.)
  • Mtoto kuacha kunyonya.
  • Mtoto kuamka kwa nadra kutoka usingizini, au kuonekana kutokuitikia kwa njia yoyote ili.
  • Dalili zinazofanana na kifafa: kupoteza fahamu na kurusha viungo vya mwili.


Dalili yoyote kati ya hizo humaanisha kuwa mtoto anahitaji matibabu.

Matibabu

Kama unadhani mtoto ana maambukizi ingawa siyo makali mpe ampisilini au amoksilini, lakini kwa maambukizi makali choma sindano ya ampisilini na jentamaisini mara moja na kutafuta msaada wa daktari. Kiwango cha dawa kitategemea uzito na umri wa mtoto.

Mtoto anapaswa kuanza kupata nafuu ndani ya siku 2. Kama hatapata nafuu katika muda huo, dawa tofauti za antibiotiki zinahitajika kuponya maisha yake.

NWTND Newb Page 13-1.png
Vidonge vya antibiotiki vinaweza kusagwa na kuchanganywa kwenye maziwa ya mama na kumpa mtoto. Lakini baadhi ya antibiotiki lazima zitolewe kwa njia ya sindano. Hizi huchomwa kwenye mshipa mrefu upande wa paja. Angalia Dawa, vipimo na tiba (kinaandaliwa) kuhusu jinsi ya kuchoma sindano kwa usalama.
Kama mama alipatwa na homa wakati wa uchungu wa uzazi, kuwa mwangalifu zaidi kwa ajili ya dalili za hatari kwa mtoto. Vilevile, mtoto ambaye aliyejisaidia kinyesi angali tumboni wakati mwingine anaweza kuvuta ndani kinyesi hiki wakati wakuzaliwa kupitia pumzi. (Majimaji ya uzazi yangekuwa na vipande vidogo vya rangi ya udongo au kijani kutokana na kinyesi. Au ngozi ya mtoto ingekuwa na madoa ya njano njano wakati wa kuzaliwa). Hii inaweza kusababisha maambukizi kwenye mapafu katika siku za mwanzo. Hivyo kuwa tayari kumtibu mtoto haraka mara dalili za maambukizi zinapojitokeza.

Kulia

Mwanaume akiwa amembeba mtoto ambaye analia akimbembeleza wakati akiongea na mwanamke.
Hebu nimshike mtoto upate kupumzika.

Baadhi ya watoto wachanga hulia sana kuliko wengine. Mtoto anayelia sana anaweza kuwa salama iwapo dalili zake zingine za kiafya ni kawaida. Angalia iwapo anapumua vizuri anapokuwa halii. Hali ya kulia karibu muda wote, na kuzidi hasa usiku, wakati mwingine husababishwa na tumbo kusokota. Hali hii kawaida hupungua baada ya miezi 3. Lakini ugumu unakuwa zaidi kwa familia kuliko hata kwa mtoto. Kuwa na huruma kwa mama ambaye ndiyo amejifungua. Hakikisha anapata muda wakupumzika na kila msaada anaouhitaji. Kama mtoto atakuwa analia muda mrefu mchana na pia hanyonyi, ana homa, au ana matatizo katika kupumua, hii inaweza kuwa dalili ya maambukizi.

Kutapika

NWTND Newb Page 14-1.png

Watoto wachanga hucheua maziwa. Wakati mwingine yanakuwa mengi na kuweza kupita mdomoni au puani. Kucheua maziwa siyo tatizo kama mtoto atakuwa ananyonya mara kwa mara na kuongezeka uzito. Jaribu kumbeba wima baada ya kunyonya. Mtoto atakuwa anatapika iwapo atatumia nguvu-badala ya maziwa kuwa yanatoka yenyewe na kumwagika nje.

Dalili za hatari
  • Kutapika mara moja baada ya nyingine, au kutoweza kutunza chochote tumboni
  • Kutapika damu
  • Ana dalili ya kupungukiwa na maji mwilini
Kumsaidia mtoto kucheua.
Mbebe mtoto juu ya bega lako au goti na kumpigapiga polepole mgongoni na kiganya chako baada ya kunyonya. Hii itamsaidia kupandisha hewa aliyomeza wakati ananyonya

Kumwongezea maji mwilini (anapokuwa hana maji ya kutosha mwilini)

Watoto hupungukiwa maji mwilini kwa urahisi, na hali ni hatari hasa kwa watoto wachanga.

Visababishi
  • Kuharisha
  • Kutapika
  • Kunyonyeshwa chini ya kila saa 2 hadi 4
  • Kula au kunywa chochote ambacho siyo maziwa ya mama (mfano maziwa ya kopo,uji, au maji.)
  • Hali ya hewa yenye joto
Dalili
  • Kukojoa mara chache, au mkojo wenye rangi nzito, na harufu kali
  • Mdomo na ulimi mkavu
  • Macho kutochangamka na ngozi kusinyaa kiasi

Lakini mtoto yeyote anaweza kupungukiwa maji mwilini.

Kupungukiwa maji sana kunaweza kusababisha macho, na utosi kurudi ndani, uzito kupungua, na ngozi ya mwili inapovutwa au kubonyezwa ndani kuchukua muda kurudi katika hali yake ya kawaida.

NWTND Newb Page 15-1.png
Matibabu

Dalili ya kwanza ya kupungukiwa maji mwilini inapoonekana,au kama mtoto anaharisha au kutapika, mtoto anyonyeshwe mara nyingi zaidi kadri atakavyoweza kunyonya. Mwamshe mtoto kunyonya angalau kila baada ya saa 2. Unaweza pia kumpatia kinywaji maalum cha kumuongezea maji mwilini. Kinywaji hiki ni mchanganyiko rahisi wa maji yalioyongezewa chumvi na sukari.Mtoto apatiwe kinywaji hiki baada ya kunyonyeshwa. Kwa nadra sana, mwanamke anaweza kuwa ananyonyesha kila baada ya muda lakini hazalishi maziwa ya kutosha (bonyeza hapa).

Kama mtoto aliyepungukiwa maji mwilini hapati nafuu baada ya saa chache, tafuta msaada wa daktari kusaidia kumuongezea maji.

Upele

Watoto wachanga hupatwa na upele, madoa, tofauti ya rangi ya ngozi sehemu mbalimbali mwilini, mambo ambayo hayana madhara na hutoweka bila matibabu yeyote. Upele sehemu za chini husababishwa na ngozi kubaki katika hali ya unyevunyevu kutokana na mkojo au kinyesi. Safisha sehemu hiyo kila baada ya muda mfupi. Badilisha nepi na nguo mara baada ya kulowa au kuchafuka. Kwa mtoto mkubwa zaidi na wapo hakuna baridi siku hiyo, unaweza kumuacha bila kumvalisha nepi ili aweze kupona. Mafuta ya zinki oksaidi yanaweza kusaidia. Iwapo tatizo hilo haliponi ndani ya siku chache, huenda ana maambukizi. Tumia dawa ya nistatini (nystatin).

Iwapo mtoto ana malengelenge au vipele vingi, hasa kama mtoto anaonekana kuwa mgonjwa au ana homa, huenda kuna maambukizi. Iwapo hakutakuwa na mabadiliko haraka, au kama dalili za maambukizi zitazidi kuwa mabaya zaidi, mpatie dawa ya antibiotiki iliyoorodheshwa hapa.

Homa ya manjano

Tatizo la ngozi ya njano au macho kuwa ya njano hujulikana kama homa ya manjano. Kwa mtoto mweusi, chunguza macho yake. Homa ya manjano katika siku ya 1, 2 hadi ya 5 baada ya kuzaliwa siyo hatari. Tiba bora zaidi ni kunyonyesha mara kwa mara. Hii itasaidia mtoto kutoa kemikali ambayo inamfanya kugeuka rangi ya njano. Muamshe kila baada ya saa mbili kunyonya. Mwanga wa jua pia husaidia. Kaa na mtoto akiwa uchi juani kwa dakika 15 au zaidi, mara kadhaa kwa siku.

Dalili za hatari
  • Kemikali ya njano huanza kuzalishwa mara moja-ndani ya saa 24 za mwanzo wa maisha.
  • Homa ya manjano huanza baadaye, lakini hufunika mwili mzima.
  • Mtoto mwenye homa ya manjano huwa na usingizi kila mara, au hawezi kuamshwa kunyonya.

Pata msaada iwapo utaona dalili zozote kama hizo.

Macho

jicho lenye tongotongo zito

Njia ndogo ambazo huruhusu machozi na mafuta kupita ili kulainisha jicho zinaweza kuziba na kusababisha macho kujaa tongotongo.Safisha macho vizuri kwa kutumia kitambaa kilicholoweshwa. Tumia kitambaa tofauti kwa ajili ya kila jicho. Kwa njia hii, kama kuna maambukizi kwenye jicho moja, hayataenea hadi jicho lingine.

Wanawake wengi wana kisonono au klamidia lakini hawajijui kwamba wameambukizwa. Tiba ya antibiotiki ya macho mara baada ya mtoto kuzaliwa itasaidia kuzuia matatizo ya macho yanayohusiana na kisonono ambacho kimetoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Jicho jekundu lenye kovu zilizovimba na pia usaha uliochanganyika na damu baada ya mtoto kufikisha siku 5 zinaweza kuwa dalili za maambukizi ya klamidia machoni. Matibabu ya klamidia ni erithromaisini kwa njia ya mdomo, kwa kuisaga na kuchanganya na maziwa kidogo ya mama na kumpa mtoto. Matibabu ya kisonono ni sindano ya seftriakzoni. Kama huwezi kufanya kipimo kubainisha ugonjwa gani unasababisha maambukizi, toa dawa kwa magonjwa yote mawili. Mama na baba pia wanapaswa kupata matibabu ya magonjwa ya klamidia na kisonono. Angalia Matatizo na magonjwa ya sehemu ya ukeni na umeni (kinaadaliwa). Iwapo maambukizi ya macho hayatapungua ndani ya siku 1 au 2, atahitaji kutibiwa na dawa nyingine ya antibiotiki ili kuzuia upofu. Tafuta msaada.

Utosi kuigia ndani

Sehemu ya utosi kichwani inapaswa kuwa bapa. Utosi ulioingia ndani au kuvimba zote ni dalili za matatizo hatari.

NWTND Newb Page 16-3.png
NWTND Newb Page 16-2.png
Utosi kuingia ndani ni dalili ya kupungukiwa na maji mwilini. Mnyonyeshe mtoto mara nyingi zaidi na kumpatia kinywaji maalum cha kumuongezea maji. Utosi kuvimba ni dalili ya homa ya uti wa mgongo. Mpatie dawa ya antibiotiki.

Kiunga mwana

Baada ya kiunga mwana kukatwa , acha kisiki chake kibaki wazi .Usikifunike. Weka nepi na nguo mbali. Epuka kukigusa, lakini iwapo ni lazima, kwanza nawa mikono yako kwa maji na sabuni. Kama kisiki hicho au sehemu inayokizunguka itachafuka, au kugandwa na damu iliyokauka, safisha na sabuni na maji kwa kitambaa kisafi sana.

Iwapo mama atafunika kisiki hicho cha kiunga mwana na kitambaa, hakikisha ni kisafi na hakibani, na badilisha kitambaa hicho mara kadhaa kila siku.

NWTND Newb Page 17-1.png
Usiguseguse kiunga mwana cha mtoto-ili umwepushe maambukizi.

Kisiki hicho kinapaswa kukauka na kudondoka ndani ya wiki moja.

Iwapo eneo linalozunguka kisiki hicho linageuka kuwa jekundu au kupata moto, kutoa harufu mbaya, au kutunga usaha, inawezekana maambukizi yameingia. Safisha vizuri na kumpatia mtoto dawa ya amoksilini.

Iwapo usa wa mtoto umekunjamana, hawezi kunyonya,au anaonekana kukakamaa, hasa kama eneo la kisiki linaoenekana kuwa na maambukizi, mtoto anaweza kuwa na pepopunda (tetanasi). Hii ni hali ya hatari. Angalia Huduma ya kwanza.