Hesperian Health Guides

Kuanzisha mazungumzo juu ya uzazi wa mpango

Katika sura hii:

Watu mara nyingi huona haya au fedheha kuzungumzia masuala ya uzazi wa mpango kwa sababu uzazi wa mpango unahusisha pia kuongelea suala la ngono. Njia bora ya kuanza mazungumzo haya ni kutanguliza jinsi gani uzazi wa mpango unavyoweza kunufaisha afya ya wamama na watoto, na manufaa yake kwa familia nzima.

Zoezi Tumia michoro au picha kuzungumzia manufaa ya uzazi wa mpango

vikaroti vidogo ambavyo vimepandwa kwa msongamano na kulia (2) karoti kubwa zilizopandwa kwa kuacha nafasi katikati.
Kupanda mimea kwa kuacha nafasi katikati ili isisongamane ni bora kwa udongo na husaidia mimea yenyewe kukua vizuri ikiwa yenye afya. Hali hiyo pia inawahusu wamama na watoto. Kuzaa kwa kuacha nafasi ya kutosha kati ya mtoto mmoja na mwingine ni bora zaidi kiafya kwa familia nzima.
Mwanaume na mwanamke wakiwa wamekumbatiana.
watu wazima wane wakiwa darasani.
Mwanamke na mwenzi wake wanaweza kufurahia tendo la ngono bila woga wa kupata mimba. Kutowahi sana kuzaa huwasaidia vijana kupata muda wa kusoma.
familia ya watu 5 kwenye mzani ikilinganisha na uzito wa chakula inachohitaji
familia ya watu 4 wakisoma na kucheza pamoja.
Idadi ndogo ya watoto humaanisha lishe zaidi kwa kila mwanafamilia. Wazazi huwa na muda zaidi wa kustarehe na kusaidia kusomesha watoto wao.
  1. Onesha kikundi picha hizi bila maelezo yake (unaweza kuzirekebisha ili ziendane na mazingira). Waombe wanakikundi kujadili manufaa gani ya kiafya au manufaa mengine ya uzazi wa mpango ambayo yanaoneshwa na picha hiyo.
  2. Tumia mawazo ya kikundi kuuliza maswali kadhaa, kama vile:
    • Ni tofauti gani ambazo uzazi wa mpango huchangia kwa mwanamke ambaye amesoma? Kwa mwanamke ambaye ana kazi na anatunza nyumba yake na familia?
    • Ni tofauti gani ambazo uzazi wa mpango unaweza kuleta kwa familia ambayo huhangaika sana kupata chakula cha kutosha? au ambayo huishi sehemu ndogo iliyobanana na ambayo haiwezi kumudu gharama za kuhama?
    • Ni tofauti gani ambazo uzazi wa mpango unaweza kuchangia katika kupata makazi bora, maji safi na salama, usafi wa mazingira hususan choo, na shule kwa ajili ya kila mtu kwenye jamii?
  3. Waulize washiriki kuchora picha zao wenyewe juu ya manufaa mengine ya uzazi wa mpango. Wawezeshe kufikiria jinsi gani uzazi wa mpango unavyoweza kuleta tofauti zaidi katika maisha ya mwanamke, familia yake, na jamii nzima.

Kuwahusisha wanaume

mwanaume akiongea na wenzake 2 wakiwa wananukuu mambo muhimu.
Asante kwa taarifa hii juu ya kliniki mpya ya huduma za uzazi wa mpango. Nitaongea na mke wangu juu ya huduma hii.

Karibia wanaume wote wanataka kuwa na wenzi na watoto wenye afya bora, lakini baadhi yao hawazungumzii uzazi wa mpango kwa sababu hawana uelewa wa kutosha juu ya huduma hiyo, au wanaweza kuwa waliwahi kusikia mambo mengi mabaya juu ya huduma hii. Kuzungumzia uzazi wa mpango huwasaidia wanaume kuheshimu maamuzi ya wanawake juu ya idadi ya watoto wangependa kuzaa na pia kushiriki katika matumizi ya njia zauzazi wa mpango na wenzi wao. Kuzungumzia suala hili kunaweza kuwasaidia wanaume na wenzi wao kuelezea jinsi wanavyoweza kufurahia tendo la ngono bila wasiwasi wa mimba kutokea.

Zoezi lifuatalo ni igizo la kuonesha familia 2 tofauti na jinsi gani zinavyoendelea. Hili ni zoezi la kuchekesha ambalo ni zuri kwa ajili ya kuwavutia wanaume katika mazungumo juu ya uzazi wa mpango.

Zoezi Mchezo wa hadithi: Hadithi za familia 2

  1. Chora michoro 2 inayolingana chini kwenye udongo wenye eneo ambalo linatosha watu 4 kusimama ndani yake. Wambie wanakikundi kuichukulia michoro hii kuwa nyumba za wanandugu 2.
  2. Waambie wanakikundi wajitolee kuigiza kama wanandoa 4, na kuwapa majina. Katika igizo hili, wenzi wa kwanza ni Adamu na Sara, na wenzi wa pili ni Musa na Rehema. Waombe kila wenzi 2 kusimama kwenye ‘nyumba’ hizo-kila wenzi katika nyumba yao. Eleza kwamba wanaume hao ambao ni mtu na kaka yake walioa siku moja. Piga mziki na kuwaomba wenzi hao kucheza kusherekhea ndoa zao!
    Familia 2 zikicheza mziki ndani ya ‘nyumba’ zao.
    Adam na Sara
    Musa na Rehema
  3. Sasa,elezea hadhithi ya jinsi kila familia inavyoendelea. Watu wengine wajitolee kuigiza kama watoto wa familia hizo, kwa mfano:
    Kila familia ilipata mtoto baada ya mwaka wa kwanza wa ndoa yao, na watoto wote ni wa kike. (Waombe watu 2 kujitolea kuigiza nafasi za watoto hao na kusimama ndani ya nyumba. Unaweza kuwapa midoli kudhihirisha nafasi yao ya utoto)


    Adamu na Sara walisha kuzungumzia juu ya suala la kupata watoto zaidi na kuamua kusubiri kwa muda. Walikwenda katika kiliniki ya kijiji kuulizia juu ya huduma za uzazi wa mpango. Mfanyakazi wa afya aliwaeleza juu ya njia mbalimbali za uzazi wa mpango ambazo zinatolewa, na aliyapatia majibu maswali yao juu ya njia zingine kama vile kuhesabu siku (fertility awareness). Adam na Sara waliamua kupata sindano ya majira kila baada ya miezi 3 ili kuzuia mimba. Sara alikwenda kufanya kazi kwa muda na kumkabidhi mama yake mzazi uangalizi wa mtoto.

    Rehema na Musa waliamua kutotumia njia yoyote ya uzazi wa mpango baada ya mtoto wao wa kwanza kuzaliwa. Waliamini kwamba kupata watoto ni majaliwa ya Mungu, na Musa ana shauku ya kupata mtoto wa kiume hivi karibuni. Wote wanataka Rehema kumtunza mtoto wao muda wote, na hivyo hana nafasi ya kuajiriwa wala kufanya biashara. Baada ya mwaka mmoja Rehema na Musa wanapata mtoto mwingine, wa kike. (Muombe mshiriki mwingine ajitolee kuigiza nafasi hiyo ya mtoto wa pili na kuingia kwenye nyumba ya Rehema na Musa.)

    Rehema na Musa wanapata mtoto mwingine wa 3 mwaka unaofuata, na mara hii ni mtoto wa kiume. (Muombe mshiriki mwingine kuingia kwenye nyumba ya Rehema na Musa na kuigiza nafasi ya mtoto wa 3.)

    Akiwa na watoto 3 wenye umri chini ya miaka 3, Rehema hataki watoto zaidi, lakini anaogopa kulizungumzia suala hili na Mumewe. Katika mwaka wao wa 5 wa ndoa, wanapata mtoto wa 4. (Muombe mshiriki kujitolea kungia nyumba ya Rehema na Musa na kuigiza nafasi ya mtoto wa 4.)

    Adam na Sara waliamua kupata mtoto mwingine pale mtoto wao wa kwanza alipofikisha miaka 3. (Mwombe mshiriki mwingine kujitolea na kuingia nyumba ya Adam na Sara na kuigiza nafasi ya mtoto wao wa pili.)

    Katika mwaka wao wa 6 wa ndoa, Rehema na Musa walipata mtoto mwingine. (Mwombe mshiriki mwingine kujitolea na kuingia nyumba ya Rehema na Musa na kuigiza nafasi ya mtoto wa 5.)

    Katika maadhimisho ya miaka 6 ya ndoa zao, familia hizo 2 zilipanga kufanya tafrija ya pamoja na kuandaa chakula. (Unaweza kutoa mkate mmoja kwa kila familia na kuwaomba wagawane.)
    familia 2, ya kwanza ikiwa na watoto 2 na nyingine na watoto 5.
  4. Mara baada ya igizo hilo kukamilika, unaweza kuanzisha mjadala wa kikundi juu ya mawazo ya jamii juu ya uzazi wa mpango, au juu ya ukubwa wa familia na mambo gani ambayo yanachangia maamuzi ya watu juu ya masuala haya. Yafuatayo ni baadhi ya maswali ambayo unaweza kuuliza:
    • Kwa nini baadhi ya watu hupendelea familia kubwa na wengine kuwa na watoto 2 au hata 1?
    • Nani huamua lini familia ipate mtoto na watoto wangapi? Maamuzi haya huwaathiri wanawake namna gani? Huwaathiri wanaume namna gani?
    • Watu wana mtazamo gani juu ya kupata watoto wa kiume au wa kike? Mitazamo ya watu huchangia namna gani maamuzi yao juu ya kupata watoto?
    • Ukubwa wa familia huathiri namna gani uwezo wa familia wa kupata chakula cha kutosha na kuhakikisha watoto wote kwenye familia wanakuwa wakiwa na afya bora?
  5. Katika kuhitimisha, unaweza kuwaomba wanakikundi mawazo yao kuhusu jinsi uzazi wa mpango unavyowezesha wanawake na wanandoa kuamua lini wapate mtoto na watoto wa ngapi.

Wanandoa/wenzi wanastahili kuzungumzia uzazi wa mpango

Kuongea na mwenzi juu ya matumizi ya njia za kudhibiti uzazi huwa ni rahisi zaidi pale wanawake wanapofanya mazoezi mapema na kuigiza jinsi ya kulizungumzia suala hilo. Wanawake wanapoigiza nafasi za wanaume hulifanya zoezi kuchekesha zaidi.

Zoezi Jizoeshe kuzungumzia juu ya kudhibiti uzazi

  1. Kwanza, waombe washiriki kufikiria sababu mbalimbali ambazo zinaweza kuwafanya wanaume kutotaka kuzungumzia suala la kudhibiti uzazi, au wanaweza kutoa sababu gani za kutotumia njia za uzazi wa mpango.
  2. Baada ya hapo, waombe wanawake wawili wawili kuigiza, mmoja kama mwanamke na mwingine kama mwanaume; mwanamke akizungumzia nia yake ya kutumia njia za uzazi wa mpango na kujaribu kumshawishi mume wake atoe ushirikiano.
    wanawake 2 wakiigiza, mmoja akiigiza nafasi ya mwanaume
    Heshima ya mwanaume huongezeka sambamba na kuongezeka kwa idadi ya watoto wake!
    Ndio, lakini idadi ndogo ya watoto humaanisha kwamba angalau kila mtoto atapata chakula cha kutosha.
  3. Baada ya kila igizo, waulize wanawake walioshuhudia majadiliano ni hoja gani zilizotolewa ambazo ni muhimu zaidi. Ni hoja gani zingine ambazo wanafikiria zinaweza kusaidia kuwashawishi wanaume? Kuna mifano kadhaa:
    • Ngono inakuwa bora zaidi kama mwanamke anakuwa hana wasiwasi wa kupata mimba.
    • Tukivuta subira kabla ya kupata mtoto mwingine, nitapata nafasi na muda wa kuchangia zaidi familia yangu.
    • Nikipata ujauzito sasa, itabidi uache chuo na kuhangaika kutafuta namna ya kuihudumia familia.
    • Siyo lazima uwe na watoto wengi ndio upate heshima- fikiria raha utakayokuwa nayo watoto wako watakapofanikiwa kimaisha kwa sababu uliweza kuwagharimia kupata elimu nzuri.
    • Kuzaa kila mwaka kutanifanya nizeeke kabla ya wakati wangu na nitashindwa kuwalea vizuri watoto hao. Je, si bora zaidi nikabaki na nguvu na afya?

Kikundi cha wanawake chachangia mabadiliko ya mtazamo miongoni mwa wanaume nchini Nepali

Wanawake nchini Nepali walianzisha mtandao wa vikundi vya kijamii vya uanaharakati mahali walipokutana kujadili juu ya afya yao na kutafuta ufumbuzi kwa matatizo ya kijamii. Walisaidiana kuboresha stadi zao za kusoma na kuandika, na kuanzisha mifuko ya kuweka na kukopa ili wanawake waweze kupata mikopo pale familia zao zinapokuwa na mahitaji ya kifedha kwa ajili ya matibabu na dharura zingine. Wanaume waliunga mkono vikundi hivyo baada ya kutambua kuwa kumsaidia mwanamke hunufaisha familia nzima.

Wanawake pia walianza kujifunza juu ya uzazi wa mpango, na baada ya muda mfupi baadhi ya wanaume walianza kuzungumzia manufaa ya kuzaa kwa kuacha nafasi ya kutosha kila baada ya mtoto na wanaume wenzao kwenye mikusanyiko mbalimbali kama vile kwenye migahawa, baraza, na vituo vya mabasi. Kadri habari juu ya matumizi ya kondom na uzazi wa mpango zilivyozidi kuenea, suala la wanawake na waume zao kupanga familia zao lilizidi kuwa jambo la kawaida na kukubalika.

wanawake 2 wakiongea.
Kabla ya hapo ilibidi mwanamke kuomba ruhusa kufanya hata jambo dogo sana kama kuuza kuku.
Lakini sasa tunaweza kufanya maamuzi juu ya mambo yanayotuhusu na familia zetu, kama vile tuzae watoto wangapi na iwapo wanapaswa kwenda shule.

Mahitaji ya vijana balehe katika kudhibiti mimba

Vijana balehe hukabiliwa na changamoto nyingi wanapotaka kujinda dhidi ya mimba zisizotakiwa. Vijana wa kike mara nyingi hushinikizwa kufanya ngono au kuzaa kabla hawajakua vizuri. Baadhi ya vijana wa kike hujihisi kuwa tayari kufanya tendo la ngono lakini siyo kuwa wamama. Vijana balehe mara nyingi hawapati huduma za kuzuia mimba wanapokuwa wanazihitaji. Na huwa ni vigumu zaidi vijana wa kike kuwahimiza wenzi wao wa kiume kutumia kondom. Vilevile, wazazi wengi huwa hawajisikii huru kuongea na watoto wao wa kike juu ya suala la ngono, mimba, na kudhibiti uzazi.

Imani za kidini na kitamaduni ambazo hukataza vijana wa kike kufanya ngono kabla ya ndoa pia huwa ni changamoto kwa vijana balehe kujifunza jinsi ya kuzuia mimba. Imedhihirika kuwa kuongea moja kwa moja na vijana juu ya uzazi wa mpango siyo kichochezi cha vijana kufanya ngono kabla hawajawa tayari. Badala yake, mazungumzo kama hayo yanaweza kusaidia kujenga hali ya kuaminiana na maelewano. Ufahamu juu ya uzazi wa mpango huwawezesha vijana wa kike kujiamini zaidi katika mahusiano yao na kudhibiti maisha yao wenyewe. Kwa ajili ya taarifa zaidi, angalia Sura 4 Ujinsia na Afya ya Ujinsia (kinaandaliwa).

Mazungumzo kati ya vijana na wazazi, walezi au watu wazima wenye ufahamu wa kutosha yanaweza kusaidia upatikanaji wa ufumbuzi wa kijamii wa kuzuia mimba za utotoni na mimba zingine zisizotarajiwa.

Zoezi Mjadala huru wa kuwasaidia vijana na watu wazima kujadili juu ya kudhibiti uzazi

kundi la vijana likiwa limekaa kwenye jamvi na watu wazima wakiwa wamekaa kwenye viti wakiwazunguka.
Mjadala huru wenye uwazi wa kutosha unaweza kuwa njia nzuri kwa vijana na watu wazima kusikiliza masuala muhimu na maoni ya kila upande.

Unaweza kuboresha zoezi la mjadala huru juu ya uzoefu wa washiriki kuhusiana na uzazi wa mpango (A fishbowl about birth experiences) (kinaandaliwa) ili zoezi liweze kuendana na mazingira yako. Mkao huo huchukua sura ya bakuli (fishbowl). Kwa mfano, anza kwa kuwezesha kundi la vijana wa kike, au kundi mchanganyiko la vijana wa kike na kiume, kukaa pamoja katika mduara na watu wazima wakiwa wameketi wakiwazunguka.

  1. Waombe vijana kwenye mduara wa ndani kujadili kwa nini upatikanaji wa huduma za kudhibiti mimba ni muhimu kwa afya ya vijana wa kike sasa na katika maisha ya baadaye. Washawishi kujadili uzoefu wao (au uzoefu wa vijana wengine) na matatizo yoyote katika kupata huduma hizi na kuzitumia.
  2. Baada ya hapo waombe washiriki watu wazima kujadili maoni waliyoyasikia. Wape fursa ya kuwauliza vijana maswali na vijana kujibu.
  3. Baada ya dakika chache, makundi hayo 2 yabadilishane mkao. Watu wazima waelezee uzoefu wao na matatizo yoyote katika kutumia huduma za uzazi wa mpango.
  4. Waombe vijana kujadili yale muhimu waliyoyasikia na wape nafasi ya kuwauliza washiriki watu wazima maswali.
  5. Katika kuhitimisha, uliza kila kikundi maswali ambayo yatawasaidia kutafakari uzoefu wa washiriki wengine. Wamejifunza nini ambacho walikuwa hawajui kabla ya zoezi? Ni mambo gani katika uzoefu na maoni ya washiriki ambayo yanafanana? Kuna tofauti zipi miongoni mwa uzoefu au maoni ya washiriki juu ya upatikanaji na matumizi ya huduma za uzazi wa mpango?

Kuhimiza huduma rafiki kwa vijana

Njia mojawapo ya kuhakikisha huduma za afya rafiki kwa vijanani kuongeza fursa kwa vijana wa kike na kiume kupata habari juu ya njia za kudhibiti uzazi, afya ya ujinsia na kuzuia maambukizi kupitia ngono.

Vijana wakiwa karibu na bango ambalo linasomeka, "Kliniki ya Vijana, saa 5 hadi 9 za jioni." na bango lingine lenye tangazo juu ya tamasha la kiafya
Kuna uwezekano mkubwa zaidi wa vijana kutumia huduma za uzazi wa mpango ambazo zimetoa kipaumbele kwa maslahi na mahitaji yao, zikitolewa katika maeneo yanayowafaa, na katika muda unaowafaa.

Kwa mfano, unaweza:

  • Kuanzisha huduma katika sehemu ambazo tayari vijana wamezizoea zikiwemo shule na vituo vya vijana.
  • Kutenga muda maalum kwa ajili ya ‘vijana pekee’katika kiliniki za kawaida hasa wakati wa saa za mchana, jioni au siku za mapumziko ya mwisho wa wiki.
  • Kuwahakikishia vijana kwamba wafanyakazi wa afya watawahudumia kwa heshima na faragha -hawatatoa nje taarifa zao za binafsi.
  • Kuwafundisha vijana kuwa washauri-rika
  • Kuwaomba vijana kupamba maeneo ya kutolea huduma hiyo, kutoa huduma ya muziki wakati wa saa za huduma ya ‘Vijana Pekee’, na kuwafanya kujisikia sehemu hiyo kuwa yao.
  • Kuhakikisha huduma zote zikiwemo za uzazi wa mpango zinatolewa bila malipo au kwa gharama nafuu kadri inavyowezekana.


Hamashisha vijana kushiriki na kuongoza shughuli muhimu kwenye kituo. Kwa mfano, kikundi cha vijana kinaweza kuandaa disko au zoezi la kusafisha mazingira ya eneo linalozunguka kituo na kuwashirikisha wanajamii. Shughuli hiyo inaweza kuambatana na utoaji wa huduma za afya zikiwemo uzazi wa mpango. Vijana wana mawazo makubwa na juhudi kubwa. Wanaweza kuibua mawazo yenye uwezo wa kuwashtua watu wazima au kuwafanya wasijisikii vizuri, lakini mwishowe watawafikia vijana wenzao wengi zaidi. Kuna mawazo zaidi juu ya huduma rafiki kwa vijana kwenye Sura ya 4: Ujinsia na Afya ya Ujinsia (kinaandaliwa) na Sura ya 5: Kudhibiti Maambukizi Kupitia Ngono (kinaandaliwa).

Shughuli zifuatazo zinaweza kusaidia kuchochea mijadala kati ya vijana na watu wazima juu ya mahitaji ya vijana na vikwazo katika kupata huduma, na baada ya hapo kufikiria mabadiliko ambayo yanahitajika katika huduma za afya ili ziweze kukidhi mahitaji ya vijana wote.

Zoezi Kuvuka mto kupata huduma za afya

  1. Tengeneza mto wa kufikirika katikati ya eneo mlipojikusanya kwa kutumia mawe, kamba, au kipande kirefu cha kitambaa. Waombe vijana kukaa upande mmoja na watu wazima kukaa upande mwingine. Waulize wote kwa nini vijana balehe wanahitaji huduma kamilifu za afya ya uzazi, zikiwemo huduma za kuzuia mimba na utoaji mimba salama, na pia elimu na ushauri juu ya ujinsia, na kwa nini mto unawatenganisha watu wazima na vijana.
    Vijana 2 na watu wazima 2 wakiongea katika pande 2 tofauti za mto wa kufikirika.
    Tayari sisi ni vijana lakini ni kama wanawake wengine, isipokuwa hatutaki kupata mimba. Tunataka kujua jinsi ya kujitunza na kujilinda kama wanawake.
    Tunahitaji kuongea na watu wazima ambao watatusikiliza maoni na changamoto zetu na siyo kutuhukumu. Tunahitaji taarifa na majibu ya moja kwa moja kwa maswali yetu.
    Hatuna aliyetuambia kuongea na hao vijana juu ya masuala haya. Pia sina uhakika kama inaruhusiwa kisheria.
    Kuna hatari nyingi siku hizi, sijui mahali pa kuanzia katika kuongea na wanangu.
  2. Eleza bayana kuwa upatikanaji wa huduma za afya unaweza kuokoa maisha ya wanawake, lakini wakati mwingine kupata huduma za afya ni sawa na kuvuka mto mkubwa uliojaa maji ambayo yanakimbia kwa kasi. Wakati mwingine watu wazima wanahitaji kuwarushia kamba vijana walio upande wa pili ili kuwasaidia kuvuka.
    Waombe wanakikundi kufikiria juu ya vikwazo na sababu kwa nini vijana balehe hawawezi au huamua kutotembelea vituo vya afya kupata huduma za afya ya uzazi kama vile nyenzo za kudhibiti uzazi, kondom, au kupata huduma ya upimaji wa maambukizi kupitia ngono. Kwa ajili ya kila kikwazo, uliza "Kwa nini?" ili kuwachochea washiriki kufikiria vikwazo vingine.
    Kadi zilizoandikwa vikwazo.
    Hakuna huduma baada ya saa za shule
    Inahitaji ruhusa ya wazazi
    Hakuna faragha
    Hakuna huduma bila malipo ya upimaji wa maambukizi kupitia ngono
    Vijana hawajui kuwa wana haki kuhusu afya ya uzazi
  3. Baada ya vikwazo vyote kuandikwa kwenye kadi, unda vikundi 2 na toa nusu ya kadi hizo kwa kila kikundi. Mara hii vikundi vinatakiwa kuwa mchanganyiko-vikijumuisha vijana na watu wazima, na kukaa pande mbili tofauti za mto wa kufikirika.
  4. washiriki wameunganishwa na kamba pande zote mbili za mto wa kufikirika.
  5. Waombe washiriki kusoma kwa sauti kubwa kikwazo kilichoandikwa kwenye kadi moja wapo kwa ajili ya kundi la ngambo ya pili. Kundi la ngambo ya pili linapaswa kutafuta jibu au “kamba ya kusaidia kuvuka mto”. Watakapopata ufumbuzi mzuri, watausoma kwa sauti kubwa kwa kundi la ngambo ya kwanza. Kama kundi la pili litakubali kwamba ufumbuzi huo utaondoa tatizo hilo, basi watatupa kamba ya kuvuka mto kwa kundi la upande uliotoa jibu. Vikundi vitasoma kadi hizo kwa zamu, na kundi lingine litapendekeza ufumbuzi. Kila mshiriki ambaye atakuwa amechangia atashikilia kamba hiyo. Mwisho wa zoezi, kamba itakuwa imevuka mara kadhaa kutoka upande mmoja wa mto kwenda mwingine, na kutengeneza utando au daraja.

    Wakati vikundi vikipendekeza njia za ufumbuzi, nukuu baadhi ya ufumbuzi kwenye karatasi pana ambayo inaweza kusomeka kwa kila mtu.
  6. Baada ya ufumbuzi kwa vikwazo vyote kwenye kadi kutambuliwa, ulizia kama kuna mawazo mapya kwa ajili ya ufumbuzi, halafu hitimisha. Muombe kila mshiriki kufikiria maana halisi ya daraja ambalo linajengwa.
  7. Halafu waombe washiriki wote kujadili mambo gani ambayo yanahitajika ili vijana waweze kupata huduma zote katika kituo cha afya. Pitia hatua tofauti zilizopendekezwa na kutoa fursa kwa washiriki kujadili njia au hatua gani ambazo zinafaa au kuhitajika zaidi. Washawishi washiriki - watu wazima na vijana kufikiria jinsi wanavyoweza kusaidia kuleta mabadiliko.