Hesperian Health Guides

Vyoo kwa afya bora (usafi wa mazingira)

Katika sura hii:

Usafi katika jamii ni muhimu sana kama ulivyo kwa mtu binafsi na familia. Usafi wa mazingira humaanisha usafi wa jamii — kutumia vyoo safi na salama, kulinda usafi usalama wa vyanzo vya maji, na utupaji salama wa taka (angalia Taka, taka kutokana na huduma za afya, na uchafuzi wa mazingira - kinaadaliwa). Uchafuzi wa mazingira husababisha magonjwa na vifo vingi ambayo vingeweza kuepukika.

wanaume na wanawake wa umri tofauti, na watoto, mmoja akiwa na magogo yakutembelea, wakijadiliana jambo katika kikundi

Juhudi yoyote ile ya jamii kwa ajili ya kuboresha usafi wa mazingira lazima iwasaidie watu kuondokana na changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kawaida. Umasikini na ukosefu wa maji ya kutosha mara nyingi ni vikwazo vikubwa kwa watu kuboresha hali yao ya usafi ikiwemo huduma ya vyoo.

Wataalam wanaweza kupendekeza mifumo ya kisasa kama vile, vyoo vinavyotumia maji kusukuma kinyesi au miundo ya kiufundi ya hali ya juu ya kutibu kinyesi. Miundo hii ya kiufundi inaweza kufanya kazi katika baadhi ya maeneo, lakini haimaanishi kwamba itatatuwa matatizo ya jamii yako au kwamba watu wataitumia. Mfanyakazi wa afya ambaye anayajua na kuyasikiliza mahitaji ya watu atakuwa na taarifa muhimu ambazo mtaalam atakuwa anakosa. Wataalam na wanajamii wanapaswa kufanya kazi pamoja katika kutatua matatizo ya jamii.

Washirikishe wanawake katika majadiliano juu ya mahitaji ya jamii na ufumbuzi wake. Wanawake mara nyingi ndiyo watoa huduma wa kwanza kwa watoto na nyumba nzima. Hivyo wanaweza kutambua maswala ya usafi wa mazingira hususan yanayohusiana na choo na maji ambayo wanaume hawayaoni. Kila mtu anaposhirikishwa katika kufanya maamuzi na kufanya kazi kwa pamoja kuboresha hali ya usafi, watu wote hunufaika.

Matumizi ya vyoo-ufumbuzi kwa suala la kinyesi cha binadamu

Kinyesi cha binadamu kisiposimamiwa vizuri na kutupwa hovyo,huweza kuchafua maji, chakula na udongo kupitia vijidudu vya maradhi na kusababisha kuharisha na matatizo mengine makubwa ya kiafya. Matumizi ya vyoo huzuia vijidudu kuingia kwenye mazingira, na kulinda afya ya jamii nzima.

mwanamke akinawa mikono kwenye bomba la maji karibu na choo

Afya siyo sababu pekee ya kujenga na kutumia vyoo. Watu pia wanahitaji:

  • Faragha: Choo kinaweza kuwa sehemu ya kawaida mathalan shimo refu katika ardhi. Lakini kutokana na mahitaji ya faragha, ni muhimu choo kuwa na kijumba na mlango au pazia.Banda au kijumba kinaweza kutengenezwa kutokana na vifaa vya kawaida, au kutokana na mchanga na sementi.
  • Usalama: Ili choo kiwe salama, kinapaswa kujengwa vizuri na sehemu salama.Hakuna atakayekitumia choo iwapo atakuwa na wasiwasi kwamba kitabomoka au kudidimia. Na kama choo kitajengwa mbali na nyumba, au sehemu iliyojitenga,wanawake wanaweza kutojihisi salama kukitumia.
  • Ubora: Watu wanaweza kuwa tayari zaidi kutumia choo mahali mtumiaji atajisikia vizuri kukaa au kuchuchumaa,na chenye banda au kijumba kinachoruhusu mtu kusimama wima. Pia wanaweza kuwa tayari zaidi kutumia choo ambacho kipo karibu na nyumba na kimeezekwa au kukingwa dhidi ya upepo, mvua, au barafu.
  • Usafi: Kama choo ni kichafu na kinatoa harufu mbaya,hakuna atakayetaka kukitumia. Choo pia kinapaswa kuwa kisafi kuzuia ueneaji wa vijidudu. Iwapo wote wanaokitumia watashiriki katika huduma ya usafi, choo kinaweza kutumika na kutunzwa vizuri.
  • Heshima: Choo ambacho kinatunzwa kwa usafi wa hali ya juu huongeza heshima kwa mmiliki wake. Hii inaweza kuwa motisha kwa watu kutumia fedha zao, juhudi na rasilimali zingine kujenga vyoo bora.

Mahali pa kujenga choo

Katika kuchagua eneo la kujenga choo, hakikisha hakitachafua vyanzo vya maji kama vile mito, visima, au chemichemi. Choo kinapaswa kuwa angalau mita 20 kutoka kwenye chanzo chochote cha maji.

Pia hakikisha kuwa choo hakitachafua maji yaliyoko chini ya ardhi. Hatari ya maji ya ardhini kuchafuliwa hutegemea na aina ya udongo, hali ya mvua au unyevunyevu katika eneo hilo, na umbali wa tabakamaji kutoka usawa wa ardhi. Kumbuka kwamba tabakamaji huwa juu zaidi wakati wa msimu wa mvua kuliko wakati wa kiangazi.

Kanuni za msingi za kuzingatia ni pamoja na:

  • Shimo la choo liwe angalau mita 2½ juu ya tabakamaji.
  • Wakati wa kuchimba shimo la choo utakapokuta ardhi ikiwa na majimaji, au kama shimo litajaa maji, hii siyo sehemu nzuri ya kuchimba choo.Vijidudu vya magonjwa kutoka kwenye kinyesi vitachafua maji yaliyoko chini ya ardhi.
  • Usijenge vyoo maeneo yanayofurika mara kwa mara.
  • Kama kuna hatari ya maji yaliyoko chini ya ardhi kuchafuliwa kutokana na choo, angalia uwezekano wa kujenga choo kilichoinuliwa juu ya ardhi. Kama hakuna njia mbadala, basi choo kijengwe upande wa chini wa mwinuko ili vijidudu vya magonjwa kutoka kwenye choo visiweze kuingia kwenye visima vya maji.
angalia kisima chenye  kina cha kutosha kuyafikia maji yaliyoko chini ya ardhi, na linganisha na choo chenye kina kifupi ambacho hakifikii maji yaliyoko chini ya ardhi
Maji yaliyoko chini ya ardhi ni maji ambayo yamefyonzwa kwenye ardhi na ambayo hutiririka chini ya ardhi. Wakati wa kujenga choo, hakikisha shimo siyo refu sana kiasi cha kuchafua maji yaliyoko chini ya ardhi.

Aina ya vyoo

Kuna aina nyingi za vyoo, na hakuna aina moja ambayo inaweza kukidhi mahitaji ya kila jamii au kaya. Katika kufanya maamuzi juu ya aina ya choo cha kujenga, fikiria juu ya mahitaji ya wale watakaokitumia na nafasi iliyopo kwa ajili ya ujenzi huo. Pia fikiria iwapo wewe na familia yako mtahitaji kutumia choo chenye muundo wa kutengeneza mboji na mnao uwezo wa kukitunza. Kama hapana, basi choo cha shimo kinaweza kuwa ndiyo bora zaidi kwako.

Hakuna choo ambacho ni kamilifu asilimia mia moja. Kila aina ya choo ina mapungufu yake. Lakini aina 3 za vyoo ambavyo vimeelezewa katika sura hii ni bora kwa ajili ya kulinda usafi na usalama wa afya ya jamii, bila madhara makubwa kwa watu na mazingira.

Vyoo hivi havitumii maji. Hii ni kwa sababu vyoo vingi vya maji huhamisha tatizo (kinyesi na vijidudu vya magonjwa) kutoka sehemu moja na kulipeleka sehemu nyingine. Havibadilishi kinyesi cha binadamu kuwa salama, na wakati huo huo huchafua maji mengi (angalia chini). Lakini iwapo unatumia maji kwa ajili ya kutawazia baada ya kujisaidia, kuna vyoo salama ambavyo unaweza kujenga, kwa mfano, choo cha kumwaga maji baada ya kujisaidia (pour-flush toilet).

Vyoo vinavyotumia maji kuondoa kinyesi na mifumo ya kusafirisha majitaka kutoka vyooni

hoteli ikimwaga maji machafu yenye kinyesi karibu na kijito ambacho ni chanzo cha maji kwa ajili ya matumizi ya watu na mifugo

Vyoo vinavyotumia maji husafirisha majitaka yenye kinyesi kupitia mifumo maalum ya bomba ambayo hutengenezwa kwa ajili ya kazi hiyo. Husaidia kuboresha afya hasa katika maeneo yenye msongamano wa makazi mijini, na mara nyingi ndiyo aina ya vyoo ambavyo watu wengi hupendelea.

Lakini vyoo vinavyotumia maji vina matatizo mengi ambayo yanaweza kutokuwa wazi moja kwa moja. Majitaka yenye kinyesi lazima yatibiwe kwanza kabla hayajawa salama kurudishwa kwenye njia za maji za kawaida au kutumika tena. Hata hivyo, gharama yake ni kubwa, na mara nyingi majitaka yenye kinyesi huelekezwa kwenye mito, maziwa au bahari bila kwanza kutibiwa vya kutosha. Hii hueneza vijidudu vya maradhi kutoka kwenye majitaka hayo hadi kwenye njia zetu za maji za kawaida au za majirani zetu.

Kemikali nyingi ambazo hutumika kutibu majitaka yenye kinyesi huchafua vyanzo vya maji ya kunywa na ardhi mahali ambapo watu huishi na kulima mazao yao ya chakula. Wakati kuna watu wengi ambao wanakosa maji ya kutosha ya kunywa, siyo sahihi kupoteza maji mengi kiasi hicho.

Choo cha shimo kilichofunikwa

NWTND was Page 10-1.png

Choo cha shimo kilichofunikwa hujengwa sakafu juu yake na huwa na tundu na mfuniko kwa ajili ya kufunika tundu hilo wakati choo hakitumiki. Sakafu inaweza kutengenezwa kwa miti, zege, au magogo yaliyofunikwa na udongo. Sakafu za zege husaidia kuzuia maji kuingia ndani na kupunguza matatizo ya kiafya kwa sababu ni rahisi kusafisha. Choo kilichofunikwa kinapaswa kuwa na sehemu ya kushikilia sakafu au kingo za zege kuzuia sakafu au shimo lenyewe kuporomoka.

Kuongeza bomba la kupunguza harufu mbaya na nzi ni muhimu na hukifanya choo kuwa bora zaidi kutumia.

Choo kilichofunikwa chenye kina cha mita 2 huchukua wastani wa miaka 5 kujazwa na familia ya watu 5.

Tatizo la vyoo vya shimo ni kwamba shimo linapojaa, choo hakiwezi kutumika tena.Hata hivyo, unaweza kutumia mabaki kwenye shimo lililojaa-ambalo kuta zake hazijasakafiwa – baada ya kuondoa banda au kijumba chake, kupanda mti eneo hilo. Au, kwa jitihada zaidi za kila siku, unaweza kugeuza mabaki kwenye shimo lenye kuta zilizosakafiwa kuwa mboji yenye thamani kubwa. Choo cha kutengeneza mboji ni choo rahisi kutengeneza.

 wanaume wawili wakitumia mawe kuimarisha shimo
wanaume wawili wakitengeneza sakafu juu ya shimo la choo

Kutengeneza choo cha shimo kilichofunikwa

  1. Chagua sehemu ambayo itafikika kwa urahisi na ambayo haina hatari ya kuchafua vyanzo vya maji.
  2. Chimba shimo mita 1 upana na angalau mita 2 kwenda chini. Kama udongo wa eneo hilo ni wa kichanga sana, unaweza kuliimarisha shimo kwa kutumia mapipa tupu ya mafuta au kwa matofali ya sementi, ili shimo lisibomoke.
  3. Tandaza magogo, mawe, matofali, bimu ya zege au malighafi nyingine inayofaa yatakayoibeba sakafu au jukwaa na kusaidia kuzuia kuta za shimo zisibomoke. Bimu ya kokoto iliyosukwa inaweza kufaa zaidi.
  4. Tengeneza jukwaa au sakafu na banda au kijumba juu ya shimo. Sakafu au jukwaa inaweza kutengenezwa kwa kutumia malighafi zilizopo kwenye jamii kama vile kokoto, magogo na udongo. Kama utaamua kujenga sakafu au jukwaa kwa kutumia magogo, tumia magogo ambayo hayaozi haraka.

Jinsi ya kutengeneza jukwaa la zege na bimu yake

Jukwaa au sakafu ikiwa na bimu (ring beam) husaidia kuzuia shimo la choo kubomoka. Pia sakafu ya zege hurahihisha usafi wa choo kufanyika.

Mfuko mmoja wa saruji wa kilo 50 unatosha kutengeneza majukwaa 2 ya vyoo na bimu zake 2 za zege. Ni rahisi zaidi vinapotengenezwa pamoja. Pia utahitaji waya za kufunga bimu na jukwaa, matofali na mbao pana kwa ajili ya kujenga bimu na kubeba zege. Utahitaji pia ubao uliotengenezwa kama tundu la kuingiza ufunguo kwa ajili ya kutengeneza tundu la choo. Majukwaa na bimu ambazo zimeoneshwa hapa ni za pembe 4 lakini unaweza kutengeneza zenye umbo la mduara.

1. Tandaza tandiko la plastiki au mifuko ya saruji iliyotumika chini kwenye sehemu tambarare. Juu yake, tengeneza ukingo wa matofali au mbao wenye sentimeta 120 urefu, sentimeta 90 upana na setimeta 6 kina.
Jukwaa au sakafu la choo Bimu
mpangilio wa sakafu la choo
mpangilio wa bimu yake
Tengeneza ukingo wa matofali au mbao wenye sentimeta 120 urefu, sentimeta 90 upana na sentimeta 6 kina. Weka kifaa cha mbao chenye muundo wa tundu la ufunguo katikati ili kulipa sura tundu la choo. Tengeneza bimu ya sentimeta 130 kwa urefu na mita 1 upana kwa nje, na mita 1 urefu na sentimeta 70 upana kwa nje.
2. Tengeneza zege kwa kuchanganya kipimo kimoja cha saruji, vipimo 2 vya kokoto, vipimo 3 vya mchanga, na maji. Mwaga zege sehemu ya jukwaa iliyotengenezwa hadi ijae nusu.
mwanaume akichota na kumimina zege kwenye msingi wa jukwaa la choo
zege ikimiminwa kwenye bimu ya jukwaa la choo

3. Weka wavu wa waya wenye ukubwa wa milimita 3 juu ya zege ambayo haijakauka ili iwe imara.
mishale ikionesha wapi pakuweka vishikio kwenye zege kwa ajili ya jukwaa la choo
Tengeneza vishikio kwa kutumia waya wenye ukubwa kuanzia milimita 8 hadi 10 na kuisimika kwenye zege karibu na kona.
Kwa ajili ya jukwaa: tumia waya 4 hadi 6 katika kila upande.
mshale ukionesha jinsi ya kulaza waya kwenye zege ndani ya bimu
Kwa ajili ya bimu: tandaza waya kila upande wa bimu.
4. Mimina zege iliyobaki na kusawazisha kwa kutumia gogo la ubao.
kuongeza zege zaidi na kuisawazisha kwa ajili ya jukwaa la choo
kuongeza zege zaidi na kuisawazisha kwa ajili ya bimu
5. Ondoa sehemu yenye umbo la tundu la funguo kutoka kwenye jukwaa mara zege itakapoanza kukauka (baada ya saa 3). Iwapo ulitumia tofali, ondoa tofali na kutengeneza shimo kwenye sehemu yenye umbo la tundu la ufunguo.
6. Funika zege na mifuko ya sementi iliyolowesha, kitambaa chenye majimaji, au shuka la plastiki. Lowesha tandiko litakalofunika zege hiyo mara kadhaa kila siku ili libaki na unyevu kwa siku 7. Unyevu huwezesha kokoto kukauka taratibu na kuwa imara zaidi.
 mwanume na mwanamke wamebeba bimu ilioimarika
7. Zege itakapokauka kabisa, peleka bimu hiyo eneo choo kitakapojengwa. Sawazisha eneo hilo, weka bimu na kuchimba shimo ndani yake. Kusanya udongo nje ya bimu ili kufitisha. Halafu weka jukwaa juu ya shimo.
8. Tengeneza mfuniko kwa ajili ya tundu la choo kwa kutumia zege au mbao. Mfuniko unaweza kuwa na kishikio, au unaweza kusogezwa kwa mguu ili kuepuka kuchafua mikono na vijidudu vya magonjwa.
Wanawake 3 wakipeleka kijumba cha choo kwenye shimo jipya

Vyoo vyenye muundo wa kutengeneza mboji

Choo chenye muundo wa kutengeneza mboji huhifadhi kinyesi cha binadamu hadi kitakapooza na kugeuka mboji. Mchakato huu huachia joto ambalo huua vijidudu vya magonjwa vilivyomo, yakiwemo mayai ya minyoo ambayo kawaida ni vigumu sana kuyaangamiza. Vyoo vyenye muundo wa kutengeneza mboji vinaweza kuonekana jambo la ajabu mwanzoni, lakini vinapotumika vizuri ni njia salama zaidi ya kudhibiti kinyesi cha binadamu na kurutubisha udongo wakati huo huo.

Chimba shimo lenye kina cha mita 1, na chini ya mita 1 upana. Sakafia kuta za shimo na kujenga jukwaa kama ambavyo ungeweza kufanya kwa shimo la choo lingine. Lakini kijumba kitengenezwe kwa njia ambayo itaruhusu kuhamishika.

Jinsi ya kutumia na kutunza choo chenye muundo wa kutengeneza mboji

  • Kabla ya kutumia, weka majani makavu ndani ya shimo. Majani hayo yatasaidia kinyesi kuoza.
  • Mimina kiganja kilichojaa udongo uliochanganyika na majivu au majani makavu kila baada ya kutumia. Hii hupunguza harufu na husaidia mchanganyiko kuoza haraka.
  • Usitupe plastiki, makopo, au aina nyingine ya taka kwenye choo.
  • Fagia na kusafisha sakafu mara kwa mara. Kuwa mwangalifu maji mengi au kiasi kikubwa cha dawa za kufanyia usafi kisingie ndani ya shimo.
  • Shimo linapokaribia kujaa, ondoa kijumba, jukwaa au sakafu na bimu. (Itachukua wastani wa mwaka 1 kwa familia ya watu 5 kujaza choo cha aina hii chenye kina cha mita 1.)
  • Jaza shimo na udongo wa sentimeta 15 uliochanganyika na mabaki ya mimea. Baada ya wiki kadhaa, mabaki hayo yatatulia.
  • Ongeza udongo na majani, maji, halafu panda mti. Miti ya matunda huota vizuri zaidi na kutoa matunda mengi ambayo ni salama.

 mwanamke akipanda mche karibu na choo cha shimo na miti mingine 3 ya matunda

  • Au, mboji inaweza kutolewa nje na kutumika kurutubisha miti au mazao ya chakula, lakini iwe imeoza kabisa. Hivyo, ruhusu ioze kabisa angalau kwa mwaka 1 na itumike tu inapokuwa imegeuka kuwa kama udongo wenye mboji usio na harufu kabisa.
  • Hamisha kijumba, jukwaa, na bimu sehemu nyingine, chimba shimo na rudia tena mchakato wa kutengeneza mboji nyingine.

Choo chenye muundo wa kutengeneza mboji -kwa ajili ya maeneo yasiyokuwa na ardhi ya kutosha

Choo cha aina hii ni muhimu sana kwa maeneo yenye msongamano wa makazi, mahali ambapo watu hawana nafasi nje ya kujenga vyoo vya shimo. Kinaweza kujengwa hata ndani ya nyumba na hakitatoa harufu kama kitatunzwa vizuri na kufanyiwa usafi mara kwa mara.

Kwa choo cha aina hii, lazima utenganishe mkojo ili kinyesi kiweze kukauka na kugeuka mboji haraka zaidi. Kutenganisha mkojo pia husaidia kupunguza harufu.

  1. Tengeneza boksi la mbao lenye ukubwa wa kutosha kuingia ndani ya ndoo yenye ujazo wa galoni 5.
  2. NWTND was Page 14-1.png

  3. Weka ndani chombo cha kuchepusha mkojo. Unaweza kununuakifaa hiki madukani, au kukitengeneza kwa kukata jagi la plastiki sehemu ya chini na pembeni, halafu ukaifitisha mbele ya tundu.
  4. Pachika ncha moja ya mrija sehemu ya choo ya kuchepusha mkojo. Weka ncha nyingine kwenye jagi kupokea mkojo
  5. Weka ndoo ya galoni 5 chini ya choo kukusanya kinyesi.
 Choo kilichotengenezwa kutokana na boksi la mbao
Ndoo ikiwa chini ya bakuli ya choo na jagi la kupokea mkojo

Jinsi ya kutumia na kutunza choo cha aina hii

Ni muhimu kila atakeyekitumia choo hiki kupewa mafunzo juu ya matumizi yake sahihi.

  • Kabla ya kutumia, weka safu ya majani makavu kwenye ndoo. Hii itasaidia kutunza usafi wa ndoo.
  • Ongeza kiganja kilichojaa mchanganyiko wa udongo na majivu au majani makavu kwenye ndoo kila baada ya kutumia. Hii husaidia kupunguza harufu na kinyesi kuoza haraka. Usitupe taka kama vile plasitiki au makopo kwenye choo. Zuia majimaji ukiwemo mkojo, kuingia kwenye ndoo. Kama kinyesi kwenye ndoo kitaelekea kuwa majimaji, ongeza udongo au majivu.
  • Mkojo utatiririka kupitia kwenye mrija na kukusanyika kwenye chombo kilichotegwa chini yake. Baadae, mkojo unaweza kuchanganywa na maji na kutumika kama mbolea. Changanya vipimo 3 vya maji na kipimo 1 cha mkojo na kumwagilia mimea mara 3 kwa wiki. Au mwaga mkojo mbali na nyumba.
mwanamme akimimina ndoo ya mabaki ya kinyesi kwenye pipa
  • Ndoo inapojaa kinyesi (takriban baada ya wiki 2 kwa familia ya watu wa 5), mimina kwenye chombo kikubwa chenye mfuniko.Hapo ndipo mabaki haya yatahifadhiwa. Chombo hiki kitakapojaa,kitunzwe kwa mwaka 1 (sehemuinayofikiwa na jua) hadi kibadilike kuwa mboji. Baada ya mwaka 1, mboji inaweza kutumika shambani, bustanini, au kwa ajili ya mimea inayooteshwa kwenye makopo. Familia inaweza kuhitaji vyombo vikubwa kadhaa kuhifadhi mabaki yote ya kinyesi yanayozalishwa.
  • Kila unapofaulisha mabaki ya kinyesi kutoka kwenye ndoo, safisha ndoo na maji yaliyochangaywa na klorini ili kuua wadudu.
  • Choo kinapokua hakitumiki, funga mfuniko wa boksi. Hii itapunguza harufu.

Vyoo vyenye muundo wa kutengeneza mboji vinahitaji matunzo makubwa. Lakini vinapotumika vizuri, ni ufumbuzi muhimu sana kwa jamii zisizo na nafasi kubwa ya kujenga vyoo, na pia kutengeneza mbolea muhimu kutokana na kinyesi.

Vyoo vinapaswa kuwa rafiki kwa matumizi ya watu wote katika jamii

Ongea na kila mtu ambaye atatumia choo hicho kujua mambo gani yanafaa kuzingatiwa kurahihisha matumizi yake kwa wote. Mchoro huu unaonesha njia za kukifanya choo kuwa rafiki kwa matumizi ya mtu mlemavu ambaye anatembelea kwenye kiti cha magurudumu matatu.

mwanamke katika kiti cha magurudumu 3 akiwa kwenye choo ambacho kimerekebishwa ili kuwa rafiki kwa matumizi yake
Banda lenye ukubwa wa kutosha kuruhusu kiti cha magurudumu kuingia ndani.
Kengele au chochote kile kutoa sauti iwapo msaada unahitajika.
Sehemu ya kuegemea kumsaidia mtu kukaa.
Papi au mbao za kushika kumsaidia mtu kutoka kwenye kiti kwenda kwenye choo.
Sehemu ya kukalia kwenye choo kwenye usawa na kiti cha magurudumu.
Mlango mpana ambao hufunguka kwa nje kurahisisha mtumiaji kuingia.
Kitasa cha mlango kikiwa na kamba ya kuvuta.
Njia ya kwenda chooni ni tambarare na rahisi kwa ajili kwenda na kutoka ndani ya nyumba.
Kumbuka, mtu mwenye ulemavu anahitaji faragha kama mtu mwingine yeyote na anapaswa kupata faragha anayohitaji.