Hesperian Health Guides

Maafa ya mlipuko wa gesi ya sumu ya Bhopal

Katika sura hii:

Mnamo usiku wa Desemba 3, 1984 katika jiji la Bhopal, India, maafa makubwa yalitokea. Kiwanda cha kutengeneza dawa za kuua wadudu ambacho kilikuwa katika eneo lenye watu wengi katika ukanda wanaoishi watu wenye kipato kidogo jijini Bhopal kilivujisha tani nyingi za gesi ya sumu kwenye hewa. Mfumo wa onyo ya tahadhari kiwandani ulizimwa, na jamii haikusikia kengele au kingora chochote kuashiria hatari.

 A woman speaking.
Aliyenusurika mmoja, Aziza alisema:
Niliamka usiku baada ya kusikia mtoto wangu akikohoa sana. Chumba kilikuwa kimejaa moshi mweupe. Nilisikia watu wakipiga kelele- kimbia… kimbia ! Hapo hapo nilianza kukohoa kila nilipojaribu kupumua, kama vile nilikuwa napumua moto!
 A woman speaking.
Mwingine aliyenusurika Champa Devu Shukla anakumbuka:
Watu waliamka ghafla na kuanza kukimbia hovyo na chochote walichokuwa wamesitiri miili yao; wengine wakiwa uchi kabisa. Walikuwa na nia moja tu ya kuponya maisha yao, na maisha ya wapendwa wao. Hivyo walikimbia tu.
Ni kama vile mtu alikuwa amejaza mwili wangu na pilipili nyekundu, macho yangu yakitiririka machozi, na pua yangu ikitoa kamasi laini. Nilikuwa na povu mdomoni.

Gesi ya sumu iliuwa watu wengi usiku huo. Baada ya siku 3 watu 8,000 walikuwa wamekufa. Lakini huu haukuwa mwisho wa maafa. Kwa ukweli huo ulikuwa ni mwanzo tu.

Baada ya miaka 20 iliyofuata, watu 20,000 walikuwa wamekufa kutokana na sumu iliyobaki kwenye miili yao. Wengi zaidi walikumbwa na matatizo makubwa ya kiafya yakiwemo maumivu na matatizo katika kupumua, kikohozi kisichopona, homa, ganzi mikononi na miguuni, udhaifu mwilini, uoga, msongo na saratani. Watoto na wajukuu wa walionusurika huzaliwa na matatizo makubwa ya viungo, yakiwemo miguu na mikono iliyodhoofu, kukua polepole,na matatizo mengi ya afya ya uzazi na mfumo wa neva. Zaidi ya watu 150,000 wameathirika kutokana na gesi ya sumu iliyovuja usiku huo jijini Bhopal.


Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022