Hesperian Health Guides

Harakati za kuleta mabadiliko

Katika sura hii:

Baada ya Juanita kutumia dawa na kuanza kujisikia vizuri, mtu angeweza kufikiria kuwa tatizo lake lilikuwa limetatuliwa. Lakini Juanita alijua kwamba hiyo haikuwa kweli. Alijua kwamba mumewe akirudi kutoka pwani, angepata maambukizo tena kama mumewe asingetumia dawa na kutumia kondomu. Juanita alijadiliana na Suyapa kuhusu tatizo hilo. Pia alijadiliana na wanawake wengine ambao waume zao hufanya kazi huko pwani, na kwa pamoja waliamua kuomba ushauri kutoka kwa Valeria.

Kutafuta kiini cha matatizo ya afya

Valeria alikubali kwamba tatizo la Juanita lilikuwa bado halijatatuliwa kwa sababu visababishi vilivyochangia tatizo hilo bado vilikuwepo. Kwa hiyo aliamua kufanya zoezi litwalo "Lakini kwa nini...?" ili kumsaidia kila mtu kuainisha visababishi vya kuwepo kwa tatizo hilo.

Valeria aliwakusanya wanawake katika mduara, na kuwataka wajibu maswali yake:

health worker Valeria asking questions that a group of women answer
Kwa nini Juanita aliugua?
Kutokana na maambukizi ya kisonono na klamidia.
Lakini kwa nini alipata kisonono na klamidia?
Kwa sababu aliambukizwa na mumewe.
Lakini kwa nini mumewe alikuwa na kisonono na klamidia?
Kwa sababu alifanya ngono na wanawake wengine.
Lakini kwa nini alifanya ngono na wanawake wengine?
Kwa sababu ya mfumo dume, na pia alikuwa mbali na mke wake kwa muda mrefu.
Lakini kwa nini alikuwa mbali na mkewe kwa muda mrefu?
Kwa sababu hakuwa na ardhi ya kutosha kulisha familia yake na alilazimika kufanya kazi pwani kwa mfululizo wa miezi mingi.
Lakini kwa nini alikuwa na ardhi kidogo kiasi hicho?
Kwa sababu sehemu kubwa ya ardhi inamilikiwa na matajiri wakubwa. (Mjadala mrefu ulifuatia baada ya jibu hili).
Ni sababu gani nyingine iliyomfanya Juanita aambukizwe?
Kwa sababu mumewe hakutumia kondomu.
Lakini kwa nini mumewe hakutumia kondomu?
Kwa sababu hajui jinsi magonjwa ya ngono yanavyoambukizwa.



Baada ya wanawake kutaja orodha ndefu ya sababu, Valeria alipendekeza kuziweka sababu hizo kwenye makundi. Kwa njia hii, ni rahisi kuweza kuona aina tofauti za visababishi vya matatizo ya afya: Sababu za kimwili.
Vijidudu vya magonjwa na vimelea au kitu chochote ambacho hakiendi vizuri kwenye mwili au kinachokosekana kwenye mwili.
Sababu za kimazingira.
Mambo mbalimbali katika mazingira ambayo yanaweza kuudhuru mwili, kama vile moshi utokanao na kupika, ukosefu wa maji safi na salama, au msongamano.
Sababu za kijamii.
Namna ambavyo watu wanahusiana au kutendeana, ikijumuisha mitizamo yao, mila na imani zao.
Sababu za kisiasa na kiuchumi.
Ni sababu zinazohusiana na madaraka — nani ana mamlaka juu ya wengine na anayatumiaje mamlaka haya, na pia kuhusu pesa, ardhi, na raslimali — ni nani anazo rasilimali hizo na nani hana.

Baada ya wanawake kuziweka sababu alizotoa Juanita katika makundi, hatimaye walipata orodha ifuatayo:

women looking at their list of causes
Hii ni orodha muhimu na imekaa vizuri, lakini tunaweza kufanya nini juu ya mambo haya?
    Sababu za kimwili
  • vijidudu vya kisonono.
  • Vijidudu ambavyo vimeonesha usugu kwa dawa.
  • miili ya wanawake ni rahisi kuambukizwa magonjwa ya ngono kuliko ya wanaume, hususan wanapokuwa dhaifu kutokana na mimba.
    Sababu za kisiasa na kiuchumi
  • miji mingi haina fursa za ajira-wanaume lazima waende mbali kutafuta kazi.
  • wanajeshi wa kigeni huchangia kueneza magonjwa ya ngono yasiyotibika kwa urahisi.
  • hakuna dawa ya kutibu vijidudu sugu vya kisonono wala maabara nzuri.
    Sababu za mazingira
  • mji umejitenga mbali na jiji.
  • barabara ni mbovu, zipo katika hali mbaya.
    Sababu za kijamii
  • mara nyingi wanaume wana wenzi wengine wa pembeni.
  • wanaume hawatumii kondomu kutokana na mfumo dume.
  • Ukosefu wa elimu juu ya magonjwa ya ngono.
  • kondomu hazipatikani kwa urahisi.

Kupanga namna ya kutatua matatizo ya afya ya jamii

Hatua iliyofuata, Valeria aliwaambia wanawake, ni kuangalia sababu hizo mbalimbali na kuamua ni zipi wao na wenzao katika jamii, wanaweza kuzibadili. Kisha wafikirie shughuli ambazo zinapaswa kufanyika ili kuleta mabadiliko haya.

Baada ya mjadala mrefu, wanawake walifikia uamuzi kuwa wasingeweza kubadili hali halisi ya waume zao kuacha familia zao kwenda nje kutafuta kazi-au hata kuwazuia kufanya ngono na wanawake wengine. Lakini wangeweza kuwawezesha kutumia kondomu kupitia elimu juu ya magonjwa ya ngono, na iwapo kondomu zitakuwa zinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu. Hatua walizoamua kuchukua ni:

three women discussing actions to take
Tumwombe Petro aongee na wanaume juu ya magonjwa ya ngono kwa vile wanaume wanamheshimu sana na kumsikiliza.
Tukutane sote kwa pamoja tujifunze namna ya kuongea na waume zetu kuhusu kutumia kondomu.
Nitaangalia uwezekano wa kituo cha afya kutoa kondomu bila malipo.

Wanachama wengine kwenye kikundi walipendekeza kufanya yafuatayo:

  • Kuunda kikundi cha jamii kuzungumzia matatizo ya afya, yakijumuisha magonjwa ya ngono.
  • Wakati wanawake watakapokuwa wakifua nguo mtoni, kuongea nao juu ya magonjwa ya ngono na jinsi ya kuyazuia.
  • Kuongea na vijana wa kiume kuhusu magonjwa ya ngono kabla hawajaondoka kwenda pwani kutafuta kazi.

Hatua ya mwisho, Valeria alisema, ni kutengeneza mpango wa kutekeleza mawazo yao kwa vitendo. Mpango huo lazima utoe jibu kwa kila swali lifuatalo:

  • Tunakwenda kufanya nini ? Tutachukua hatua gani?
  • Lini tutafanya mambo haya?
  • Ni akina nani tutawashirikisha?
  • Ni nyenzo au vitu gani tutahitaji?
  • Ni nani anayewajibika kuhakikisha kwamba mpango huu unatekelezwa?
  • Tutajuaje kama mpango unafanikiwa ?
wanawake 3 wakiangalia mpango wao wa utekelezaji
  • Sababu: Wanaume hawatumii kondomu.
  • Shughuli: Wasaidie wanaume kujifunza jinsi magonjwa ya ngono yanavyoambukizwa.
  • Nani/Nini: Petro ataongea na wanaume kuhusu magonjwa ya ngono na jinsi kondomu zinavyozuia maambukizi.
  • Lini: Wanaume watakaporudi kutoka pwani.
  • Ni vitu/nyenzo gani tunahitaji? Kondomu.
  • Ni nani anayewajibika? Juanita atamwomba Petro.
  • Tutatanyaje tathmini? Kuangalia iwapo wanaume wataanza kutumia kondomu.



Ili kukusaidia katika kutumia njia hii ya kutatua matatizo ya afya, ifuatao ni chati yenye hatua zote. Upande wa kushoto ni hatua za kufuata na upande wa kulia ni sehemu husika ya hadithi ya Juanita. Wakati wowote utakapokuwa na tatizo la afya, unaweza kutumia chati hii kukusaidia kukumbuka njia hii ya kutafuta ufumbuzi kwa tatizo husika.

Amua ni visababishi gani ambavyo wewe na jamii yako mnaweza kubadili au kuondoa.
Hatua za kufuata Sehemu husika ya hadithi ya Juanita
1. Anza kwa kutilia shaka 1. Petro hakujua sababu ya tatizo. Alihitaji taarifa zaidi.
2. Tafuta taarifa zaidi kuhusu tatizo hilo kadri inavyowezekana. Uliza maswali zaidi 2. Petro alimwuliza Juanita maswali ili kutafuta ni nini kinaweza kuwa chanzo cha tatizo.
3. Fikiria magonjwa yote ambayo yanaweza kusababisha dalili hizo. 3. Petro alifikiria kuhusu magonjwa yote ambayo yanaweza kusababisha dalili hizo-maambukizo ya ugonjwa wa ngono, aina zingine za maambukizo ukeni, au hata saratani.
4. Angalia vidokezo ambavyo vinaweza kukusaidia kubainisha jawabu sahihi zaidi. 4. Petro alijaribu kuchunguza iwapo uambukizo wa ugonjwa wa ngono unaweza kuwa ndiyo sababu ya tatizo la Juanita.
5. Amua ni jawabu lipi sahihi zaidi. 5. Petro aliamua kwamba huenda Juanita alikuwa na ugonjwa wa ngono.
6. Amua tiba inayofaa zaidi. 6. Petro hakujua bayana ni vijidudu gani vilivyosababisha aina ya ugonjwa wa ngono aliokuwa nao Juanita. Hivyo aliamua kumpa dawa ambazo hutibu magonjwa kadhaa ya ngono.
7. Kama hakuna mafanikio, basi rudia upya. 7. Juanita alitumia vidonge lakini hakupata mafanikio, bali alipata dalili mpya. Petro aliamua kuomba msaada kutoka kwa tabibu mwenye uzoefu zaidi.
8. Chunguza kiini cha tatizo. 8. Juanita na marafiki zake walifikiria visababishi mbalimbali vya magonjwa ya aina hii kwenye jamii yao, kama vile umasikini, ukosefu wa usawa katika umilikaji wa ardhi, mtizamo ya kijinsia, na ukosefu wa taarifa.
9. Weka visababishi hivi kwenye makundi ili kufikiria nini kifanyike. 9. Wanawake waliviweka visababishi hivi katika makundi ya kimwili,kimazingira, kijamii, kisiasa na kiuchumi.
10. Amua ni sababu zipi wewe na jumuiya yako mnaweza kuzibadili.10. Waliamua kuanza kwa kushughulikia visababishi vya kijamii, walifikiri wangeweza kuwafanya wenzi wao watumie kondomu.
11. Amua ni vitendo au shughuli gani ambazo zinaweza kufanyika kuleta mabadiliko yanayotarajiwa. 11. Waliamua kujifunza namna ya kuongea na wenzi wao kuhusu matumizi ya kondomu, kufuatilia iwapo kituo cha afya kingeweza kutoa kondomu za bure, na kumwomba Petro aongee na waume zao kuhusu magonjwa ya ngono.
12. Tengeneza mpango wa kutekeleza vitendo au shughuli hizo. 12. Walitengeneza mpango kwa kila kitendo au shughuli waliyoamua kufanya.



Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Feb 2018