Hesperian Health Guides

Kula chakula cha kutosha

Katika sura hii:

Kila mtu anahitaji kula chakula cha kutosha. Chakula cha kutosha hutupatia nishati na nguvu ambavyo miili na nafsi zetu huhitaji kila siku.

Ukosefu wa chakula kwa wiki kadhaa au miezi husababisha matatizo makubwa ya kiafya na ambayo hudumu kwa muda mrefu. Watoto, wazee, wagonjwa, watu wanaoishi na VVU, na wanawake wenye ujauzito huathirika zaidi (na haraka) kutokana na ukosefu wa chakula. Hivyo, ni muhimu kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha, hasa kwa watu wenye uwezo mdogo wa kujitunza wenyewe.

Watoto hasa wanahitaji chakula cha kutosha

Kuliko mtu mwingine yeyote, watoto wanahitaji chakula cha kutosha kila siku. Ukosefu wa lishe bora mwanzoni wakati wa utotoni husababisha udumavu wa kimwili, kushambuliwa na magonjwa mara kwa mara, na matatizo ya kujifunza ambayo hudumu kwa maisha yote.

Ili kuhakikisha watoto wanapata lishe bora na ya kutosha:

  • Wanyonyeshwe au kupewa maziwa ya mama pekee bila chakula au kinywaji kingine hadi watakapoota meno yao ya kwanza — takriban wanapofikisha miezi 6.
  • Hata kama utaanza kumpa mtoto chakula anapofikisha miezi 6, endelea kunyonyesha. Ni bora zaidi kunyonyesha hadi miaka 2 au hata zaidi. Kumpatia mtoto maziwa ya mama na chakula huhakikisha mtoto kamwe hatakosa kile anachohitaji kukua na kustawi.
  • Utakapoanza kumpatia chakula, mpe kidogo kidogo mara kadhaa kwa siku. Halafu ongeza aina ya vyakula na kipimo. Mtoto wa miaka 2 anapaswa kula angalau mara 4 kwa siku. Mtoto ambaye ameacha kunyonya anahitaji milo zaidi kuliko yule ambaye bado ananyonya.
  • Watoto wadogo watengewi chakula kwenye vyombo vyao wenyewe. Halafu uhakikishe kuwa kila mtoto amekula chakula chake.
  • Wape wasichana chakula sawa na wavulana. Wasichana na wavulana wanahitaji chakula kinacholingana ili wote waweze kuwa na afya na wenye nguvu.
  • Tibu tatizo la kuhara mara moja kwa kutumia kinywaji maalum cha kuongeza maji mwilini (rehydration drink) na vinywaji vingine.
  • Tumia dawa ya mebendazo (mebendazole) kuwatibu watoto wanapokua na minyoo. Kama watoto wengi katika eneo hilo wana minyoo toa dawa ya mebendazo kwa watoto wote kwenye jamii yako kila baada ya miezi 6 kuzuia maambukizi.

Katika umri tofauti, watoto wanahitaji chakula kwa mahitaji mbalimbali. Bonyeza hapa kujifunza zaidi jinsi ya kuwalisha watoto wachanga na watoto wadogo.