Hesperian Health Guides
Watoto Wachanga na Unyonyeshaji: Dawa
HealthWiki > Toleo Jipya: Mahali Pasipo na Daktari > Sura ya 27: Watoto wachanga na unyonyeshaji > Dawa za antibiotiki:Watoto wachanga na unyonyeshaji
Yaliyomo
Watoto Wachanga na Unyonyeshaji: Dawa
Ampisilini na amoksilini: Dawa zenye uwezo wa kupambana na maambukizi ya aina nyingi ya vijasumu
Ampisilini na amoksilini ni dawa zenye asili ya penisilini zenye uwezo wa kupambana na aina mbalimbali za vijasumu. Hii inamaanisha kuwa huua aina nyingi za bakteria kuliko dawa zingine katika kundi la penisilini. Dawa hizi mbili mara nyingi hutumika kama mbadala wa nyingine. Ukiona pendekezo la kutumia ampisilini katika kitabu hiki, kawaida unaweza kutumia amoksilini katika nafasi yake, kwa kuzingatia kipimo sahihi (angalia chini).
Ampisilini na amoksilini ni salama sana na msaada mkubwa hasa kwa watoto wachanga na watoto wenye umri mkubwa zaidi. Dawa zote mbili husaidia katika kutibu kichomi (nimonia) au maambukizi sikioni. Ampisilini pia ni muhimu katika kutibu homa ya uti wa mgongo na maambukizi mengine makali kwa watoto wachanga.

Dawa zote hizi mbili, lakini hasa ampisilini, huwa na mwelekeo wa kusababisha kichefuchefu na kuharisha. Epuka kuwapa watoto ambao tayari wanaharisha. Unaweza kuwapa dawa nyingine.
Madhara mengine ya pembeni ni upele. Pia uvimbe vimbe unaowasha kwenye ngozi ya mwili ambao huja na kutoweka ndani ya saa kadhaa huenda ni dalili ya mzio wa dawa ya penisilini. Simamisha matibabu ya dawa hiyo mara moja na usimpe mtoto huyu dawa ya penisilini tena. Madhara ya baadaye kutokana na mzio yanaweza kuwa mabaya zaidi na hata kutishia maisha. Kwa ajili ya matatizo kama hayo, dawa ya erithromaisini inaweza kutumika.
Upele uliozagaa ambao huonekana kama surua , na ambao kawaida huanza wiki moja baada ya kuanza kutumia dawa na kuchukua siku kadhaa kutoweka , siyo lazima iwe dalili ya mzio. Lakini haiwezekani kujua bayana kama upele huo umetokana na mzio au la. Hivyo ni bora zaidi kusimamisha matibabu kwa dawa hiyo.

Usugu wa mwili dhidi ya dawa hizi unazidi kuwa jambo la kawaida. Kutegemea na mahali unapoishi,dawa hizi zinaweza kutofanya kazi tena dhidi ya magojwa kadhaa yakiwemo kisonono, maambukizi ya bakteria kwenye ngozi au sehemu za ukeni /umeni na njia ya mkojo, na ugonjwa wa kuhara ukichanganyika na damu unaosababishwa na bakteria ya , shigella, na maambukizi mengine.

Ampisilini na amoksilini hufanya kazi vizuri zinapotumiwa kwa njia ya mdomo. Ili kumpa vidonge mtoto, saga vidonge hivyo au toa unga kwenye ganda na kugawanya ili kupata kiasi cha dawa unachohitaji. Halafu changanya unga huo wa dawa katika maziwa kidogo kutoka titi la mamake. Mpatie mtoto maziwa yaliyochanganywa na dawa kwa kutumia kikombe au kijiko. Ampisilini inaweza kutolewa pia kwa njia ya sindano, lakini inapaswa kutumika tu dhidi ya magonjwa makali kama vile homa ya uti wa mgongo, au wakati mtoto anatapika au hawezi kumeza.
Kama zilivyo antibiotiki (viua vijasumu) zingine, kuna kiwango cha muda kwa ajili ya kuendelea kutoa dawa hizi. Endelea kutoa dawa hadi dalili zote za maambukizi (ikiwemo homa) zipotee angalau kwa saa 24. Iwapo mtoto ana VVU, mpe dawa kwa ajili ya siku ambazo zimeorodheshwa. Vivyo hivyo, wakati mwingine kuna kiwango cha kiasi ha dawa ambacho unatakiwa kutoa. Kwa ujumla, toa kiasi cha chini kwa mtoto mwenye uzito au mwili mdogo au kwa ajili ya maambukizi ambayo siyo makali sana, na kiasi cha juu kwa mtoto mwenye unene zaidi au mwenye maambukizi makali zaidi.
AMOKSILINIKwa ajili ya maambukizi mengi ya watoto wachanga.
¼ ya kidonge chenye ganda cha miligramu 250 AU
½ kijiko cha chai (mililita 2.5) cha dawa ya maji ya miligramu 125 au mililita 5 AU
¼ kijiko cha chai (miligramu 1.25) chaa dawa ya maji ya miligramu 250 au mililita 5.
Mpatie dawa hadi saa 24 baada ya dalili zote za maambukizi kutoweka.
AMPISILINIKwa ajili ya maambukizi mengi ya watoto wachanga
½ ya kidonge chenye ganda chenye miligramu 250 AU
Kijiko 1 cha chai (miligramu 5) cha dawa ya maji ya miligramu 125 /mililita 5.
Mpatie dawa hadi saa 24 baada ya dalili zote za maambukizi kutoweka.
Kwa ajili ya maambukizi makali kwa watoto wachanga kama vile kichomi (nimonia) au uti wa mgongo
Choma sindano yenye mchanganyiko wa dawa ya ampisilini na jentamaisini (gentamicin) pembeni kwenye msuli wa paja. Angalia Dawa, Vipimo na Matibabu (kinaadaliwa) jinsi ya kuchoma sindano. Angalia taarifa hizi juu ya ampisilini, na pia angalia onyojuu ya dawa ya jentamaisini.
Erithromaisini
Erithromaisini hufanya kazi dhidi ya maambukizi mengi kama penisilini lakini gharama yake ni ghali kidogo kuliko penisilini. Katika sehemu nyingi za dunia, erithromaisini inafanya kazi vizuri zaidi kuliko penisilini kwa baadhi ya maambukizi ya kichomi (nimonia). Inaweza pia kutumika dhidi ya dondakoo na kifaduro (aina ya kikohozi kikali kinachosababishwa na bakteria ambao huwaandama sana watoto).
Kwa watu wenye mzio na penisilini, erithromaisini ni dawa mbadala mzuri. Kwa maambukizi mengi, inaweza pia kutumika badala ya tetrasaikilini.

Erithromaisini mara nyingi husababisha kichefuchefu na kuharisha , hasa miongoni mwa watoto. Usitumie kwa zaidi ya wiki 2 kwa sababu inaweza kusababisha nyongo ya manjano.

Miligramu 0.75 (hii ni zaidi kidogo ya theluthi nane - 1/8 ya kijiko cha chai) ya dawa ya maji ya enthromaisini yenye miligramu 250 /mililita 5, AU
¼ ya kidonge cha miligramu 250 kilichosagwa na kuchanganywa kwenye maziwa kutoka titi la mama au kwenye maji.
Jentamaisini
Jentamaisini ni dawa kali sana kwa ajili ya kuua vijidudu. Hutolewa tu kwa sindano au kupitia dripu (kwenye mshipa wa damu). Dawa hii inaweza kuharibu figo na uwezo wa kusikia. Hivyo itumike tu katika hali ya dharura.
Katika kutibu kichomi (nimonia) au homa ya uti wa mgongo miongoni mwa watoto wachanga na watoto wengine, toa mchanganyiko wa jentamaisini na ampisilini.

Dawa ya Jentamaisini lazima itolewe kwa kuzingatia usahihi wa dozi kamili. Kipimo cha dawa kikizidi huweza kusababisha uharibifu wa figo au uziwi wa kudumu. Toa kipimo cha dawa sahihi kinacholingana na uzito wa mtoto. Usitoe kipimo cha dawa kwa kuangalia umri wake. Na usitoe Jentamaisini kwa zidi ya siku 10. Epuka dawa iliyokolezwa - miligramu 10 kwa mililita ni bora kuliko miligramu 40 kwa mililita.
Seftriakzoni (Ceftriaxone)
Seftriakzoni ni dawa kali ambayo inaweza kutumika kutibu sumu kwenye damu kutokana na kidonda ambacho kimeoza na homa ya uti wa mgongo. Lakini ni chaguo la pili kwa sababu ni dawa yenye hatari zaidi kwa watoto wachanga. Seftriakzoni hasa husaidia sana katika kutibu kisonono, yakiwemo maambukizi ya kisonono machoni mwa watoto wachanga.

Uchomaji wa sindano ya seftriakzoni unaweza kuambatana na maumivu. Unaweza kuichanganya na asilimia moja ya lidokeni (lidocaine) iwapo unajua jinsi ya kuichanganya.

Usitoe dawa ya seftriakzoni kwa mtoto mwenye chini ya wiki moja. Epuka pia kuwapa watoto ambao walizaliwa njiti au wakiwa na uzito mdogo. Usitoe dawa hii iwapo kuna dalili ya nyongo ya manjano (jaundice).

Kwa ajili ya matibabu ya kisonono kwa watoto wachanga wenye umri wa siku 7 au zaidi
Kwa mtoto mchanga mwenye wastani wa uzito wa kilogramu 3, choma miligramu 150.
Kwa mtoto mchanga mwenye kilogramu 3, choma miligramu 225 mara moja kwa siku.
Kwa mtoto mkubwa zaidi mwenye kilogramu 6, choma miligramu 450 mara moja kwa siku.