Hesperian Health Guides

Utangulizi

Katika sura hii:

Uhamasishaji Jamii Juu ya Afya ya Mazingira ni moduli ya kwanza kutoka katika Mwongozo wa Jamii juu ya Afya ya Mazingira. Mwongozo huu uliandaliwa na Hesperian Foundation kwa ushirikiano na mashirika na vikundi vya kijamii kutoka zaidi ya nchi 33.

Mwongozo wa Jamii juu ya Afya ya Mazingira unajumuisha mawazo na uzoefu wa wadau kuhusu afya ya mazingira kutoka nchi zinazoendelea na zilizoendelea. Ni mkusanyiko wa mawazo, njia, maelezo, na ufumbuzi wa vitendo kutoka jamii mbalimbali kote duniani kwa manufaa ya wafanyakazi wa afya, walimu, wanaharakati wa maswala ya kijamii, wataalam wanaofanya kazi katika miradi ya maendeleo, na wote wale ambao wanataka kuboresha afya zao na za jamii zao.

Baada ya kupata idhini kutoka Shirika la Hesperian Foundation na msaada kwa ajili ya kuchangia kuutafsiri katika Kiswahili, COBIHESA kwa kushirikiana na wadau wengine nchini tulifikia uamuzi wa kuugawa mwongozo huu katika moduli 4. Sababu kuu ikiwa ni kurahihisha matumizi yake katika ngazi ya jamii, hususan ubebaji, usomaji na kwa ajili ya uwezeshaji wa mafunzo juu ya afya ya mazingira katika ngazi ya jamii. Moduli hizo 4 ni:

1. Uhamasishaji wa jamii kwa ajili ya afya ya mazingira

2. Tuhifadhi maliasili kwa manufaa ya wote

3. Usimamizi wa taka ngumu na kemikali za sumu

4. Ujenzi wa vyoo na matumizi yake


Kila moduli imegawanywa katika sehemu kadhaa zikiwa na malengo mahsusi. Maelezo ndani ya moduli hizi pia yamesindikizwa na michoro ya watu, mitambo na mazingira mbalimbali. Baadhi ya watu huenda wasifanane na watu katika jamii yako. Bila kujali wanaishi wapi,wanavaa namna gani na nyumba zao zikoje, wote wanapambana na changamoto za afya ya mazingira. Hivyo tunaweza kujifunza kutoka kwao na mazingira ya nchi zao.

Nani anastahili kutumia mwongozo huu?

Mwongozo huu unafaa sana kwa ajili ya matumizi ya mashirika yasiyo ya kiserikali na vikundi vya kijamii na wanachama wake,wafanyakazi wa serikali wa ugani katika sekta zote, walimu na hata wanafunzi shuleni na vyuoni, na wanaharakati wa mazingira na maendeleo kwa ujumla.

Nitautumiaje mwongozo huu kwa mafanikio zaidi?

Soma malengo ya moduli, halafu endelea hatua kwa hatua. Ipo mifano hai, visa mafunzo na michoro juu ya uzoefu wa jamii kuhusu afya ya mazingira kutoka nchi mbalimbali. Hali hii huufanya mwongozo huu kuwa rafiki kwa mtumiaji.

Mwongozo huu ni chanzo muhimu cha maarifa juu ya afya ya mazingira. Hivyo soma kwa lengo la kujifunza. Lakini pia ni zana ambayo unaweza kutumia kuwezesha watu wengine ndani ya familia, jirani, shuleni, vyuoni, katika vikundi, au hata kupitia vipindi vya redio.

Wasomaji na watumiaji wanahimizwa sana kusoma moduli zote tatu na kuzitumia kwa ukamilifu katika kazi ya kulinda na kuboresha afya ya jamii na mazingira kwa ujumla.

Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Jan 2024