Hesperian Health Guides

Njia salama za utoaji mimba

Katika sura hii:

Mimba inaweza kutolewa kutoka tumboni na mfanyakazi wa afya ambaye amepitia mafunzo. Zipo njia kadhaa za utoaji mimba:

Utoaji mimba kwa kunyonya au kufyonza (vacuum aspiration, MVA)

Mimba hutolewa kwa kufyonzwa au kunyonywa kwa kutumia mrija maalum ambao huingizwa kwenye tumbo la uzazi kupitia uke na mlango wa tumbo la uzazi (seviksi). Hii inaweza kufanyika bila kumpa mama dawa za usingizi, ingawa wakati mwingine dawa huchomwa kwenye mlango wa kizazi kusaidia kupunguza maumivu. Utoaji kwa njia ya kunyonywa au kufyonzwa ukifanyika kwa mkono, bomba la sindano hutumika kuutoa ujauzito. Ama sivyo, mashine ndogo ya umeme hutumika.

WWHD10 Ch15 Page 244-1.png
cannula
vacuum aspirator
curette

Utoaji kwa mkono kwa kutumia bomba la sindano (MVA) ni rahisi na salama, na huchukua dakika 5 hadi 10 tu. Kawaida hufanyika kwenye kliniki au kituo cha afya, au kwenye ofisi ya daktari. Aina hii ya utoaji mimba ni salama unapofanyika ndani ya wiki 12 za mwanzo (miezi 3) za ujauzito. Baada ya wiki 12, njia hii itumike tu kama mwanamke yupo katika hatari kubwa na huna njia nyingine ya kumsaidia. Njia hii ya MVA husababisha matatizo kidogo ukilinganisha na njia zingine zilizoelezewa hapa chini (njia za upanuaji na ukwanguaji — dilation and curettage).

Katika baadhi ya sehemu, njia ya utoaji mimba kwa kutumia vifaa vya kunyonya au kufyonza (MVA) pia hutumika kutoa nje hedhi ya mwezi iliyochelewa. Mwanamke wakati mwingine anaweza kutojua kuwa ana mimba- kwamba hedhi yake ya kila mwezi haijaja. Hii hujulikana kama kurekebisha hedhi (menstrual regulation). Njia ya MVA pia hutumika kutibu uvujaji damu kutokana na jaribio la kutoa mimba ambalo halikukamilika au mimba iliyoharibika. (Kwa taarifa zaidi juu ya njia ya utoaji mimba kwa vifaa vya kunyonya au kufyonza — soma Kitabu cha Wakunga A Book for Midwives ambacho kimechapishwa na Hesperian.)

Utoaji mimba kwa njia ya kutumia vifaa vya ukwanguaji (upanuaji na ukwanguaji)

Mimba hukwanguliwa kwa kutumia kifaa kijulikacho kama curette, ambacho hufanana na kijiko kidogo na kimetengenezwa maalum ili kingizwe kwenye tumbo la uzazi. Kifaa hiki ni kikubwa kiasi na ni kikali; hivyo, mlango wa kizazi unapaswa kutanuliwa. Utanuaji huu unaweza kusababisha maumivu.

Njia hii ya upanuaji na ukwanguaji huhitaji muda mwingi zaidi (takriban kati ya dakika 15 hadi 20), na huwa na maumivu zaidi, na hugharimu zaidi kuliko njia ya MVA. Kawaida hufanyika kwenye chumba cha upasuaji na mwanamke mara nyingi hupewa dawa za usingizi.

Utoaji mimba kwa dawa (utoaji mimba kitabibu)

Baadhi ya dawa za kisasa hutumiwa na madaktari na wafanyakazi wa afya wengine kutoa mimba. Njia hii ya utoaji mimba kitabibu inahusisha utoaji dawa ambazo husababisha tumbo la uzazi kubana na kuutoa nje ujauzito. Dawa hizi aidha humezwa au kuyeyushwa mdomoni. Iwapo dawa sahihi zitatumika kwa usahihi, njia ya utoaji mimba kitabibu ina ufanisi mkubwa na ni salama. Kwa vile hakuna kitu kinachowekwa tumboni, kuna hatari ndogo ya maambukizi ambacho ndicho chanzo kikuu cha vifo vya wanawake vinavyohusiana na utoaji mimba usiyo salama.
Kabla ya kutumia dawa kwa ajili ya utoaji mimba:

Taarifa zaidi
jinsi ya kutumia dawa kwa ajili ya utoaji mimba
  • Hakikisha unajua jina la dawa na dozi sahihi ya dawa hiyo au dawa zingine ambazo utatumia. Kamwe usitumie dawa ambayo huna uhakika nayo. Kama ni salama, jaribu kuongea na mfanyakazi wa afya unayemwamini kabla ya kutumia dawa hizo.
  • Matumizi ya dawa kwa ajili ya utoaji mimba hufanikiwa zaidi kwa mimba ambayo haijafikisha wiki 9 au siku (63). Anza kuhesabu baada ya siku ya kwanza ya hedhi yako ya mwisho. Unaweza kutumia njia hii ya utoaji kwa dawa hadi wiki 12 za ujauzito, lakini vidonge vitakuwa na ufanisi mdogo na unaweza kupata madhara zaidi ya pembeni, kama vile hedhi nzito, mabonge ya damu, au kichefuchefu.
MUHIMU! Hakikisha upo karibu na kiliniki-mwendo usiozidi saa moja, mahali ambapo unaweza kupata msaada zaidi iwapo ujauzito utatoka na kusababisha kutokwa na damu nyingi, hasa kama mimba ilikuwa na zaidi ya wiki 9. Kutokwa damu na mkakamao wa misuli tumboni ukiwa na maumivu makali, kuhusiana na utoaji mimba kwa dawa, havitofautiani na madhara ya kawaida mimba inapoharibika, na ni vigumu daktari kutofautisha.

Dawa zinazotumika kwa ajili ya utoaji mimba

Kama huwezi kupata huduma salama ya utoaji mimba, wasiliana na Women on Web. Wanaweza kusaidia.

Mifepristone hupatikana katika baadhi ya nchi ambazo zinaruhusu utoaji mimba kisheria. Lakini katika nchi nyingi, dawa hii haipatikani. Kawaida hutolewa kwa njia ya vidonge vya kumeza.

Misoprostol hutumika kwa ajili ya vidonda vya tumbo, na inapatikana katika nchi nyingi. Kawaida hutumika peke yake-bila dawa nyingine kutoa mimba, ingawa hufanikiwa zaidi inapotumika pamoja na mifepristone. Misoprostol inapotumika peke yake ufanisi wake huwa mdogo na madhara ya pembeni huongezeka, hasa ikitumika kwa ujauzito wa zaidi ya wiki 9.

Dalili za ujauzito kawaida hutoweka baada ya saa 48. Kama utaendelea kujisikia kama bado una mimba, nenda kliniki au hospitalini ukachunguzwe. Kuna hatari ya madhara kwa mtoto atakayezaliwa kama utaamua kuendelea na ujauzito huo.

Dalili za hatari baada ya utoaji mimba kwa njia ya dawa (medical abortion)

  • Kutokwa na damu nyingi kupitia ukeni – kulowesha zaidi ya padi kubwa 2 ndani ya saa 1 kwa saa 2 mfululizo. Wahi kliniki au hospitalini mara moja.
  • Homa ambayo huanza siku moja baada ya dozi ya mwisho ya misoprostol na kudumu siku kadhaa inaweza kuwa dalili ya maambukizi (ingawa hii ni nadra kwa utoaji mimba kwa kutumia dawa). Mwone mfanyakazi wa afya aliyepitia mafunzo.

Namna ya kujua kama tendo la utoaji mimba litakuwa salama

Siyo rahisi mara zote kujua kama tendo la utoaji mimba litakuwa salama. Jaribu kwenda kwenye kituo ambako utoaji mimba utafanyika, au uliza mtu yeyote ambaye aliwahi kutembelea kituo hicho masuali yafuatayo:

  • Umewahi kusikia wanawake waliougua au kufariki kutokana na huduma ya utoaji mimba katika kituo hicho? Kama ndiyo, nenda sehemu nyingine.
  • Nani atafanya huduma hiyo na wamepata mafunzo ya namna gani? Madaktari, manesi, wafanyakazi wa afya, na wakunga wa jadi wote wanaweza kutoa mimba. Hata hivyo, utoaji mimba unaofanywa na mtu ambaye hajapata mafunzo juu ya njia za utoaji mimba salama na jinsi ya kuzuia maambukizi ni hatari sana.
chumba kisafi kikiwa na meza ya uchunguzi, vifaatiba ambavyo vimepangwa vizuri, na sehemu ya sinki au beseni na maji yanayotiririka kwa ajili ya kunawia mikono
Chumba hiki kinaonekana salama.
  • Je chumba ambacho kitatumika ni kisafi na nadhifu? Kama ni kichafu na hakipo katika mpangilio mzuri huenda na huduma ndivyo itakavyokuwa.
  • Je kuna sehemu maalum kwa ajili ya kunawa mikono? Mfanyakazi wa afya ambaye hana sehemu ya kunawia mikono yake hawezi kutoa huduma safi na salama.
  • Vifaa vinaonekana kama kwenye picha iliyooneshwa juu, au vinaonekana kama viliokotwa mahali au kutengenezwa nyumbani? Vifaa ambavyo vimetengenezwa nyumbani vinaweza kusababisha majeraha na maambukizi.
  • Vifaa vinasafishwaje na kutakaswa ili kuua wadudu? Vifaa vinapaswa kulowekwa kwenye dawa ya kutakasa (disinfectant) au kuchemshwa kwenye maji ili kuua wadudu ambao wanaweza kusababisha maambukizi.
  • Je gharama ya huduma ikoje? Kama gharama iko juu sana, inaweza kumaanisha kuwa mfanyakazi wa afya anajali fedha tu, na siyo afya yako.
  • Je kuna huduma zingine za afya ambazo zinatolewa sambamba na huduma ya utoaji mimba? Kituo bora cha afya pia kitajitahidi kutoa huduma zingine muhimu ambazo wanawake wanahitaji, kama vile uzazi wa mpango, tiba kwa magonjwa ya ngono na kinga dhidi ya VVU.
  • Utapelekwa wapi kama matatizo yataibuka wakati au baada ya tendo hilo la utoaji mimba? Kunapaswa kuwepo mpango wa kukupeleka hospitali iwapo dharura itatokea.
chumba kichafu sana kikiwa na vifaa duni ambavyo vimezagaa hovyo; na mwanaume aliyekamata chupa amekaa miguu yake ikiwa kwenye meza ya uchunguzi
Chumba hiki kinaonekana siyo salama.


Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Mei 2017