Hesperian Health Guides

Hadithi ya Juanita

Katika sura hii:


Juanita anaishi katika kijiji kidogo kwenye milima ya Honduras, mahali ambapo yeye na mumewe hulima mahindi kwenye eneo dogo la ardhi. Eneo lao haliwezi kuzalisha chakula cha kuitosha familia hiyo yenye watoto watatu. Hivyo mara kadhaa kila mwaka Raulo, mumewe Juanita, pamoja na wanaume wenziwe hapo kijijini huenda Pwani kutafuta kazi katika mashamba makubwa.


mwanamke akiwa anajisaidia kwenye choo cha nje

Kiasi cha wiki tatu baada ya safari ya mwisho, mumewe Juanita alirudi nyumbani kutoka Pwani. Juanita alianza kugundua dalili za kutokwa na damu nyingi ukeni tofauti na kawaida. Kisha alianza kupata maumivu wakati wa kukojoa. Juanita alijua kwamba kulikuwa na tatizo lakini hakujua ni tatizo gani.

Juanita aliamua kuomba msaada kwa rafiki yake Suyapa. Suyapa alimshauri anywe chai iliyotengenezwa kwa mbelewele za mahindi, kwa sababu hata yeye iliwahi kumsaidia wakati alipokuwa na tatizo la maumivu wakati wa kukojoa. Hivyo, Juanita alijaribu kutumia chai hiyo – lakini maumivu na kutokwa damu havikuisha. Kisha Suyapa akamshauri atumie tiba aliyowahi kutumia rafiki yake Maria wakati alipokuwa na maumivu baada ya kujifungua. Mkunga wa jadi alikuwa amempa Maria kitambaa kilichosokotewa dawa ya majani ili aifunge kuzunguka tumbo lake. Juanita alijaribu tiba hiyo bila mafanikio. Alidhani kwamba pengine kama angekiingiza kile kitambaa ndani ya uke wake, ingesaidia. Lakini haikusaidia chochote na tatizo likaendelea.

Mwishowe, Juanita aliamua kwenda kumwona mfanyakazi wa afya, Petro. Juanita alijisikia aibu kwamba mwanaume angemchunguza ukeni, lakini hakua na jinsi kutokana na hofu ya kuwepo tatizo kubwa.

Tatizo ni nini?

Petro alimwambia Juanita kwamba ili aweze kumsaidia, alihitaji kwanza kujua kwa undani kuhusu ugonjwa huo. Hivyo alimwuliza Juanita maswali yafuatayo:

illustration of the below: health worker asking questions
  • Ni dalili gani zilikufanya uhisi kwamba kuna tatizo?
  • Ni mara ngapi umekuwa na dalili hizo? Dalili hizo zikoje?
  • Je, uliwahi kuwa na dalili hizo kabla, au unamfahamu mtu yeyote kwenye familia au jamii yako ambaye amewahi kuwa na dalili hizo?
  • Je, uliwahi kuwa na dalili hizo kabla, au kuna ye yote kwenye familia au jumuiya yako amewahi kuwa na hizo dalili kabla?
  • Je, kuna jambo lolote ambalo linafanya dalili hizo kupungua au kuzidi ?


Ni vigumu kutofautisha baadhi ya magonjwa

Baada ya kumsikiliza Juanita kwa makini akielezea maumivu yake na kutokwa na damu, Petro alieleza kwamba mara nyingi dalili zinaashiria kwa ujumla aina ya matatizo ya afya ambayo mtu anaweza kuwa nayo. Lakini wakati mwingine magonjwa kadhaa tofauti huweza kuwa na dalili zinazofanana. Kwa mfano, mabadiliko ya kiasi cha damu itokayo ukeni, rangi yake, au harufu yake, huweza kusababishwa na:

  • Magonjwa ya ngono (STDs)
  • Maambukizo ukeni ambayo hayatokani na magonjwa ya ngono.
  • Ugonjwa wa nyonga (PID) ambao kawaida ni maambukizo kwenye tumbo la uzazi na mirija yake, mara nyingi ya kisababishwa na maambukizi kupitia ngono.
  • Saratani ya shingo ya kizazi.


Ili kuweza kujua vizuri ni ugonjwa gani kwa dalili alizokuwa nazo Juanita, Petro alihitaji kujua iwapo Juanita na mumewe walikuwa wakitumia kondomu, na iwapo mmoja wao aliwahi kuwa na wenzi wingine. Juanita alihisi mumuwe alikuwa na wenzi wengine, kwa sababu alikuwa akikaa miezi kadhaa kule alikokuwa akifanyia kazi. Lakini hawakuwahi kujadili jambo hilo na hivyo hakuwa na uhakika. Mara ya mwisho mumewe alipokuja nyumbani, hata hivyo, alikuwa akilalamika juu ya maumivu wakati wa kukojoa. Alikuwa akilaumu vyakula alivyokula huko Pwani alikokuwa akifanyia kazi.

Kwa maelezo haya ya nyongeza, Petro alihisi Juanita alikuwa na ugonjwa wa ngono, huenda kisonono au klamidia. Lakini kwa vile ni vigumu kutofautisha haya magonjwa mawili, ni bora kuyatibu yote.


Ukurasa huu ulihuishwa: 20 Machi 2018