Hesperian Health Guides

Jinsi ya kula vizuri unapokuwa na uwezo mdogo

Katika sura hii:

Katika dunia mahali ambapo baadhi ya watu wana ardhi, rasilimali, na fedha na wengine hawana, njaa itaendelea kuwepo. Na vipindi vya njaa vitaendelea kutokea iwapo vita, milipuko ya magonjwa, uchafuzi wa mazingira uliokithiri, ukosefu wa utunzaji bora wa ardhi, na sera zinazowalazimisha watu kuhama vitaendelea kuibuka. Sababu hizi za ukweli na msingi juu ya njaa lazima zishughulikiwe ili kuhakikisha kila mtu anapata chakula cha kutosha.

Lakini familia au jamii moja inaweza kula vizuri hata kama wana rasilimali kidogo. Na kwa kula vizuri, wanaweza kupata nguvu za kuzalisha mali na kusimama imara kupigania haki zao za kibinadamu.

Chombo chenye unga, mchele, mayai matunda na mbogamboga

Mbinu za kupata mlo wa kutosha na wenye lishe

  • Nunua vyakula vya kawaida visivyo ghali kama vile maharagwe, na nafaka. Vyakula hivi vina virutubishi zaidi na gharama yake ni nafuu kuliko vyakula ambavyo vimetengenezewa viwandani kama vile mikate mieupe, biskuti, na supu za kwenye makopo, au asusa.
NWTND Nut Page 13-2.png
  • Kama unaishi vijijini, chuma au hata winda vyakula vya asili kama vile uyoga unaoliwa, mboga za majani za porini na matunda, wanyama wadogo, au wadudu. Vyakula hivi mara nyingi huwa na virutubishi vingi, na havigharimu fedha.
Mwanamke akipanda mimea katika vyombo, kwenye baraza ya nyumba yake ghorofani
  • Fuga kuku kwa ajili ya mayai na nyama. Baadhi ya watu hujenga mabwawa madogo ya kufugia samaki kwa ajili ya kula.
  • Panda chakula chako mwenyewe kwenye vyombo au bustanini.
  • Nunua chakula kila mara kwa wingi. Kununua chakula kidogo kidogo-kwa bei ya rejareja- huwa ghali zaidi kuliko kununua chakula kwa wingi –kwa bei ya jumla, chakula ambacho unaweza kutumia kwa muda mrefu zaidi. Kama huwezi kumudu chakula kingi kwa wakati mmoja, unaweza kushirikiana na jirani yako au mwanafamilia, na baadaye kugawana gharama.
Mwanamke akimnyonyesha mtoto wake
  • Watoto wachanga na watoto wadogo wanahitaji maziwa ya mama — siyo maziwa au vyakula vya viwandani. Maziwa ya mama ndiyo lishe bora zaidi kwao na hayana gharama.
  • Epuka vyakula vya makopo yakiwemo maziwa yaliyoongezewa ladha ambavyo huuzwa kwa ajili ya watoto wachanga na watoto wadogo. Vyakula hivi ni kupoteza fedha. Maziwa ya kawaida ya wanyama, au vyakula ambavyo vimepikwa vizuri na kupondwapondwa vina gharama nafuu zaidi na pia huleta afya zaidi kwa watoto kuliko “vyakula vya watoto wachanga” vilivyofungashwa viwandani au “maziwa ya watoto”
Kopo la maziwa ya mtoto ya unga,karatasi iliyobandikwa juu inasema yana kiwango kidogo cha vitamini, na madini,sukari na mafuta zaidi kuliko maziwa halisi. Pia ni ghali zaidi
  • Usitupe mchuzi wa maharagwe, nyama au mbogamboga ambao hutokea wakati wa kupika. Mchuzi huu umesheheni virutubishi na unaweza kuzuia anemia. Kunywa au tumia mchuzi huo kupika nafaka au vyakula vingine. Au pika na maji kidogo na kufunika chombo-ili virutubishi vibaki ndani.
  • Tumia fedha uliyonayo kwa ajili ya chakula. Pombe, tumbaku, na pombe au soda hugharimu fedha nyingi na havina tija kilishe.