Hesperian Health Guides

Saratani

Katika sura hii:

Saratani ni ugonjwa gani?

mwanamke akiangalia kupitia darubini.
Seli ni ndogo sana, unaweza kuziona tu kwa kutumia darubini.

Mili yetu na viumbehai vimeundwa na seli. Seli ni chembe au uniti ndogo za aina tofauti ambazo kwa kufanya kazi pamoja hutengeneza kiumbehai. Kila seli pia ni hai. Hujigawa ili kutengeneza seli mpya, na kila seli hatimaye hufa.

Wakati mwingine seli mpya hutengenezwa zikiwa na hitilafu na kuwa hafifu. Kawaida hii haisababishi madhara yoyote kwa mwili kwa ujumla, kwa sababu ni seli moja tu kati ya mamilioni ya seli, na baada ya muda mfupi hufa. Lakini wakati mwingine seli yenye hitilafu hujigawa na kutengeneza seli zaidi na zaidi zinazofanana. Seli hizi zenye hitilafu huzaliana na kutengeneza tungamo au kivimbe chenye madhara kwa afya (tyuma).

Kivimbe kinaweza kuwa siyo hatari, maana yake hakienei au kusababisha madhara. Au kinaweza kuwa na madhara, kikiendelea kukua na kuvamia sehemu zingine za mwili. Hii ni saratani. Kutegemea na aina ya seli na mahali zinapoota, saratani inaweza kukua polepole na bila madhara, au kusababisha ugonjwa hatari au hata kifo.

Saratani siyo ugonjwa mmoja. Kila aina ya saratani ni tofauti. Baadhi zinaweza kuzuilika na zingine hutibiwa kwa urahisi na hata kupona. Saratani zingine ni hatari sana.

Kama una hofu kuwa una saratani

mwanamke akiongea na mwanaume.
Inaweza kuwa saratani — au yanaweza kuwa maambukizi ya kawaida!

Kufikiria kuwa una saratani kunaweza kukutia hofu sana. Usichelewe kutafuta msaada iwapo una dalili yoyote ambayo inaweza kuashiria saratani, lakini kuwa mtulivu na kumbuka dalili nyingi za saratani pia ni dalili za magonjwa mengine ya kawaida yasiyo hatari. Kwa aina nyingi za saratani, njia pekee yenye uhakika ya kujua kama unayo ni kupata kipimo cha biopsi ambacho kinahusisha uchunguzi wa tishu iliokatwa kutoka mwili-hai kwa kutumia hadubini. Kipimo cha biopsi hupatikana kwenye hospitali na baadhi ya vituo vya afya. Wakati wa kupimwa, mfanyakazi wa afya huondoa kipande kidogo sana cha tishu kutoka sehemu ambayo inafikiriwa kuathiriwa na saratani na kukichunguza kwa kutumia hadubini kuangalia kama kuna seli zenye hitilafu.

Kama kivimbe kipya kinaanza kuota au kusababisha maumivu, chini ya ngozi yako au sehemu yoyote ndani ya mwili wako, kinapaswa kuchunguzwa. Hii ni muhimu hasa kama ni kigumu na hakitembei. Kivimbe kinaweza kuwa ni maambukizi au uvimbe wa kawaida tu ambao hauna madhara na utatoweka wenyewe. Lakini inaweza kuwa dalili ya saratani, aina ambayo inawezekana kugundulika haraka na kutibiwa. Muulize daktari kama una kivimbe ambacho:

mwanaume mwenye vivimbe kadhaa shingoni na kiunoni.
  • Kinakua na kuongezeka
  • Ni kipya na kinaendelea kuwepo baada ya wiki kadhaa
  • Kinasababisha maumivu
  • Ni kigumu ukikigusa

Mwili hupambana na maambukizi kupitia mfumo wa limfu, lakini tezi za limfu zinaweza pia kuwa sehemu ambapo saratani huanzia. Muone mfanyakazi wa afya iwapo una uvimbe au kivimbe ambacho kimeendelea kuwepo:

  • Nyuma ya sikio
  • Kwenye shingo au chini ya kidevu
  • Chini ya kwapa na kwenye kinena


Kama mtu ana kivimbe kwa miaka mingi ambacho hakiongezeki au kubadilika, huenda siyo saratani.

Zipo dalili za kawaida ambazo huashiria aina tofauti za saratani, lakini siyo saratani zote huwa na dalili hizi. Na dalili zote zinaweza kusababishwa na matatizo sugu ya kiafya ambayo hayahusiani na saratani. Katika sura hii, utasoma juu ya dalili ambazo zinahusiana mahsusi na:

Dalili za kawaida kwa saratani nyingi

Kwa ujumla, dalili hizi hujitokeza saratani inapokuwa imefikia kiwango kikubwa, hivyo siyo dalili nzuri za kutegemea katika kubainisha saratani mapema.

mwanamke akiwa kwenye chumba cha kusubiria cha kiliniki ya uchunguzi wa saratani. Bango linasema " Uchunguzi wa saratani ya matiti kila jioni."
Uchunguzi wa saratani huokoa maisha. Huduma hii inapaswa kupatikana kwa kila mtu.
  • Kupungua uzito
  • Kujisikia mchovu muda wote
  • Maumivu makali ambayo hayapungui


Kama unadhani unaweza kuwa na saratani, tafuta mfanyakazi wa afya wa kukushauri juu ya njia mbalimbali zilizopo kwa ajili ya matibabu au huduma na wapi pa kuzipata. Tafuta mtu wa kukusindikiza kila unapokwenda kukutana na daktari kukusaidia kuuliza maswali na kukumbuka taarifa.

Programu za uchunguzi wa saratani

Baadhi ya saratani zinaweza kugundulika mapema, kabla hazijaonesha dalili, kupitia programu za uchunguzi zinazopima watu walio katika hatari ya kupatwa na saratani mbalimbali. Programu za uchunguzi kwa ajili ya saratani mara nyingi hulenga saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti kwa sababu inawezekana kugundua saratani hizi kabla hazijaleta madhara, na saratani hizi mara nyingi zinaweza kutibiwa vizuri bila kuleta madhara zikigundulika mapema.

Saratani inapogudulika mapema, uwezekano wa matibabu kufanikiwa unakuwa mkubwa zaidi.


Nani anapata saratani?

Tunajua mambo mengi juu ya nini kinachosababisha saratani, lakini mara zote hatujui kwa nini baadhi ya watu hupata saratani na kwa nini wengine hawapati. Kila mtu anaweza kupata saratani na uwezekano huongezeka kadri umri unapoongezeka. Kwa aina chache za saratani (hasa saratani ya matiti), kuwa na mtu mmoja kwenye familia mwenye saratani ni kiashiria kuwa huenda mtu mwingine naye atakuwa nayo. Lakini saratani nyingi haziwi na mbegu kifamilia. Tunajua kuwa:

  • Uchawi, laana, au ibilisi havisababishi saratani.
  • Njia za uzazi wa mpango hazisababishi saratani.
  • Saratani siyo adhabu kwa ajili ya kosa ulilofanya.
  • Saratani haienei kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine — haiwezekani kupata saratani kwa karibu au kukaa muda mrefu, au kumhudumia mtu mwenye saratani.


Baadhi ya mambo kama vile uvutaji sigara husababisha saratani. Vilevile, baadhi ya kemikali ambazo huingia katika miili yetu kazini au kupitia vyakula, bidhaa tunazotumia, na kutokana na uchafuzi wa hewa au maji huweza kusababisha saratani. Kuna njia za kuzuia saratani lakini kuna mambo mengi yanayosababisha saratani ambayo mtu mmoja mmoja ana udhibiti juu yake. Hata kama watu 2 tofauti watawekwa katika mazingira hatari, haimaanishi kuwa wote 2 watapata saratani.

Kwa sababu saratani na visababishi vyake vinaweza kuonekana kutatiza, watu wenye saratani mara nyingi hunyanyapaliwa au hutendewa vibaya na wengine. Hii inaweza kuwazidishia ugonjwa. Watu wenye saratani wanahitaji upendo na misaada kama wagonjwa wengine.