Hesperian Health Guides

Shukrani

Katika sura hii:

Afya ya wanawake ipo mikononi mwako


Afya ya wanawake ipo mikononi mwako. Duniani kote, mamilioni ya wanawake huishi maeneo ya vijijini au mijini ambapo hakuna madaktari au mahali ambapo huduma za afya ni ghali sana. Wanawake wengi hupata matatizo na hata kupoteza maisha bila ulazima kutokana na kushindwa kupata huduma za afya, na kukosa taarifa sahihi kuhusu afya zao.

Kitabu hiki kimeandikwa kwa ajili ya wanawake hawa, na kwa ajili ya mtu yeyote anayependa kuboresha afya ya wanawake. Kwa kutumia lugha rahisi na mamia ya picha, kinatoa taarifa kuhusu mambo mengi yahusuyo matatizo ya afya ya wanawake. Ni matumaini yetu kwamba kila mmoja, wasichana, wanawake, na wafanyakazi ya afya – watakiona kitabu hiki kuwa muhimu na hata chenye kuokoa maisha. Lengo letu ni kutoa taarifa hizi kwa wanawake wengi iwezekanavyo, na sehemu nyingi iwezekanavyo.

Wakati wa kuandaa kitabu hiki, tuliwauliza wanawake kutoka sehemu mbalimbali duniani kuhusu mahitaji ya afya zao, imani zao, na desturi zao – na mambo mengine ambayo wangependa yawemo kwenye kitabu hiki. Wanawake kutoka sehemu nyingi duniani walikutana katika vikundi na kujadili kuhusu mada za afya na kisha wakatutumia ripoti zao. Hii ilituonyesha kwamba ingawa huduma za afya ya wanawake zimejikita katika suala la afya ya uzazi, wanawake hawa pia waliona kuwa yapo matatizo mengine muhimu kuhusu afya yao. Hivyo kitabu hiki kinajumuisha mambo mbalimbali ambayo yanaathiri afya ya wanawake. Wanawake hawa walitusaidia kuandaa kitabu hiki kupitia sauti zao, uzoefu wao na simulizi zao.Tuliongozwa na tathmini zao kuhusu ni nini muhimu zaidi, ni nini hakikueleweka vizuri au hakikuwa sahihi, na iwapo taarifa na maelezo yaliyomo yangekuwa na manufaa katika jamii zao.

Iwapo unao uwezo wa kusoma, pengine unaweza kusaidia kuwasomea wengine wasiojua kusoma. Pia unaweza kuwashirikisha wanawake wengine walio katika afya duni juu ya taarifa na maarifa yaliyomo ndani ya kitabu hiki – hiki siyo kitabu cha kutumiwa na mwanamke mmoja mmoja peke yake. Kadri tunavyogundua mambo na mawazo ambayo yanasaidia kutatua matatizo ya afya ya wanawake, kufanya kazi kwa pamoja na kujifunza kutoka kwa kila mmoja ni miongoni mwa mambo muhimu na ya lazima katika kuleta mabadiliko.


WWHND 2010 inside cover.png