Hesperian Health Guides

Sura ya 4: Kuielewa miili yetu

HealthWiki > Pale ambapo Wanawake hawana Daktari > Sura ya 4: Kuielewa miili yetu

Katika sura hii:

Sura hii inahusu sehemu za mwili ambazo hutengeneza mfumo wa uzazi wa mwanamke au mwanaume. Taarifa hii itakusaidia kutumia vizuri sehemu za kitabu hiki zilizobaki.
WWHND10 Ch4 Page 43-1.png
Balehe
Kila mwanamke hubadilika kutoka usichana na kuwa mwanamke...
WWHND10 Ch4 Page 43-2.png
Umri wa kuzaa
...na baada ya hapo kutoka kuwa mwanamke na kuwa mwanamke mwenye umri zaidi.
WWHND10 Ch4 Page 43-3.png
Hedhi kukomaa
Sehemu ya nyonga ya mwanamke
mifupa ya nyonga
Unaweza kuhisi mifupa yako ya nyonga chini kidogo ya kiuno. Mifupa hii ni sehemu ya nyonga. Sehemu ya nyonga ni kila kitu kati ya mifupa ya nyonga. Hapo ndipo sehemu za uzazi za mwanamke zilipo.

Kwa kiasi kikubwa mwili wa mwanamke hautofautiani na wa mwanaume. Kwa mfano, wanawake na wanaume wote wawili wana moyo, figo, mapafu na sehemu zingine zinafanana. Lakini tofauti kubwa ni viungo vya uzazi vya mwanamke na mwanaume. Hivi ndivyo viungo vinavyomwezesha mwanaume na mwanamke kutengeneza mtoto. Matatizo mengi ya afya ya wanawake yanahusiana na viungo vya uzazi.

Mtu yeyote hapaswi kuona aibu kwa sababu ya sehemu yeyote ya mwili wake.

Wakati mwingine ni vigumu kuongelea kuhusu viungo vya uzazi, hasa kama wewe ni mtu mwenye aibu au ikiwa hujui majina ya sehemu hizi. Mahali pengi, viungo vya uzazi huchukuliwa kama sehemu za siri.

Lakini kuelewa jinsi sehemu za miili yetu zinavyofanya kazi hutusaidia kujua namna ya kuzitunza vizuri zaidi. Tunaweza kutambua mapema matatizo na sababu zake na kuweza kufanya maamuzi jinsi ya kuyashughulikia. Kadri tunavyoelewa ndivyo tutakavyokuwa na uwezo wa kufanya maamuzi juu ya ushauri tunaopata kutoka kwa watu wengine- iwapo unafaa au la.

Kwa vile jamii tofauti wakati mwingine huwa na majina tofauti kwa viungo vya mwili, katika kitabu hiki tutatumia majina ya kisayansi au kitabibu. Kwa njia hii, wanawake wengi kutoka maeneo tofauti ya dunia wataweza kuyaelewa maneno yaliyotumika.


Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Jan 2024