Hesperian Health Guides

Matatizo ya kiafya ya watoto wachanga ambao ndiyo wanatoka kuzaliwa

In this chapter:


Mtoto mchanga mwenye afya hupumua kwa urahisi, bila msukumo. Anapaswa kunyonya kila saa 2 hadi 4 na kuamka peke yake bila kuamshwa anaposikia njaa au kujilowesha. Ngozi yake inakuwa safi au inakuwa na wekundu mdogo kwa mbali au na upele mdogomdogo ambao hutoweka baada ya siku chache. Mtoto ambaye haonyeshi mambo hayo anaweza kuwa na matatizo na anahitaji msaada wa haraka.

Magonjwa ambayo huchukua siku au wiki kadhaa kuua watu wazima yanaweza kumuua mtoto ndani ya saa chache


Maambukizi

Maambukizi kwa mtoto mchanga ambaye amezaliwa siyo muda mrefu uliopita ni hatari sana na huhitaji tiba kwa kutumia antibiotiki mara moja. Kwa kutegemea umbali wako kutoka kwenye kituo cha afya na dawa ulizonazo, unatakiwa kutafuta msaada mara moja au kutoa tiba wewe mwenyewe-hata kama njiani utapata msaada.

Dalili za hatari

  • Kupumua haraka haraka: zaidi ya pumzi 60 kwa dakika wakati amelala au akiwa amepumzika.
  • Kupata hewa kwa shida: Kifua kuvuta ndani, mtoto kukoroma, pua kulazimika kutanuka na kufunguka wakati wa kulala au kupumzika.
NWTND Newb Page 12-1.png
kifua kinavuta kwa ndani
pua kutanuka
  • Homa, zaidi ya nyuzi joto 37.5º sentigredi, au joto la mwili kushuka chini ya nyuzi joto 35.5º sentigredi.
  • Upele mkali ukiandamana na vipele vikubwa vingi au malengelenge. (Upele mdogo ni jambo la kawaida.)
  • Mtoto kuacha kunyonya.
  • Mtoto kuamka kwa nadra kutoka usingizini, au kuonekana kutokuitikia kwa njia yoyote ili.
  • Dalili zinazofanana na kifafa: kupoteza fahamu na kurusha viungo vya mwili.


Dalili yoyote kati ya hizo inaweza kumaanisha kuwa mtoto amepata ambukizo. Iwapo mtoto ana dalili zaidi ya moja, yuko hatarini zaidi na anahitaji kupatiwa antibiotiki haraka. Kama ana dalili moja, lakini hapati nafuu haraka, anahitaji kutibiwa.

Iwapo mama alikuwa na homa wakati wa uchungu wa uzazi, kuwa mwangalifu zaidi kuchunguza dalili zozote za hatari ambazo anaweza kuwa nazo mtoto. Vilevile, mtoto ambaye alijisaidia haja kubwa angali bado tumboni anaweza kuvuta kinyesi hiki wakati akipumua mara anapozaliwa. (Majimaji ya uzazi yanaweza kuwa na vitu vya rangi ya udongo au kuonekana na rangi inayoelekea kwenye kijani kutokana na kinyesi hicho. Au ngozi ya mtoto inaweza kuwa ilichafuliwa na kuwa na sehemu zenye rangi inayoelekea kwenye njano wakati mtoto anapozaliwa.) Hali hii inaweza kusababisha maambukizi kwenye mapafu katika siku chache za mwanzo. Hivyo, kuwa tayari kutibu watoto kama hao haraka mara dalili ya kwanza inapojitokeza.

Matibabu

Choma sindano ya ampisilini na jentamaisini mara moja. Endelea kumtibu kwa siku tano. Kiwango cha dawa kitategemea na uzito wa mtoto.

Mtoto anapaswa kuanza kupata nafuu ndani ya siku 2. Kama hatapata nafuu katika muda huo, dawa tofauti za antibiotiki zinahitajika kuponya maisha yake. Pata msaada wa daktari haraka.

NWTND Newb Page 13-1.png
Choma sindano kwenye mshipa mrefu upande wa paja. Angalia Dawa, Vipimo na Tiba (kinaandaliwa) kuhusu jinsi ya kuchoma sindano kwa usalama.

Kulia

Mwanaume akiwa amembeba mtoto ambaye analia  akimbembeleza wakati akiongea na mwanamke.
Hebu nimshike mtoto upate kupumzika.

Baadhi ya watoto wachanga hulia sana kuliko wengine. Mtoto anayelia sana anaweza kuwa salama iwapo dalili zake zingine za kiafya ni kawaida. Angalia iwapo anapumua vizuri anapokuwa halii. Hali ya kulia karibu muda wote, na kuzidi hasa usiku, wakati mwingine husabishwa na msokoto wa tumbo. Hali hii kawaida hupungua baada ya miezi 3. Lakini ugumu unakuwa zaidi kwa familia kuliko hata kwa mtoto. Kuwa na huruma kwa mama ambaye ndiyo amejifungua. Hakikisha wanapata muda wakupumzika na kila msaada wanaouhitaji. Kama mtoto atakuwa analia muda mrefu mchana na pia hanyonyi, ana homa, au ana matatizo katika kupumua, hii inaweza kuwa dalili ya maambukizi.

Kutapika

NWTND Newb Page 14-1.png

Watoto wachanga hucheua maziwa. Wakati mwingine yanakuwa mengi na kuweza kupita mdomoni au puani. Kucheua maziwa siyo tatizo kama mtoto atakuwa ananyonya mara kwa mara na kuongezeka uzito. Jaribu kumbeba wima baada ya kunyonya. Mtoto atakuwa anatapika iwapo atatumia nguvu-badala ya maziwa kuwa yanatoka yenyewe na kumwagika nje.

Kumsaidia mtoto kucheua.
Mbebe mtoto juu ya bega lako au goti na kumpigapiga polepole mgongoni na kiganya chako baada ya kunyonya. Hii itamsaidia kupandisha hewa aliyomeza wakati ananyonya

Dalili za hatari

  • Kutapika mara moja baada ya nyingine, au kutoweza kutunza chochote tumboni
  • Kutapika damu
  • Ana dalili ya kupungukiwa na maji mwilini

Kumwongezea maji mwilini(anapokuwa hana maji ya kutosha mwilini)

Watoto hupungukiwa maji mwilini kwa urahisi, na hali ni hatari hasa kwa watoto wachanga.

Visababishi

  • Kuharisha
  • Kutapika
  • Kunyonyeshwa chini ya kila saa 2 hadi 4
  • Kula au kunywa chochote ambacho siyo maziwa ya mama (mfano maziwa ya kopo,uji, au maji.)
  • Hali ya hewa yenye joto

Dalili

  • Kukojoa mara chache, au mkojo wenye rangi nzito, na harufu kali
  • Mdomo na ulimi mkavu
  • Macho kutochangamka na ngozi kusinyaa kiasi

Lakini mtoto yeyote anaweza kupungukiwa maji mwilini.

Kupungukiwa maji sana kunaweza kusababisha macho kurudi ndani, utosi kurudi ndani, uzito kupungua, na mwili kushindwa kuitikia ipasavyo.

NWTND Newb Page 15-1.png

Matibabu

Dalili ya kwanza ya kupungukiwa maji mwilini inapoonekana,au kama mtoto anaharisha au kutapika, mtoto anyonyeshwe mara nyingi zaidi kadri atakavyoweza kunyonya. Mwamshe mtoto kunyonya angalau kila baada ya saa 2. Unaweza pia kumpatia kinywaji maalum cha kumuongezea maji mwilini (kinaandaliwa). Kinywaji hiki ni mchanganyiko rahisi wa maji yalioyongezewa chumvi na sukari.Mtoto apatiwe kinywaji hiki baada ya kunyonyeshwa. Kwa nadra sana, mwanamke anaweza kuwa ananyonyesha kila baada ya muda lakini hazalishi maziwa ya kutosha (bonyeza hapa).

Kama mtoto aliyepungukiwa maji mwilini hapati nafuu baada ya saa chache, tafuta msaada wa daktari kusaidia kumuongezea maji.

Upele

Watoto wachanga hupatwa na upele, madoa, tofauti kwenye rangi sehemu mbalimbali ya mwili , mambo ambayo hayana madhara na hutoweka bila matibabu yeyote. Upele sehemu za chini husababishwa na ngozi kubaki katika hali ya unyevunyevu kutokana na mkojo au kinyesi. Safisha eneo hilo kila baada ya muda mfupi. Badilisha nepi na nguo zilizolowa mara baada ya kulowa au kuchafuka. Kwa mtoto mkubwa zaidi na ikiwa ni siku isiyo na baridi, unaweza kumuacha bila kumvalisha nepi ili kumwezesha kupona. Mafuta ya zinki oksaidi yanaweza kusaidia. Iwapo tatizo hilo haliponi ndani ya siku chache, huenda ana maambukizi. Tumia dawa ya nistatini (nystatin).

Iwapo mtoto ana malengelenge au vipele vingi, hasa kama mtoto anaonekana kuwa mgonjwa au ana homa, huenda kuna maambukizi. Iwapo hakutakuwa na mabadiliko haraka, au kama dalili za maambukizi zitazidi kuwa mabaya zaidi, mpatie dawa ya antibiotiki iliyoorodheshwa hapa.

Homa ya manjano

Tatizo ya ngozi ya njano au macho kuwa ya njano hujulikana kama homa ya manjano. Kwa mtoto mweusi, chunguza macho yake. Homa ya manjano katika siku ya kwanza, pili hadi tano baada ya kuzaliwa siyo hatari. Tiba bora zaidi ni kunyonyesha mara kwa mara. Hii itasaidia mtoto kutoa kemikali ambayo inamfanya kugeuka rangi ya njano. Muamshe kila baada ya saa mbili kunyonya. Mwanga wa jua pia husaidia. Kaa na mtoto akiwa uchi juani kwa dakika 15 au zaidi, mara kadhaa kwa siku.

Dalili za hatari

  • Kemikali ya njano huanza kuzalishwa mara moja-ndani ya saa 24 za mwanzo wa maisha.
  • Homa ya manjano huanza baadaye, lakini hufunika mwili mzima.
  • Mtoto mwenye homa ya manjano huwa na usingizi kila mara, au hawezi kuamshwa kunyonya.

Pata msaada iwapo utaona dalili zozote kama hizi.

Macho

jicho lenye tongotongo zito

Njia ndogo ambazo huruhusu machozi na mafuta kupita ili kulainisha jicho zinaweza kuziba na kusababisha macho kujaa tongotongo.Safisha macho vizuri kwa kutumia kitambaa kilicholoweshwa. Tumia kitambaa tofauti kwa ajili ya kila jicho. Kwa njia hii, kama kuna maambukizi kwenye jicho moja, hayataenea hadi jicho lingine.

Jicho jekundu lenye kovu zilizovimba na pia usaha uliochanganyika na damu baada ya mtoto kufikisha siku 5 zinaweza kuwa dalili za maambukizi ya klamidia au kisonono machoni. Mpatie mtoto dawa ya erithromaisini kwa njia ya mdomo, kwa kuisaga na kuchanganya na maziwa kidogo ya mama. Mama na baba pia wanapaswa kupata matibabu ya magonjwa ya klamidia na kisonono. Angalia Matatizo na magonjwa ya sehemu ya ukeni na umeni (kinaadaliwa). Iwapo maambukizi ya macho hayatapungua ndani ya siku 1 au 2, atahitaji kutibiwa na dawa nyingine ya antibiotiki .

Utosi kuigia ndani

Sehemu ya utosi kichwani inapaswa kuwa bapa. Utosi uliodumbukia ndani au kuvimba vyote ni dalili za matatizo hatari .

NWTND Newb Page 16-3.png
NWTND Newb Page 16-2.png
Utosi kudumbukia ndani ni dalili ya kupungukiwa na maji mwilini. Mnyonyeshe mtoto mara nyingi zaidi na kumpatia kinywaji maalum cha kumuongezea maji (kinaadaliwa). Utosi kuvimba ni dalili ya homa ya uti wa mgongo (kinaadaliwa). Mpatie dawa ya antibiotiki.

Kiunga mwana/rurela

Baada ya kiunga mwana kukatwa , acha kisiki chake kibaki wazi .Usikifunike. Weka nepi na nguo mbali. Epuka kukigusa, lakini iwapo ni lazima, kwanza nawa mikono yako kwa maji na sabuni. Kama kisiki hicho au sehemu inayokizunguka itachafuka, au kugandwa na damu iliyokauka, safisha na sabuni na maji kwa kitambaa kisafi sana.

Iwapo mama atafunika kisiki hicho cha kiunga mwana na kitambaa, hakikisha ni kisafi na hakibani, na badilisha kitambaa hicho mara kadhaa kila siku.

NWTND Newb Page 17-1.png
Usiguseguse kiunga mwana cha mtoto-ili umwepushe maambukizi.

Kisiki hicho kinapaswa kukauka na kudondoka ndani ya wiki moja.

Iwapo eneo linalozunguka kisiki hicho linageuka kuwa jekundu au kupata moto, kutoa harufu mbaya, au kutunga usaha, inawezekana maambukizi yameingia. Safisha vizuri na kumpatia mtoto dawa ya amoksilini.

Iwapo mtoto amekunjamana uso, hawezi kunyonya,au anaonekana kukakamaa, hasa kama huenda eneo la kisiki limepata maambukizi, mtoto anaweza kuwa na pepopunda. Hii ni hatari na inapaswa kushughulikiwa haraka sana. Angalia Huduma ya Kwanza (kinaandaliwa).