Hesperian Health Guides

Njia za kuzuia mimba

Katika sura hii:

Wanawake ambao wanataka kuzuia mimba wanaweza kufanya maamuzi bora zaidi wanapokuwa na fursa ya kuchagua kati ya njia mbalimbali. Pia wanahitaji taarifa sahihi zinazoeleweka vizuri kuhusu matumizi ya kila njia na kiwango cha ufanisi wa njia hiyo iwapo itatumika kwa usahihi. Wanaume pia watakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuhimiza uzazi wa mpango iwapo watakuwa na uelewa juu ya manufaa ya uzazi wa mpango kwa ujumla na njia mbalimbali za kuzuia mimba na jinsi ya kuzitumia.

Ili kutumia njia za kudhibiti uzazi kwa mafanikio, wanawake na wanaume wote wanahitaji kuielewa miili yao na ujinsia wao.

HAW Ch7 Page 190-1.png

Hatua ya kwanza ni kujifunza jinsi viungo vya uzazi vya wanawake na wanaume vinavyofanya kazi, na mambo gani yanatokea wakati wa tendo la ngono. Kwa taarifa zaidi soma Sura ya 4: Ujinsia na Afya ya Ujinsia (kinaandaliwa), na Mahali Wanawake Wanapokuwa Bila Daktari (kinaandaliwa).

Mwanamke yeyote ambaye ameanza kupata hedhi ya kila mwezi anaweza kutumia njia za kudhibiti uzazi. Wanawake tofauti hupendelea njia tofauti kwa sababu tofauti katika vipindi tofauti wakati wa maisha yao. Kwa mfano, mwanamke anaweza kupendelea njia moja anapokuwa kijana na kabla hajapata watoto; mwingine anaweza kupendelea njia nyingine wakati anavuta subira ili kuacha nafasi nzuri kati ya mtoto na mtoto; na njia nyingine anapoamua kutozaa tena.

Hata hivyo, wanawake wengi wanashindwa kuzuia mimba wanapotaka kufanya hivyo kwa sababu hawana taarifa sahihi juu ya uzazi wa mpango, au hawawezi kupata huduma zinazotoa nyenzo za kudhibiti uzazi.

Njia tofauti kwa mahitaji tofauti

Njia bora zaidi ya uzazi wa mpango ni ile yenye ufanisi na ambayo mwanamke anajisikia vizuri zaidi kuitumia. Sehemu ifuatayo inaonesha njia toafuti za uzazi wa mpango ili kumsaidia mwanamke kuamua njia ipi ni bora kwake.

Njia zote za kudhibiti uzazi hufanya kazi kwa ufansi zaidi zinapotumika kwa usahihi kila mara mwanamke anapotaka kuzuia mimba. Mfano kama ni kondom, mkazo ni kuitumia kwa usahihi kila mara anapofanya tendo la ngono, au kama ni vidonge vya majira kutumia kidonge muda uleule kila siku. Mfanyakazi wa afya mzoefu anaweza kumsaidia mwanamke kuamua njia ipi inayomfaa kutumia.

Njia tofauti huzuia mimba kwa namna tofauti


Njia za vizuizi (Barrier methods) huzuia mbegu ya uzazi ya mwanaume kulifikia yai la uzazi wa mwanamke. Njia hizi hutumika kila mara mwanamke anapofanya tendo la ngono. Njia hizi hazibadilishi uwezo wa mwanamke kuzaa au hedhi yake ya kila mwezi.

Kondom ndiyo njia pekee ambayo huzuia mimba na papo hapo kutoa kinga nzuri dhidi ya maambukizi kupitia ngono vikiwemo virusi vya UKIMWI (VVU). Unaweza kutumia kondom kwa wakati mmoja na njia zingine za uzazi wa mpango zikiwemo vidonge vya majira.

NJIA ZA VIZUIZI
Njia ya uzazi wa mpango Uwezo wa kuzuia mimba Taarifa zingine muhimu
Kondom ya kiume
FPChart-1.png
Mkubwa Hufanya kazi kwa ufanisi zaidi inapotumika na dawa ya kuua mbegu za kiume na kilainishi cha asili ya maji. Zinapatikana sehemu nyingi kwa bei nafuu au bila malipo.
Kondom ya kike
FPChart-2.png
Mkubwa Usitumie kwa wakati mmoja na kondom ya kiume.
Daframu (vizibo, vizuizi)
HAW Ch7 Page 191-3.png
Mkubwa Hufanya kazi kwa ufanisi zaidi inapotumika na dawa ya kuua mbegu za kiume. Hufanikiwa inapokuwa na kipimo sahihi. Huhitaji ukaguzi wa mfanyakazi wa afya. Kama itatumika mara kwa mara; inapaswa kubadilishwa baada ya miaka 5.


Njia za homoni: Njia hizi kwa muda maalum huzuia ovari za mwanamke kuachia mayai ya uzazi. Mwanamke anaposimamisha matumizi ya njia ya homoni, ovari zake huanza tena kuzalisha mayai, na anaweza kupata mimba isipokuwa kama ataanza kutumia njia nyingine ya kuzuia mimba. Njia za homoni zinaweza kusaidia kurekebisha tatizo la mwanamke kupata hedhi bila mpangilio, na kupunguza maumivu wakati wa hedhi. Ongea na mfanyakazi wa afya juu ya matumizi sahihi na madhara ya pembeni ambayo yanaweza kutokea.

<tr"> </tr>
NJIA ZA HOMONI
Njia ya uzazi wa mpango Uwezo wa kuzuia mimba Taarifa zingine muhimu
Vijiti
FPChart-6.png
Mkubwa zaidi Hufanya kazi kwa ufanisi kwa miaka 3 hadi 5 kutegemea na aina ya vijiti. Lazima vingizwe na kutolewa na mfanyakazi wa afya ambaye amepitia mafunzo.
Sindano
Sw NWTND FP Page 15-3.png
Mkubwa sana Huzuia mimba kwa mwezi 1, 2, au 3 kutegemea na aina ya sindano.
Vidonge vya majira
HAW Ch7 Page 191-6.png
Mkubwa sana Ufanisi wake ni mkubwa zaidi unapotumia kidonge 1 kila siku katika muda uleule bila kuruka kutumia kidonge chochote


Kitanzi (intrauterine devices): Hizi ni nyenzo ndogo za plastiki ambazo huingizwa kwenye kizazi cha mwanamke. Kitanzi huzuia mbegu za uzazi za mwanaume kuungana na yai la mwanamke na kulirutubisha. Pale kinapotolewa, mwanamke anaweza kupata mimba kama kawaida.

VITANZI (IUDs)
Njia ya uzazi wa mpango Uwezo wa kuzuia mimba Taarifa zingine muhimu
Kitanzi (IUD)
FPChart-7.png
Mkubwa zaidi Hufanya kazi vizuri kwa muda wa miaka 5 hadi 12, kutegemea na aina ya kitanzi. Kitanzi kinapaswa kuingizwa na mfanyakazi wa afya ambaye amepitia mafunzo maalum.


Njia za kudumu: Njia hizi zinajumuisha upasuaji ambao hautaruhusu tena yai la uzazi la mwanamke kurutubishwa na mbegu ya uzazi ya kiume. Upasuaji huu kwa wanaume unaitwa vasektomi. Upasuaji kwa mwanamke unajulikana kama kufunga kizazi.

NJIA ZA KUDUMU
Njia ya uzazi wa mpango Uwezo wa kuzuia mimba Taarifa zingine muhimu
Vasektomi
FPChart-11.png
Mkubwa zaidi Mwanamke au mwanaume hataweza kupata watoto tena baada ya upasuaji huu, lakini upasuaji huu hautaathiri uwezo wa mwanamke au mwanaume kufanya na kufurahia tendo la ngono.
Kufunga kizazi (tubal ligation)
FPChart-12.png
Mkubwa zaidi


Njia za asili: Njia hizi zinajumuisha kuepuka mwingiliano wa kingono (ume kuingizwa ukeni) mwanamke anapokuwa katika kipindi chake cha rutuba (siku za kubeba mimba). Tendo la ngono lisilohusisha kuingiliana kawaida huzuia mimba kutokea.

NJIA ZA ASILI
Njia ya uzazi wa mpango Uwezo wa kuzuia mimba Taarifa zingine muhimu
Ngono bila kuingiliana kimwili (bila kuingiza hata kidogo ume ndani ya uke)
FPChart-8.png
Mkubwa zaidi Ni nadra migusano ya kingono kusababisha maambukizi yoyote kuhusiana na ngono. Kuna uwezekano mdogo ngono kwa njia ya mdomo kusababisha maambukizi ya kingono. Ngono kwa njia ya haja kubwa husambaza maambukizi kwa urahisi, yakiwemo magonjwa ya ngono ya kawaida na VVU. Kila mara tumia kondom unapofanya ngono kwa njia ya haja kubwa.
Unyonyeshaji (katika miezi 6 ya kwanza tu)
FPChart-9.png
Mkubwa sana Katika kutumia njia hii, mwanamke lazima awe anampa mtoto wake maziwa ya mama tu, bila hata maji, kwa miezi 6 ya kwanza, na anapaswa kuwa hajaanza kupata hedhi yake ya kawaida ya kila mwezi.
Njia ya kuhesabu siku (Fertility awareness)
FPChart-10.png
Mkubwa Mwanamke anapaswa kujua lini atakuwa katika siku zake za kuweza kushika mimba (suku za rutuba), na hivyo kuepuka kufanya ngono wakati akiwa kwenye siku hizo. Baadhi ya wanawake hutumia kondom katika siku hizo badala ya kuepuka ngono kabisa.
Kuchomoa ume mwanaume anapofika kileleni
FPChart-13.png
Mdogo sana Ni vigumu sana kutumia njia hii kwa mafanikio. Hata kama mwanaume atachomoa ume, majimaji kidogo yenye mbegu za kiume yanaweza kuingia ukeni na kusababisha mimba.


Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya hali na njia ambazo wanawake wanaweza kupendelea:


wanawake wawili wawili wakiwa wanaongea, yakifuatia mapendekezo kwa ajili ya kila mmoja wapo.
Nataka niendelee kupata hedhi yangu kila mwezi kama kawaida.
Sitaki kulazimika kufanya jambo Fulani kila siku.
Unaweza kupendelea: Njia za vizuizi na kitanzi

Unaweza kuepuka: Njia ya vijiti, sindano za majira
Unaweza kupendelea: Njia ya vijiti, sindano za majira, na kitanzi

Unaweza kuepuka: Vidonge vya majira, njia za asili
HAW Ch7 Page 193-2.png
Sitaki wazazi wangu wajue kuwa natumia njia ya kuzuia mimba
Sitaki kuweka au kupandikiza vitu kwenye uke wangu au kwenye kizazi changu.
Unaweza kupendelea: Sindano za majira, njia za vizuizi

Unaweza kuepuka: Vidonge vya majira, vijiti
Unaweza kupendelea: Njia za homoni, kondom ya kiume, njia za asili

Unaweza kuepuka: Deframu-Vizuizi (Diaphragm), kondom ya kike, kitanzi


HAW Ch7 Page 193-3.png
Nataka niwe huru kufanya tendo la ngono wakati wote ninapojisikia bila vikwazo.
Sitaki kuzaa watoto tena.
Unaweza kupendelea: Njia za homoni, kitanzi

Unaweza kuepuka: Njia ya vizuizi, njia za asili
Unaweza kupendelea: kufunga uzazi kabisa, njia ya vijiti, sindano za majira, kitanzi

Unaweza kuepuka: Njia za asili, vizuizi, vidonge vya majira
HAW Ch7 Page 193-4.png
Nataka kupata mtoto ndani ya mwaka mmoja.
Nina hofu mwenzangu amefanya ngono na watu wengi na anaweza kuni-ambukiza magonjwa ya ngono.
Unaweza kupendelea: njia za vizuizi, vidonge vya majira, njia za asili

Unaweza kuepuka: Vijiti, sindano za majira, kitanzi, kufunga uzazi kabisa
Unaweza kupendelea: Kondom za kiume au kike

Unaweza kuepuka: Kufanya ngono bila kondom
HAW Ch7 Page 194-1.png
Nanyonyesha mtoto wangu. Sitaki kuzaa mtoto mwingine hadi angalau baada ya miaka 2.
Mwenzangu hataki kuhusishwa na matumizi ya njia yoyote ya uzazi wa mpango.
Unaweza kupendelea: kondom ya kiume au kike, vizuizi (diaphragm), njia ya vijiti, kitanzi, kidonge kidogo cha majira, sindano ya majira yenye homoni ya projestini tu

Unaweza kuepuka: Vidonge mseto vya majira, sindano za majira kila mwezi hadi mtoto atakapofikisha miezi 6 au hedhi yako ya kila mwezi kurudi kama kawaida
Unaweza kupendelea: Kondom ya kike, kizuizi (diaphragm), njia za homoni, kitanzi

Unaweza kuepuka: : Kondom za kiume, njia za asili

Njia za kuzuia mimba katika dharura

Mwanamke anaweza kutumia njia za dharura za kuzuia mimba baada ya kufanya ngono bila kutumia njia yoyote ya kuzuia mimba, au kama hakuitumia njia husika kwa usahihi. Kwa mfano, njia za dharura zinaweza kutumika kama ikigundulika kuwa kondom ina tobo au imeathirika kwa namna yoyote ile. Au kama kondom ilichanika wakati wa tendo la ngono; au kama mwanamke alisahau kutumia kidonge cha majira kwa zaidi ya siku 1.

Njia nyigine ya kuzuia mimba wakati dharura (Plan B) ni kutumia dozi kubwa ya vidonge vya majira vyenye homoni zile zile, mara moja, ndani ya siku baada ya kufanya tendo husika la ngono. Inawezekana pia kutumia aina Fulani za vidonge vya majira kama mbadala wa plan B. Njia nyingine ya dharura ni kitanzi kuingizwa na mfanyakazi wa afya ambaye amepitia mafunzo maalum ndani ya siku 5 baada ya tendo la ngono husika. Wanawake wote wanapaswa kufahamu njia za kuzuia mimba wakati wa dharura na kuweza kuzitumia kama wanatakiwa kufanya hivyo.

Wanawake wengi hasa wasichana hushinikizwa au kulazimishwa kufanya ngono bila kuafiki au bila mpango. Njia za dharura pia zinaweza kusaidia kuzuia mimba baada ya kubakwa. Bahati mbaya, taarifa juu ya njia za dharura za kuzuia mimba hazipatikani katika maeneo mengi. Kama taarifa juu ya njia hizi za dharura hazipatikani katika jamii yako, ongea na wafanyakazi wa afya, walimu, na viongozi wa jamii na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo wanajishughulisha na kusaidia kuzuia mimba zisizotarajiwa, hasa miongoni mwa vijana.

Kwa taarifa zaidi juu ya njia za kuzuia mimba wakati wa dharura, angalia Vyanzo vingine (Other Resouces) na Sura ya 13: Uzazi wa Mpango katika kitabu Mahali Wanawake Wanapokuwa Bila Daktari (kinaandaliwa)).

Mwanamke akiongea
Tuliandaa mpangokazi kuhakikisha kuwa wanawake wote kwenye jamii na wafanyakazi wa afya ambao wanaweza kutoa huduma kwa wanawake baada ya kubakwa, wanajua jinsi ya kutumia kwa usalama vidonge vya kawaida vya majira kwa ajili ya kuzuia mimba wakati wa dharura.

Ukweli na maneno ya mitaani au fikra zisizo na uhakika juu ya uzazi wa mpango

Fikra zisizo na uhakika, majungu, au taarifa potofu juu ya baadhi njia tofauti za kuzuia mimba vinaweza kuwafanya watu kuogopa kuzijaribu, hata kama wangetaka kufanya hivyo. Watu wanahitaji taarifa sahihi ili waweze kuchagua njia mojawapo na kuitumia kwa kuiamini. Unaweza kutumia mifano kama iliyopo hapa ya kutengeneza maigizo, au michezo ambayo inaweza kuwasaidia kutenganisha ukweli na uongo ambao husikia kila.

Maneno ya mitaani: Baadhi ya watu husema kuwa vidonge vya majira husababisha wanawake kuugua.
Ukweli: Wanawake wengi kamwe hawajisikii kuugua kutokana na vidonge vya majira, lakini baadhi huumwa na kichwa au kujihisi hovyo hovyo wanapoanza kutumia vidonge hivi. Hali hii kawaida hutoweka baada ya kutumia vidonge hivi kwa miezi 2. Mwanamke anaweza kubadilisha na kuanza kutumia aina nyingine ya vidonge ambayo havimsababishii hali yoyote ya kutojisikia vizuri.
Maneno ya mitaani: Baadhi ya watu husema kuwa njia za uzazi wa mpango huwapunguzia wanawake uwezo wa kuzaa au kutozaa kabisa pale wanapoacha kuzitumia.

Ukweli: Njia pekee ya uzazi wa mpango ambayo huwazuia wanawake kutokuwa na uwezo wa kuzaa kabisa ni upasuaji ambao huhusisha kufunga mirija ya uzazi au kuondoa kizazi. Wanawake wengi wanaweza kupata mimba mara moja baada ya kusimamisha matumizi ya njia yoyote ile ya uzazi wa mpango. Baadhi ya wanawake wanaweza kutokuwa na uwezo wa kubeba mimba kwa miezi michache baada ya kusimamisha matumizi ya njia ya uzazi wa mpango ya homoni.

Maneno ya mitaani: Baadhi ya watu husema wanawake hawawezi kupata mimba wakati wa siku zao za hedhi.

Ukweli: Wanawake wanaweza kupata mimba wakati wote katika mzunguko wao wa hedhi, hasa kama hedhi haipatikani tarehe zile zile kila siku 28.

Maneno ya mitaani: Baadhi ya watu husema kusuuza uke, kuoga maji ya moto mara baada ya ngono au kufanya ngono mkiwa mmesimama husaidia kuzuia mimba.

Ukweli: Hakuna jambo lolote kati ya hayo juu ambalo linaweza kuzuia mimba.
Maneno ya mitaani: Baadhi ya watu husema upasuaji wa vasektomi humdhoofisha mwanaume kingono na kumfanya asimridhishe mwenzi wake katika tendo la ngono.
Ukweli: Vasektomi huzuia tu mwanaume kuachia mbegu za kiume. Vasektomi haiathiri hisia zake au uwezo wake wa kufanya ngono.

Njia nyepesi nyepesi za kupashana taarifa juu ya uzazi wa mpango

Mjadala katika kikundi juu ya njia za kuzuia mimba unaweza kumsaidia kila mtu kuelewa njia zipi ambazo zinaweza kuwafaa wanawake katika mazingira tofauti. Wakati mwingine, kujadili tu njia tofauti katika makundi ambayo yanajumuisha vijana, wazee, au mamamkwe husaidia kuondokana na vikwazo dhidi ya matumizi ya uzazi wa mpango.

wanawake 2 wakiongea..
Basi, kama mwanamke ana uhakika kwamba hataki kuzaa tena, si anaweza kutumia njia ya kitanzi? Kitanzi hudumu muda mrefu. Au anaweza kufanyiwa upasuaji-kufunga uzazi kabisa.
Nimesikia ni rahisi zaidi mwanaume kufanyiwa upasuaji wa kufunga uzazi.

Kuonesha matumizi ya njia tofauti

kikundi cha wanawake kikichunguza baadhi ya vifaa vya kuzuia mimba vilivyopo mezani.

Njia moja wapo ya kujifunza juu ya uzazi wa mpango ni kualika mfanyakazi wa afya kuonesha matumizi ya njia tofauti zilizopo kwenye jamii yako. Kila mtu anaweza kukamata na kuchunguza vifaa hivyo tofauti na jinsi vinavyofanya kazi. Mfanyakazi wa afya anaweza kuelezea jinsi kila njia inavyozuia mimba na pia kujibu maswali kutoka kwa washiriki. Mfanyakazi wa afya pia anaweza kuwaomba washiriki kufikiria njia za uzazi wa mpango ambazo zinaweza kufaa mazingira husika.

Kwa taarifa za kuaminika juu ya njia za uzazi wa mpango, angalia Vyanzo vingine (Other Resources) na Sura ya 13 Uzazi wa Mpango (kinaandaliwa) katika kitabu Mahali Wanawake Wanapokuwa Bila Daktari (kinaandaliwa).

Michezo ya bao (Board games) juu ya uzazi wa mpangos

Mchezo wa bao unaweza kuwa njia changamfu ya kujadili njia za uzazi wa mpango na sababu kwa nini wanawake wanaweza kupendelea njia tofauti. Mjadala hufanyika wakati wa mchezo wa bao na kukisaidia kikundi:

  • kupima ufahamu wao juu ya njia tofauti za uzazi wa mpango.
  • kuchunguza sababu za wanawake kupendelea njia tofauti.
  • kufanya mazoezi ya utoaji wa ushauri kwa wanawake juu ya njia za uzazi wa mpango mbalimbali.
  • kuchunguza mambo gani zaidi juu ya uzazi wa mpango ambayo wanawake wangependa kujifunza.

Zoezi Mchezo wa bao juu ya uzazi wa mpango

Maandalizi:
Mfano wa mchezo wa bao (pichani chini)unaonesha aina ya maswali kuhusu ukweli juu ya uzazi wa mpango na maswali mengine ya kuendesha majadiliano. Kama unatengeneza maswali yako binafsi juu ya ukweli kuhusu uzazi wa mpango, hakikisha unajumuisha pia fikra za kawaida (maneno ya mitaani) na utata ambao kawaida hujitokeza katika jamii yako (kwa taarifa zaidi angalia Ukweli na fikra zisizo sahihi juu ya uzazi wa mpango.

wanawake 2 wakiongea wakati wa mchezo wa bao.
Je, kama Zahoro hataki kusubiri hadi Hadija amalize shule ndiyo wapate mtoto?
Katika hali kama hiyo, dada yangu alitumia uzazi wa mpango bila hata kumwambia mume wake ! Hadija anaweza kutumia sindano za majira au njia ya vijiti na hakuna atakayejua.

Jinsi ya kucheza:

Pale kete ya timu au mchezaji inapoangukia sehemu ya swali la majadiliano (lenye alama "?"), waombe kupendekeza kwa washiriki wote ufumbuzi 1 au 2 kuhusu tatizo ambalo limeoneshwa kwenye kadi, na baada ya hapo kuelezea kwa nini ufumbuzi mmoja unaweza kuwa bora kuliko mapendekezo mengine. Waalike washiriki wengine kutoa maoni yao pia. Kete la kikundi linapoangukia sehemu ya swali juu ya ukweli kuhusu uzazi wa mpango (lenye alama "✓"), wawezeshe kujibu maswali na kuwauliza wengine kama wanaafiki majibu hayo.

Baada ya kucheza mchezo wa bao juu ya uzazi wa mpango, waalike washiriki kuzungumzia mambo muhimu waliyojifunza kutokana na zoezi hilo. Uliza kama kuna maswali mengine yanayohusiana na uzazi wa mpango ambayo kikundi kingependa kujadili au kujifunza zaidi. Tumia majibu yao katika kupanga mazoezi au shughuli zingine za kujifunza.

Maswali kwa ajili ya mchezo wa bao juu ya uzazi wa mpango

Maswali juu ya ukweli kuhusu afya yanaweza kusaidia kikundi kujifunza mambo ya msingi juu ya njia tofauti za kuzuia mimba. (Majibu yameoneshwa hapa, lakini usiyaweke kwenye kadi zako. Badala yake, yaandike kwenye karatasi tofauti kukusaidia kukumbuka.)
rundo la kadi za ukweli juu ya afya, zikiwa na alama ya "✓" nyuma ya kila kadi.
Rundo la kadi za mjadala, zikiwa na alama ya"?" nyuma ya kila kadi.
Mfano wa mchezo wa bao juu ya uzazi wa mpango.
Ongeza maoni kama vile, "Mimba zisizotakiwa, rudi nyuma vyumba 4 "au" Uliongea na mwenzi juu ya kondom, nenda mbele vyumba 2."
mfano wa maswali juu ya ukweli kuhusu afya.
Ni zipi kati njia za uzazi wa mpango zifuatazo ambazo hufanya kazi vizuri zaidi kuzuia mimba?

Mwanaume kuchomoa ume anapokaribia kileleni au kondom?


(Njia sahihi: Kondom)
HAW Ch5 Page 124-2.png
Mwanamke hawezi kupata mimba kama atafanya ngono akiwa katika siku zake za hedhi.

Ni kweli au siyo kweli?


(jibu sahihi: Siyo kweli)
HAW Ch5 Page 124-2.png
Vasektomi (upasuaji wa kufunga uzazi kwa wanaume) huondoa hamu au uwezo wa wanaume kufanya ngono?

Kweli au siyo kweli?


(jibu sahihi: Siyo sahihi)
mifano ya maswali ya kuchochea majadiliano.
Naomi alikuwa akitumia vidonge vya majira. Lakini ghafla kliniki yake iliishiwa vidonge hivyo vya majira. Mfanyakazi wa afya alimuambia kuwa kuanzia sasa kliniki hiyo itakuwa inatoa kondom tu kwa sababu shirika la misaada ambalo linawasaidia halitoi njia nyingine ya uzazi wa mpango. Naomi anajua kuwa wanaume kijijini kwake hawataki kutumia kondom. Anataka kulitafutia ufumbuzi tatizo hili lakini hajui pa kuanzia.

Unafikiri Naomi afanye nini? Kwa nini?
HAW Ch5 Page 125-2.png
Mariamu anampenda sana mpenzi wake Baraka. Uhusiano wao una zaidi ya mwaka mmoja na hivi karibuni waliamua kufanya ngono kwa mara ya kwanza. Njia ya kuzuia mimba walioitumia ni Baraka ‘kuchomoa ume ili kutomwaga shahawa ndani’. Baadaye, Mariamu alijaribu kumuuliza Baraka juu ya njia za kuzuia mimba ambazo wanaweza kutumia siku za usoni. Lakini Baraka alimuambia kuwa ni wajibu wa mwanamke kutumia njia za kuzuia mimba, na siyo wa mwanaume.

Unafikiri Mariamu anaweza kufanya nini? Kwa nini?
HAW Ch5 Page 125-2.png
Adamu na Chiku walioana hivi karibuni. Kabla ya kuoana, Adamu alikuwa amefanya ngono na wanawake wengi tofauti. Chiku anafikiria bado anaendelea kufanya ngono na makahaba anapokwenda kustarehe na rafiki zake. Chiku amekuwa akisisitiza kutumia kondom na Adamu ili kujilinda dhidi ya maambukizi kupitia ngono na mimba. Lakini sasa anataka kupata mtoto na Adamu.

Unafikiri Chiku afanye nini kwani sasa anataka kupata mtoto? Kwa nini?

Maswali ya kuchochea majadiliano yaelezee mifano halisi katika maisha na kuangalia baadhi ya sababu kwa nini wanawake wanaweza kupendelea njia tofauti za uzazi wa mpango. Hakuna majibu sahihi au yasiyo sahihi kwa maswali hayo. Lengo ni kujadili hali husika kama kikundi.