Hesperian Health Guides

Kwa upande wa maafisa afya

Katika sura hii:

Kuwawezesha wanawake waweze kujisaidia wenyewe

Katika sura hii, Petro na Valeria walifanya kazi kubwa kuwasaidia wanawake wa jamii ya Juanita kuweza kutatua tatizo la afya. Sababu ya Petro na Valeria kufanikiwa kiasi hicho ni kwamba hawakuwambia Juanita na rafiki zake nini cha kufanya. Badala yake, Petro na Valeria, waliwawezesha wanawake kujifunza na kuamua nini cha kufanya wao wenyewe.

Wewe pia unaweza kuwawezesha wanawake katika jamii yako kwa kufuata huo mfano wa Petro na Valeria. Unaweza:

  • Kuwamegea maarifa au ujuzi wako. Ili kuweza kujisaidia wenyewe, wanawake wanahitaji taarifa. Matatizo mengi ya afya yanaweza kuzuilika iwapo watu watajua namna ya kuyazuia . Lakini kumbuka kwamba siyo lazima uwe na majibu yote ili uweze kuwawezesha watu. Mara nyingi hakuna jawabu rahisi. Ni vema kukiri wakati hujui jambo fulani. Kwa kufanya hivyo watu unaofanya nao kazi watakuheshimu kwa kuwa mwaminifu.
three women talking
Sina uhakika juu ya suala hili lakini naweza kufuatilia kutafuta ukweli.

Wamegee maarifa na ujuzi ulionao wanawake, wafanyakazi wa afya, na watu wengine wenye mamlaka ya kutoa maamuzi kwenye jamii.

  • Watendee wanawake kwa heshima. Kila mtu anapaswa kutendewa kama vile anao uwezo wa kuelewa matatizo yake ya afya, na uwezo wa kufanya maamuzi mazuri kuhusu matibabu yake. Kamwe usimlaumu mwanamke kwa matatizo ya afya aliyonayo, au kwa maamuzi aliyofanya huko nyuma.
a health worker in an office talking with a woman
Tulichokijadili ni siri. Sitomwambia mtu mwingine.
  • Matatizo ya afya ya mtu ni siri. Matatizo ya afya ya mtu hayapaswi kujadiliwa sehemu ambayo watu wengine wanaweza kuyasikia. Kamwe usimwambie mtu mwingine tatizo la afya ya mtu iwapo mhusika hajaridhia.
  • Kumbuka kwamba kusikiliza ni muhimu zaidi kuliko kutoa ushauri. Mara nyingi mwanamke anahitaji mtu atakaye msikiliza bila kumhukumu. Kwa kusikiliza, unamfanya ajue kwamba unamjali na kwamba yeye ni muhimu. Na kadri atakavyopata fursa ya kuongea, anaweza kugundua kwamba anayo baadhi ya majawabu ya tatizo lake.
  • Mshirikishe mwenye tatizo katika kulitatua, siyo wewe kulitatua kwa niaba yake.Hata kama matatizo ya mwanamke ni makubwa sana na hayawezi kutatuliwa kabisa, bado zipo njia mbalimbali ambazo anaweza kuchukuwa. Kama mfanyakazi wa afya unaweza kumsaidia kutambua njia mbadala alizonazo, na kumsaidia kutafuta taarifa anazohitaji ili aweze kufanya uamuzi wake mwenyewe.
kundi la wanawake wakijadiliana
Jifunze kutoka kwao unaowawezesha, na wao watajifunza kutoka kwako.
  • Jifunze kutoka kwa watu unaowawezesha. Kujifunza jinsi wengine wanavyotatua matatizo yao kunaweza kukusaidia kuwawezesha wengine vizuri zaidi (na pengine hata wewe mwenyewe).
  • Heshimu mila za watu na mawazo yao. Sayansi ya kisasa haina majawabu yote. Na madawa mengi ya kisasa yanatokana na utafiti wa dawa za mimea au mitishamba na tiba za jadi. Kwa hivyo ni muhimu kuheshimu na kuchukua kila chenye manufaa kutoka tiba zote – na kutambua kwamba tiba zote mbili zaweza kusababisha madhara iwapo zitatumika vibaya.
  • Tambua ni kitu gani watu wanapenda kujifunza. Ni rahisi kuangukia kwenye mtego wa kutoa taarifa au elimu bila kutambua iwapo itakuwa na manufaa au la. Hili hutokea mara nyingi kwa wafanyakazi wa afya wanaotoa hotuba zilizoandaliwa kabla. Lakini kama utajitahidi kugundua kwanza hasa watu wanachotaka kujifunza, watapata elimu itakayowasaidia. Hii pia itawasaidia kupanua elimu waliyo nayo tayari.
mfanyakazi wa afya akiongea na kundi la wanawake; mmoja akionekana kutokuwa na hamu na kinachoongelewa
Madini chuma hupatikana kwenye himoglobini, mioglobini na vimeng’enyo mbalimbali. Wakati wa umri wa kuzaa, wanawake wanahitaji miligramu 18 kila siku ili kukidhi mahitaji yao wakati wa hedhi, ujauzito na kunyonyesha.
Naona hawana hamu ya kujifunza juu ya lishe bora.
Sielewi anaongelea nini. Huu ni kupoteza muda!
mfanyakazi wa afya akiongea na kikundi cha wanawake; wote wanasikiliza
Kwanini wanawake wengi wakati wa ujauzito hutokwa na damu nyingi hadi kusababisha kifo ? Sababu mojawapo ni anemia au upungufu wa damu. Wanawake wengi hawali vyakula vya kutosha vyenye madini chuma kama nyama.
Lakini nyama ni ghali sana. Kuna vyakula vingine ambavyo tunaweza kula kupata madini chuma ya kutosha?
  • Panga pamoja na watu, usiwapangie. Wakati unapopanga kazi yako, hakikisha kwamba unaongea kwanza na wanawake na wanaume katika jamii husika. Tafuta mawazo yao juu ya tatizo unalotaka kutatua. Kwa pamoja, zungumzia wanachofikiria kuwa kiini cha tatizo na ni kwa namna gani wangependa kulitatua hilo tatizo. Kufanya kazi pamoja huzaa matokeo mazuri zaidi!


Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Feb 2018