Hesperian Health Guides

Upandaji upya misitu

Katika sura hii:

Misitu ya kale (misitu ya zamani ambayo haijawahi kukatwa au kuharibiwa vibaya) inazidi kuwa adimu. Pale msitu wa kale unapotoweka, hautaweza kuota tena na kuwa na aina mbalimbali za mimea na wanyama ambao walikuwepo awali. Lakini misitu itakayofuata (misitu iliyoharibiwa lakini ikarudia kuota) inaweza kuwa na rasilimali kama zile za misitu ya kale endapo itaruhusiwa kukua na kusheheni bioanuwai. Na misitu inayopandwa na watu na kusimamiwa vizuri inaweza pia kutoa rasilimali nyingi kwa ajili ya afya ya jamii.

Msitu uliostawi huchukua muda mrefu kukua, lakini kuna mambo mengi ambayo unaweza kufanya ili kuupa mwanzo mzuri. Kudhibiti mmomonyoko, kuandaa udongo na kupanda miti ya asili, au miti ambayo inafaa katika eneo lako husaidia msitu kukua vizuri.

Je upandaji miti husaidia wakati wote?

Kabla ya kuanza mradi wa jamii wa upandaji miti, unapaswa kuwa na uhakika kwamba mradi huo utakidhi mahitaji ya jamii na mazingira yake. Miti inaweza kushindana na mazao kwa ajili ya maji na ardhi kidogo iliyopo. Mara nyingi ni vigumu kutunza miti michanga katika mazingira mabaya. Kupanda miti mahali ambapo haitaweza kutunzwa huchangia mradi na miti yenyewe kufa.

Kama jamii yako inategemea sana mazao ya msitu, mathalan mbao au matunda, upandaji miti unaweza kuwa njia sahihi na ya haraka ya kunufaika na rasilimali za misitu. Kama jamii yako inategemea zaidi msitu kwa ajili ya uwindaji au kuhifadhi ardhi, hewa na maji, basi unaweza kunufaika zaidi kwa kuilinda ardhi hiyo isitumike wakati miti inaendelea kukua kwa wakati wake.

Misitu haistawi na wala haistahili kuoteshwa sehemu zote. Ni miti michache ambayo inaweza kuota yenyewe jangwani, maeneo yenye tingatinga na hata savanna. Iwapo watu watajaribu kupanda miti katika maeneo haya, inaweza kuvuruga uwiano wa asili kati ya miti na wanyama. Lakini katika maeneo mengine ambapo miti ni michache, kama vile miji na majiji, kupanda miti kando kando ya barabara, karibu ya viwanda na kwenye maeneo ya kupumzikia kunaweza kuboresha afya na ustawi wa jamii.

Nani anamiliki ardhi na sheria zinasemaje?

Kama unataka kuhifadhi ardhi na kupanda msitu upya, na baadaye uweze kuvuna mazao yake, hakikisha kwamba utaruhusiwa kuutumia msitu pale utakapokua. Kujua mapema nani mmiliki kisheria wa ardhi inayotarajiwa kupandwa msitu na kupata kibali chake kabla ya kupanda miti itasaidia kuepuka matatizo baadaye. Ardhi ambayo kwa sasa inaonekana duni na haina rutuba itaongezeka thamani mara itakapofunikwa na msitu uliostawi. Pia baadhi ya maeneo yana sheria zinazozuia watu kukata au kutumia aina fulani ya miti hata kama walipanda wenyewe. Chunguza iwapo kuna sheria za aina hii mahali unapoishi.

Kila aina ya mti ina matumizi yake tofauti

Uamuzi kuhusu aina gani ya miti ya kupanda ni bora ukazingatia mahitaji na matakwa ya watu katika jamii husika.

People sit together and discuss.
Kama tunataka sehemu ya kuburudika na kustarehe...
...tunapaswa kupanda miti yenye kivuli katika maeneo ya umaa, kama vile bustani.
Lakini tunahitaji pia kulinda vyanzo vyetu vya maji?
Tunapaswa kupanda miti ambayo hukua polepole kandokando na mito na kuzunguka chemchemi
People sit together and discuss.
Tunahitaji kuzuia mmomonyoko...
...tunaweza kupanda miti yenye mizizi mirefu kwenye miinuko ya milima ambayo ilipoteza misitu yake.
People sit together and discuss.
Tunahitaji chakula, dawa na majani kwa ajili ya mifungo yetu.
Tunaweza kupanda miti mchanganyiko katika ardhi ya umma ili kila mtu awe huru kuitumia.


Ingawa inaweza kuchukua muda mrefu na subira, maarifa na mahitaji ya kila mtu yakizingatiwa, tunaweza kuandaa mpango mzuri wenye manufaa kwa jamii nzima.




Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022