Hesperian Health Guides

Hadithi ya Mira

Katika sura hii:


msichana akipiga picha akilini akiwa na mume wake mwenye sura nzuri na mwenye huruma

Mira alipokuwa msichana mdogo, alikuwa na ndoto ya kuishi kwenye nyumba kubwa, yenye umeme na sakafu ya vigae. Mume wake angekuwa mzuri na mwenye huruma, na angeweza kufanya lolote apendalo. Lakini familia ya Mira ilikuwa na hali duni na Mira alikuwa mtoto wa mwisho kwenye familia ya mabinti wanne. Wakati mwingine, baba yake alikuwa akinywa pombe na kumpiga mama yake, akilia kwa sababu ya ‘balaa’ ya kuzaa wasichana wengi.

Mira alipofikisha miaka 14, aliangua kilio alipogundua kuwa ndoto zake zisingeweza kuwa kweli. Tayari ilikuwa imepangwa aolewe: Mira angeolewa na mwanaume aliyechaguliwa na baba yake. Alikuwa na ardhi na baba yake Mira alidhani familia itafaidika kutokana na ndoa hiyo. Mira hakuwa na maamuzi katika jambo hilo.

Baada ya mtoto wake wa 2 kuzaliwa — mtoto wa kiume — mumewe aliacha kusisitiza kufanya tendo la ndoa mara kwa mara. Mira alifurahishwa sana na jambo hilo. Ingawaje mume wake alikuwa hamuumizi Mira, alikuwa na vidonda sehemu yote ya uume, jambo lililomnyima raha. Miaka zaidi ya 20 iliyofuata, Mira alipata zaidi ya watoto 6, pamoja na binti mdogo aliyefariki akiwa na umri wa miaka 3, na mvulana aliyefariki mara baada ya kuzaliwa.

Siku moja Mira alipokuwa chooni, aligundua damu iliyokuwa ikitokea ukeni wakati haikuwa kipindi chake cha hedhi. Mira alikuwa hajawahi kufanyiwa uchunguzi wa afya, na hivyo alimwomba mumewe iwapo angeweza kumwona daktari. Mumewe alimjibu kwamba hawaamini madaktari na zaidi ya hayo, hakuwa na fedha. Mira alikuwa na miaka 40 wakati alipoanza kuumwa mfululizo maumivu chini ya tumbo. Maumivu yalimpa wasiswasi lakini hakujua ni nani wa kuongea naye kuhusu jambo hilo. Miezi kadhaa baadaye, hatimaye Mira aliamua kwenda kinyume na matakwa ya mumewe na kwenda kupata msaada wa kiafya. Alikuwa amepata hofu juu ya maisha yake na kuamu kukopa fedha kutoka kwa rafiki yake.

Katika kituo cha afya, Mira alipata dawa kwa ajili ya tatizo la kutokwa damu ukeni ingawaje hakufanyiwa uchunguzi. Mira alirudi nyumbani usiku huo akiwa mchovu na mwenye masikitiko kwa kwenda kinyume cha matakwa ya mumewe, na kutumia akiba ya rafiki yake. Kadri wiki zilivyopita, afya ya Mira ilizidi kuwa mbaya na alianza kukataa tamaa kwa kugundua kwamba kulikuwa na tatizo.

Mira amelala kitandani, akionekana kuwa anaumwa sana, wakati mume wake na watoto wake wakiwa wameketi pembeni karibu naye

Mwishowe hali ya Mira ilizidi kuwa mbaya sana na mumewe kuamini kuwa kweli ni mgonjwa. Waliazima baiskeli na kumpeleka hospitali ya mjini. Baada ya kusubiri kwa siku kadhaa, Mira alihudumiwa hospitalini na kuambiwa kwamba alikuwa na saratani ya shingo ya kizazi iliyokomaa. Daktari alisema kwamba angeweza kuondolewa kizazi lakini saratani tayari ilikuwa imesambaa sana.

Tiba pekee ambayo ingeweza kuokoa maisha yake ilikuwa inapatikana upande mwingine wa nchi na ni ghali sana. Kisha daktari aliuliza, “Kwa nini hukua unafanya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi mara kwa mara? Iwapo tungeigundua mapema, tungeweza kulitibu tatizo kwa urahisi.” Lakini tayari Mira alikuwa amechelewa sana. Baadaye, Mira alirudishwa nyumbani na kabla haijapita miezi miwili, alifariki dunia.

Kwa nini Mira alifariki dunia?

Yafuatayo ni baadhi ya majibu ya kawaida kwa swali hili:

Daktari anaweza kusema...
WWHND10 Ch1 Page 10-1.png
Mira alikufa kwa sababu ya saratani ya shingo ya kizazi iliyoenea sana kwa sababu hakupata matibabu mapema.
Au mwalimu anaweza kusema...
WWHND10 Ch1 Page 10-2.png
Mira alikufa kwa sababu hakujua kwamba alipaswa kufanyiwa uchunguzi wa saratani ukeni mara kwa mara.
Au mfanyakazi wa afya anaweza kusema...

WWHND10 Ch1 Page 10-3.png

Mira alikufa kwa sababu mumewe alimwambukiza vidonda alivyokuwa navyo kwenye ume pamoja na magonjwa mengine ya ngono (STDs). Maambukizi haya yalimweka Mira katika hatari kubwa ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.

Majibu hayo yote ni sahihi. Wanawake wanaoanza kufanya mapenzi katika umri mdogo na kuambukizwa vidonda ukeni, wapo katika hatari kubwa ya kupata saratani ya shingo ya kizazi. Na iwapo saratani hii itagundulika mapema kupitia uchunguzi wa shingo ya kizazi au kupitia kipimo cha Pap test, mara nyingi huweza kutibika.

Hata hivyo majibu haya yanaonesha kiwango kidogo cha uelewa wa tatizo. Kila mmoja anamlaumu mtu mmoja — ama Mira au mume wake — bila ya kwenda mbali zaidi. Mira alikuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupoteza maisha yake kutokana na saratani ya shingo ya kizazi kwa sababu alikuwa mwanamke mwenye hali duni kiuchumi, aliyeishi katika nchi vile vile yenye huduma za afya duni.

visababishi vya afya duni ni pamoja na ndoa za utotoni au za mapema, kukosa uwezo wa kufanya maamuzi katika mahusiano,ukosefu wa elimu ya afya, ukosefu wa fedha za kulipia huduma za afya,wafanyakazi wa afya ambao hawajapitia mafunzo juu ya afya ya wanawake, na ukosefu wa huduma za afya kwa wanawake.
Vifuatavyo ni baadhi ya viunganishi ambavyo kwa pamoja vilichangia kifo cha Mira kama vinavyoonekana kwenye mnyororo hapo chini. Viunganishi hivyo pia ndivyo huchangia matatizo mengi ya afya ya wanawake.

Jinsi umaskini na hadhi duni ya wanawake kwa pamoja vilivyosababisha kifo cha Mira

Unaweza kuchunguza kiini cha sababu za kifo cha Mira au sababu za matatizo mengine ya afya kwa kutumia zoezi liitwalo, "Lakini ni kwa nini?"

Mira na familia yake walikuwa na hali duni kiuchumi, hivyo aliozwa na kuanza kufanya ngono akiwa bado mdogo sana. Akiwa mwanamke, alikosa mamlaka katika uhusiano wake na mumewe. Alikuwa hana mamlaka ya kuweza kuamua lini apate mtoto na awe na watoto wangapi, hakuwa na mamlaka juu ya mumewe kuhusu mahusiano yake na wanawake wengine. Umaskini wa familia yake ulimaanisha kuathirika kilishe kwa maisha yake yote, jambo ambalo lilidhoofisha mwili wake na kumwacha katika hatari zaidi ya magonjwa.

Ingawa jamii ya Mira ilikosa huduma za afya, lakini kituo cha afya cha karibu kilikuwa na huduma za afya kwa wanawake kama vile uzazi wa mpango na elimu na ushauri juu ya VVU na UKIMWI. Hata hivyo, wafanyakazi wa afya hawakuwahi kupewa mafunzo kuhusu matatizo mengine ya afya ya wanawake, yakiwemo magonjwa hatari kama vile saratani ya shingo ya kizazi. Hawakujua jinsi ya kuchunguza maambukizi na magonjwa mengine kuhusu mfumo wa uzazi, au kufanya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi. Kwa hivyo, hata kama Mira angalikuwa amekwenda mapema kwa ajili ya matibabu, wafanyakazi wa afya wasingeweza kumsaidia.

Matokeo yake, Mira alilazimika kusafiri umbali mrefu kwa gharama kubwa kwenda kumwona daktari ambaye aliweza kumwambia tatizo lake. Kwa wakati huo, alikuwa tayari amechelewa.

Hatimaye, nchi yake Mira ilikuwa maskini, yenye bajeti kidogo kwa ajili ya huduma za afya. Kama zilivyo serikali nyingi katika nchi maskini, serikali ya nchi yake iliwekeza kwenye huduma nyingine muhimu, lakini siyo afya ya wanawake. Sehemu kubwa ya bajeti kwa ajili ya afya ya wanawake ilikwenda kwenye hospitali kubwa mijini badala ya kuanzisha programu za afya ya jamii ambapo wanawake kama Mira wangefikiwa kwa urahisi zaidi. Hii inamaanisha kwamba huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi — na matatizo mengine mengi ya afya ya wanawake — hazikupatikana.

Umaskini na hadhi duni ya wanawake vilikuwa vikwazo vikubwa kwa Mira katika ngazi zote 3 — katika familia yake, katika jamii yake na katika nchi yake. Vikwazo hivi ndivyo vilichangia tatizo la afya ambalo lilisababisha kifo chake.


Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Feb 2018