Hesperian Health Guides

Njia ya vijiti na sindano za kuzuia mimba

Katika sura hii:

Kama kilivyo kidonge kidogo cha majira, njia ya vijiti na sindano za kuzuia mimba vina homoni ya projestini tu, lakini mwanamke hatakiwi kukumbuka kutumia kidonge kila siku. Njia ya vijiti na sindano za majira ni rahisi kutumiwa kwa siri. Hata hivyo, siyo njia ya vijiti wala sindano za majira ambayo inatoa kinga dhidi ya maambukizi yanayopitia ngono vikiwemo VVU.

Vijiti vikiwa vinaingizwa mwilini.

Jinsi ya kutumia njia ya vijiti au sindano za majira

Vijiti vya majira ni virija vidogo vya plastiki ambavyo mfanyakazi wa afya huingiza chini ngozi ya upande wa ndani wa mkono wa mwanamke. Huzuia mimba kwa miaka 3 hadi 5, kutegemea na aina ya vijiti.

NWTND FP Page 15-2.png
sindano na dawa ya majira.

Sindano za majira hutolewa na mtaalam wa afya, mara moja kila mwezi 1, 2, au 3, kutegemea na aina ya sindano.

Vijiti na sindano za majira ni njia rahisi kutumika kwa siri, na mwanamke hatakiwi kukumbuka kutumia kidonge kila siku. Vijiti vyote vya majira na baadhi ya sindano zina projestini tu. Aina moja ya sindano (sindano ya kila mwezi) ina homoni zote mbili –estrojeni na projestini. Hivyo sindano hii haifai kwa wanawake ambao hawawezi kutumia vidonge mseto vya majira. Mwanamke anaweza kuamua kusimamisha sindano za majira au kuondoa vijiti vya majira kama atataka kupata mimba. Njia ya vijiti au sindano haiwezi kutoa kinga yoyote dhidi ya maambukizi yanayopitia ngono vikiwemo VVU.

Madhara ya pembeni

Sindano za majira za kila mwezi zinaweza kuwa na madhara ya pembeni yanayofanana na vidonge mseto vya majira. Njia ya vijiti na sindano za projestini tu zina madhara ya pembeni yanayofanana na vidonge vidogo vyenye projestini tu.

Dawa ambazo huingiliana na njia ya vijiti na sindano za majira

Rifampicin (dawa ya kifua kikuu) na baadhi ya dawa za kifafa hupunguza ufanisi wa njia ya vijiti na sindano za majira. Kama unatumia dawa hizi, tumia njia tofauti ya uzazi wa mpango. Wanawake ambao wanatumia insulini kwa ajili ya tatizo la kisukari wanaweza kuhitaji kurekebisha kiasi cha insulini wanachotumia baada ya kuanza njia ya vijiti au sindano za majira.

Kusitisha matumizi ya vijiti au sindano za majira

Ili kusitisha matumizi ya vijiti, unapaswa kupata mtaalam wa afya ambaye ataviondoa. Mwanamke anaweza kupata mimba mara moja baada ya kuondoa vijiti hivyo vya majira. Kusimamisha sindano za majira ni rahisi. Ni suala la kuacha kuchoma sindano hizo. Inaweza kuchukua muda mrefu zaidi kwa mwanamke kupata mimba baada ya kusimamisha matumizi ya sindano za kuzuia uzazi. Hata hivyo wanawake wengi wanaweza kupata ujauzito ndani ya mwaka 1.