Hesperian Health Guides

Kupigania haki za kibinadamu na kisheria kuhusiana na mazingira

Katika sura hii:

Hadi leo hii, eneo la tukio la uvujaji gesi halijawahi kusafishwa na kiwanda kilichotelekezwa kimebaki kama kumbukumbu muhimu ya maafa hayo. Malundo ya kemikali zenye sumu bado yametapakaa katika eneo la wazi, na maji yaliyoko chini ya ardhi ya Bhopal yamechafuliwa na sumu. Watu wengi hawakupata matibabu waliyohitaji. Kwa sababu hizi,watu wa Bhopal hawaamini kwamba maafa hayo yamepita. Wanaona kuwa maafa hayo bado yanaendelea na ni jambo ambalo wanalazimika kukabiliana nalo kila siku.

Kiwanda hicho cha dawa za kuua wadudu kilimilikiwa na shirika la kimataifa-kampuni kubwa inayofanya biashara katika nchi nyingiijulikanayo kama Union Carbide. Watu walionusurika maafa hayo walijua kuwa haikuwa sahihi kwa maisha yao kuangamizwa na maafa hayo. Walioathiriwa hawakuwa na fedha za matibabu au kuhudumia wanafamilia ambao wasingeweza kufanya kazi tena. Waliitaka kampuni hiyo kuwajibika. Lakini Union Carbide ilisema maafa hayo yalisababishwa na mfanyakazi mmoja kiwandani, na kukataa kuwajibika.

Kama ilivyo kwa watu wengine wanaopigania haki zao, waathirika wa maafa ya Bhopal walijua kuwa umasikini wao siyo tu ulizidisha matatizo yao, ila ulikuwa ni sehemu kubwa ya sababu ya kutokea kwa maafa hayo.

Kwa nini maafa hayo yalitokea?

Maafa ya Bhopal yalikuwa, na bado ni tukio baya sana ambalo halikustahili kutokea. Hata hivyo, pamoja na ubaya wa maafa hayo, tukio hilo halikuwa jambo la kushangaza. Zoezi la lakini kwa nini? linaweza kusaidia kuelewa sababu za msingi za maafa hayo.

A small group of people sit and discuss.
Kwa nini watu wengi kiasi hicho waliathirika kutokana na maafa hayo ya gesi ya sumu?
Kwa sababu kiwanda kilijengwa katika eneo la watu wengi masikini.
Lakini kwa nini kiwanda kilijengwa eneo hilo?
Kwa sababu serikali na kampuni ya kimataifa haikujali usalama wa watu masikini.

Duniani kote, mashirika yana tabia ya kujenga viwanda, dampo, na miradi ya viwanda vinavyochafua mazingira katika maneo ya watu masikini na wenye hadhi ndogo. Kwa njia hii, nchi masikini na jamii zao hugeuzwa kuwa majalala ya viwanda chafuzi, bidhaa na uchafu. Hii ndiyo sababu swala la kulinda afya ya mazingira siyo swala la mtu mmoja mmoja kubadili bidhaa tunazotumia, lakini sisi sote kuhoji kwa nini wale wenye uwezo mkubwa hutumia uwezo wao vibaya na kwa nini wale wenye uwezo mdogo miongoni mwetu hulazimika kuathirika kiafya.

A small group of people sit and discuss.
Lakini kwa nini kampuni ya Kimarekani ilikuwa inatengeneza viuatilifu nchini India? Lakini kwa nini serikal
Kwa sababu wangeweza kupata faida kubwa sana.
Lakini kwa nini wangeweza kupata faida kubwa sana?
Kwa kuwalipa wafanyakazi mishahara midogo na kutogharamia usalama na afya za wafanyakazi na wakazi wa eneo hilo.
Lakini kwa nini serikali za India na Marekani ziruhusu Kampuni hiyo kufanya kitu kama hiki?

Kampeni ya kimataifa kwa ajili ya haki kwa watu wa Bhopal

A man speaks as he sits on the side of a bed where a sick woman reclines; a sickly child sits next to him.
Eh Mungu janga hili lisitokee tena mahali popote duniani !

Walionusurika maafa ya uvujaji wa gesi huko Bhopal waliendesha juhudi za pamoja kutangaza masaibu yao na kutaka kampuni husika kuwajibika. Waliandaa migomo ya kuacha kula hadi wasikilizwe. Waliandamana na kutembea kilomita 750, bila kula wala kunywa maji, hadi makao makuu ya jimbo. Pia waliandamana na kutembea hadi makao makuu ya nchi kudai haki itendeke. Wanawake waliweka hema mbele ya ofisi ya Waziri Kiongozi wa Jimbo. Walikaa kwenye hema hiyo kwa miezi 3. Kila siku kuanzia mapambazuko hadi machweo, waliimba nyimbo zenye madai yao.

Miaka kadhaa baada ya maafa hayo, mahakama iliamuru kampuni ya Union Carbide kulipa Dola za Marekani milioni 460 kwa serikali ya India. Huu ulikuwa ushindi muhimu, lakini usiotosheleza. Sehemu kubwa ya fedha hizo haikuwafikia watu walioathirika. Mara baada ya hapo, kampuni ya Union Carbide iliuzwa kwa kampuni nyingine ya kimataifa iitwayo Dow chemical company. Kampuni hiyo mpya ilikataa kubeba wajibu huo au kuwasaidia walioathirika kupata matibabu. Siyo serikali ya India mahali ajali ilitokea, wala serikali ya Marekani mahali ambapo kampuni zote mbili zina makazi yao makuu, ilikuwa tayari kuwawajibisha viongozi wakuu wa kampuni hizo zilizohusika na maafa hayo.

Walionusurika na maafa hayo waliandaa kampeni ya kimataifa kuendelea na mapambano ili haki iweze kupatikana. Walijenga mtandao na kuungwa mkono na wanafunzi, vikundi vya kimazingira, na mashirika ya haki za binadamu. Kwa msaada wa watu kutoka sehemu zote duniani, waathirika wa maafa ya Bhopal walifikisha madai yao makao makuu ya kampuni ya Union Carbide na Dow chemicals. Waathirika hao waliwatia moyo wengine nao kuanza mgomo wa kutokula chakula na kuchukua hatua zingine kuonyeha mateso ya waathirika.

Na kipindi chote hicho, waathirika wameendelea kuhudumia familia zao, kujihangaikia kwa ajili ya matibabu, na kuunga mkono waathirika wa maafa mengine kama hayo. Wanaendelea kuishi.

Kauli mbiu ya kampeni kwa ajili ya upatikanaji haki ya watu wa Bhopal ni: Maafa ya Bhopal kamwe yasijirudie! Lengo lao ni kuzuia maafa kama hayo kutokea sehemu yeyote ile duniani. Kwa kuifanya kampeni yao kuwa ya kimataifa, wamefundisha watu katika sehemu mbalimbali za dunia kuhusu athari za muda mrefu kutokana na madhara ya gesi au kemikali za sumu kwa binadamu. Waathirika wa Bhopal wameionyesha dunia kwamba ajali za wiwandani zinaweza kutokea wakati wowote, na mara nyingi watu masikini na wenye uwezo mdogo ndiyo huathirika kuliko watu wengine. Mapambano ya watu wa Bhopal kwa ajili ya haki zao na upatikanaji wa haki duniani kwa ujumla ni mfano bora kwa viongozi wa jamii, wahamasishaji, wanaharakati na wapigania haki popote duniani.


Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022