Hesperian Health Guides

Kwa ajili ya wafanyakazi wa afya

Katika sura hii:

Mfanyakazi wa afya akiwa amemtembelea mama mwenye shughuli nyingi na watoto wake 3 Kama wewe ni mfanyakazi wa afya, watembelee watoto mara kwa mara. Muda mwafaka zaidi wa ziara hizi za kitabibu ni kila wakati mtoto anapokuwa amefikia tarehe yake ya kupata chanjo (angalia Chanjo - kinaadaliwa), au kila baada ya miezi kadhaa kwa mwaka wa kwanza, na mara 1 kila mwaka baada ya hapo.

Mtembelee zaidi mtoto atakapoonesha dalili za matatizo ya kiafya, kama vile kukua polepole. Unapaswa pia kurudi (au kumuomba mama kukuona) baada ya kumtibu mtoto kutokana na ugonjwa fulani, kuona iwapo amepata nafuu au anahitaji huduma zaidi.

Japokuwa inaweza kuwa rahisi kuwaomba akina mama kuwaleta watoto wao kwenye kliniki kwa ajili ya uchunguzi,mara nyingi ni bora zaidi kwa mfanyakazi wa afya kuwatembelea nyumbani. Ni bora zaidi watoto wachanga na watoto wadogo kukaa mbali na wagonjwa wengine ambao wanaweza kuwepo kwenye kliniki. Pia, akina mama wengine hawawezi kuwaacha watoto wao wengine au kazi zao, hivyo hawaendi kliniki. Akina mama hao hasa ndiyo wanaohitaji zaidi msaada wa mfanyakazi wa afya kuwapima watoto wao wachanga na watoto wengine wadogo.

Watoto ambao wanahitaji uangalizi wako zaidi ni wale ambao huwa hawaji kwako kukuomba msaada.


  • Ulizia kuhusu hali ya mtoto - kama anaendelea vizuri kiafya na anakua vizuri.
  • Mwangalie mtoto kuanzia kichwa hadi kidole. Mtoto mwenye afya huwa timamu na pia mwenye shauku. Ngozi yake inakuwa haijaharibiwa na madoa au vitu vingine, na mwili wake ukiendelea kuongezeka na kuwa na nguvu zaidi.
  • Ulizia kuhusu ulaji wa mtoto. Watie wazazi moyo kuendeleza unyonyeshaji na chakula chenye virutubishi.
  • Mpime mtoto uzito. Au kama mama yake amekua akishiriki katika huduma ya ufuatiliaji wa ukuaji wa mtoto, angalia kutoka kwenye kumbukumbu jinsi mtoto amekua akiendelea (angalia popote ambapo taarifa za maendeleo ya uzito wa mtoto zimeorodheshwa).
  • Tazama kuona iwapo mtoto ni msafi na iwapo mazingira ya nyumbani ni salama kiafya. Ziara hizi zinaweza kutoa fursa ya kuifundisha familia juu ya usalama na uzuiaji wa magonjwa, au kujua wanahitaji msaada gani kuifanya kaya yao kuwa salama zaidi na mtoto kuwa na afya nzuri zaidi.
  • Hakikisha unawashirikisha mama na familia kile ulichojifunza katika ziara hiyo.

Huduma kwa watoto ni njia moja wapo ya wafanyakazi wa afya kujipatia uaminifu na heshima kutoka kwa jamii. Wazazi watakapokuwa wanaona ukiwahudumia watoto wao, watajisikia huru zaidi kukuulizia maswali juu ya afya zao wenyewe. Kukagua maendeleo na afya ya mtoto mara kwa mara ni njia nzuri ya kuhakikisha kuwa mama na wanafamilia wengine pia wanaendelea vizuri na kupata huduma wanazozihitaji.

Tumia fursa hizo kuwafundisha watoto juu ya afya. Watoto huzungumzia kila wanachojifunza na familia zao na watoto wengine. Wanaweza kusaidia kuanzisha mlipuko wa tabia njema za kiafya katika jamii.

Mtoto anapoongezeka ina maana ana afya nzuri

Tunza kumbukumbu za ukuaji wa mtoto kwenye kadi, kama ilioyoonyeshwa chini. Mama au mtoa huduma anapaswa kutunza kadi hii. Mweleze jinsi inavyotumika, ili aelewe kama mtoto wake anarudi nyuma au la.

Mwonekano wa kadi ya afya ya mtoto


Mwonekano wa kadi ya ufuatiliaji wa ukuaji wa mtoto

Jinsi ya kutumia kadi hii

Mwonekano wa kadi miezi ya maisha ya mtoto ikiwa imeandikwa chini
Hatua ya 1
Andika mwenzi wa mwanao kuzaliwa, hapa:
Kadi inaoonesha mtoto alizaliwa Aprili.
Hatua ya 2
Andika miezi mingine inayofuatia mwezi wa mtoto wako kuzaliwa.
Mwonekano wa kadi yenye tone ambalo linaonesha uzito wa mtoto mwezi huu
Hatua ya 3
Kila mwezi pima uzito wa mtoto wako katika kilo.
Weka tone kwenye kadi mahali ambapo uzito wa mtoto unakutana na mwezi huu.
Mwonekano wa kadi yenye matone mengi yakionesha mwenendo wa ukuaji wa mtoto katika kipindi fulani
Hatua ya 4
Kila mwezi mpime mtoto uzito na kuongeza tone lingine kwenye kadi. Unganisha matone hayo na msitari.
Kwa watoto wengi wenye afya nzuri, msitari wa matone huwa kati ya laini hizi 2.
ANGALIA MWELEKEO WA MSITARI AMBAO UNAONESHA UKUAJI WA MTOTO. Kielelezo cha maendeleo bora, kikiwa na msitari wa matone unaokwenda juu; mwelekeo hatari kukiwa na msitari wa matone unaokwenda tambarare; na mwelekeo hatari sana, msitari wa matone ukiwa unakwenda chini.
Jambo muhimu ni kwamba mtoto anapaswa kuendelea kukua.
Msitari wa matone kamwe usiendelee kuwa tambarare.
Au usiende chini.

Iwapo utagundua kwamba mtoto haongezeki, mtembelee mara nyingi zaidi. Angalia kama unaweza kumwezesha kupata chakula zaidi. Chunguza iwapo kuna ugonjwa ambao unakwamisha ukuaji wake.

Maendeleo

Maendeleo humaanisha uwezo wa mtoto kukua. Jinsi anavyotumia mwili wake, anavyowasiliana na anavyojifunza kutatua matatizo: atakuwa anafanya hayo kwa namna yake ya pekee. Lakini anapaswa wakati wote kuendelea kutoka hatua moja hadi nyingine badala ya kukwama katika hatua moja. Kama mtoto atakuwa akiendelea polepole, anahitaji huduma ya ziada.

Kwa nini baadhi ya watoto hukua polepole kuliko wengine? Wakati mwingine hakuna sababu-tofauti kati ya watu ni jambo la kawaida. Lakini ugonjwa na lishe duni vinaweza kupunguza maendeleo ya mtoto kwa njia zisizo za kawaida. Aina mbalimbali za ulemavu pia zianaweza kuathiri maendeleo ya mtoto. Kwa mfano, unaweza kutojua mara moja kwamba mtoto ana uziwi. Badala yake, unaweza kugundua kwamba hajifunzi kuongea mapema kama dada au kaka zake walivyofanya. Angalia maendeleo ya mtoto wako kwa sababu kuendelea polepole kunaweza kuwa dalili kwamba ana tatizo la kiafya au ulemavu ambao unahitaji kushughulikiwa haraka.

Mtoto wa miezi 3 anapaswa:
  • Kutabasamu
  • Kuitikia sauti au matembezi
  • Kuonyesha hisia kwa sauti au nyuso alizozoea
  • Kutambua mikono yake


Mtoto akiwa amelala upande akicheza na mikono yake

  • Kulia anapokuwa na njaa au kutojisikia vizuri
  • Kunyonya bila matatizo makubwa
  • Kuinua kichwa chake anapokuwa amelalia tumbo lake
Mtoto aliyelalia tumbo lake akiwa ameinua kichwa chake
Mtoto wa miezi 6 anapaswa:
  • Kugeuza kichwa chake kuelekea mahali sauti zinapotoka
  • Kujiviringisha kutoka tumbo lake kuelekea mgongo wake, na kurudi kwenye tumbo lake


Mwanaume akichezesha kinya’nga na mtoto wake mchanga,akiwa amelalia tumbo lake na kuinua kichwa
  • Kuwatambua watu aliowazoea
  • Kuokota vitu chini na kuviweka mdomoni
Mtoto akiweka kitu cha kuchezea mdomoni
Mtoto wa mwaka 1 anapaswa:
  • Kuelewa na kuiga sauti na maneno rahisi
  • Kucheza michezo rahisi


Mwanaume na mtoto wakicheza
  • Kujaribu kuweka kitu kimoja ndani ya kingine
  • Kukaa na kutambaa bila msaada
  • Kujivuta na kuwa katika hali ya kusimama


Mtoto akitumia kimeza ndogo kujivuta ili aweze kusimama


Mtoto wa miaka 3 anapaswa:
Msichana akiwa na mdogo wake wakifagia
  • Kuelewa na kuongea sentensi rahisi
  • Kufanya kazi ndogondogo kama kufagia
  • Kutambua hisia za watu wengine
Mtoto akikimbia
  • Kuchambua vitu
  • Kukimbia, kuruka na kupanda

Kama mtoto atakuwa anaendelea polepole, unaweza kufanya mambo 2 kusaidia:

  1. Muombe mfanyakazi wa afya kuchunguza iwapo kuna sababu yoyote ya kiafya ambayo inahusika na kusuasua kwa maendeleo ya mtoto.
  2. Weka bidii zaidi kwenye nyanja ambazo mtoto anachukua muda mrefu kuendelea.
Mwanamke anaongoza mikono ya mtoto wake ili kumsaidia kuonja kitu
Msaidie mtoto kupiga hatua katika maeneo ambayo anaonekana kuwa nyuma.

Angalia Kimbatisho A kwa ajili ya kadi zote za maendeleo ya mtoto. Kadi hizo ni nyenzo muhimu kwa wazazi na pia wafanyakazi wa afya kutunza kumbukumbu za maendeleo ya mtoto na kumsaidia kadri anavyokua.