Hesperian Health Guides

Majeraha ya moto

Katika sura hii:

Majeraha madogo ya moto

Kwa ajili ya majeraha madogo ya moto, haraka mwaga maji baridi juu ya ngozi iliyoungua kwa dakika 15 hadi 30. Hii itasaidia kupooza na kusafisha ngozi na kupunguza maumivu.

NWTND fa Page 37-1.png

Tunza eneo la jeraha kwa usafi kwa kutumia sabuni isiyochubua na maji kadri litakavyokua linapona. Asali au juisi ya aloevera husaidia kuharakisha uponyaji wa vidonda vidogo, lakini inapaswa kuwekwa tu baada ya jeraha la moto kupoa.

Majeraha madogo ya moto yanapaswa kupona ndani ya wiki 1 hadi 3.

Majeraha hatari ya moto

Majeraha hatari ya moto yanajumuisha:

  • Majeraha ya moto ambayo yameingia ndani. Huwa hayaumi isipokuwa yakibinywa kwa sababu neva zinakuwa zimeangamizwa. Hayabadiliki rangi yanapobinywa. Yanaweza kuwa na rangi ya madoa madoa, lakini kama yameingia ndani, yanaweza kuwa yananata na meupe, au kama ngozi ngozi ya grei, au meusi kama mkaa.
  • Majeraha makubwa ya moto. Jeraha kubwa la moto ni lile ambalo hufunika asilimia 10 au zaidi ya mwili. Hata kama halijaingia ndani, jeraha la moto la ukubwa huu ni hatari. Unaweza kukadiria kiasi gani cha mwili kimeungua kwa kigezo cha ukubwa wa kiganja cha mkono wa mtu aliyeungua. Je jeraha linafunika ukubwa wa kiganja cha mkono ? Hii ni takriban asilimia 1 ya mwili. Viganja 10 ni takriban asilimia 10.
  • Jeraha la moto ambalo hufunika kiungio, uso, au via vya uzazi. Majeraha haya yanaweza kuweka alama kubwa za kudumu na kumtia mtu ulemavu, hususan mtoto.
  • Majeraha ya moto yakiungana na majeraha mengine.
  • Majeraha ya moto miongoni mwa watoto. Watoto hukabiliana na matatizo makubwa katika kupona kutokana na majeraha ya moto na kila inapowezekana wanapaswa kuhudumiwa kwenye hospitali zenye zana za kutosha kutibu majeraha ya moto.


Tafuta msaada kwa ajili ya majeraha hatari ya moto. Wakati mnaelekea hospitali au kituo cha afya, mpe maji ya kunywa kidogokidogo kila baada ya muda mfupi kama yuko macho na ana fahamu zake. Funika eneo la jeraha na kitambaa safi. Kwa majeraha hatari, epuka kuingiza kidonda kwenye maji baridi—maji yanaweza kususha sana joto la mwili kiasi cha kuhatarisha maisha. Jaribu kumtuliza mgonjwa.

Matibabu
  • Mtu mwenye jeraha kubwa la moto au ambalo limeingia ndani anaweza kupungukiwa na maji mwilini kutokana na majimaji ya mwili kupotea yanapochuruzika kutoka kwenye kidonda. Mpe vinywaji zaidi. Kawaida ni bora zaidi kumpa kinywaji hicho kupitia dripu. Kupungukiwa na maji mwilini pia kunaweza kusababisha mshituko. Hivyo angalia iwapo kuna dalili zilizoorodheshwa. Angalia Kuwahudumia wagonjwa (inaandaliwa) kwa ajili ya taarifa zaidi juu ya utaratibu wa kumuongezea mtu maji mwilini.
  • Majeraha ya moto na eneo linalozunguka ni rahisi sana kupata maambukizi. Tunza jeraha katika hali ya usafi na safisha kila siku kwa maji yanayotiririka, au kwa kuloweka jeraha kwa muda mfupi ndani ya maji safi. Sabuni kidogo isiyo kali husaidia lakini usitumie dawa za kuua wadudu au aidini. Hivi vitachelewesha uponyaji. Taratibu pangusa au kwangua kiasi kidogo cha tishu iliyokufa.
  • Paka jeraha lihamu ya kuzuia maambukizi na baada ya hapo funika na shashi safi au aina nyingine ya kitambaa safi. Funga vizuri ili kuweka mgandamizo kiasi kwenye kidonda bila kuzuia mzunguko wa damu. Badilisha bandeji kila siku na kila mara inapochafuka. Bandeji chafu inaweza kusababisha maambukizi. Unaweza kuhitaji kuloweka bandeji ambayo imegandamana kwenye kidonda. Hakikisha kuwa vidole vya miguu au mikono ambavyo vimeungua vinafungwa kila kidole kivyake na kutenganishwa.
  • Toa dawa ya antibiotiki kama baadhi ya dalili zifuatazo zitaonekana: ngozi kutoa harufu mbaya, ngozi kutunga usaha, kugeuka nyekundu au kupata moto, au mgonjwa kupata homa. Angalia taarifa juu ya dawa za antibiotiki. Hakikisha ratiba yake ya chanjo za tetanasi imeenda kama inavyostahili. Angalia Chanjo (inaandaliwa).
  • Kama malengelenge yatapasuka, tunza usafi wa eneo hilo. Kama hayajapasuka, usijaribu kuyatoboa. Malengelenge yaliyo wazi hupata maambukizi kwa urahisi.
  • Majeraha ya moto yanauma sana. Usisite kumpa dawa za kupunguza maumivu zenye nguvu zikiwemo mofini (morphine) au dawa zingine katika kundi hilo. K ila mara mpe dawa ya kupunguza maumivu kabla ya kukisafisha kidonda au kubadilisha bandeji kwenye kidonda hatari. Vidonda vya moto huanza kuwasha vinapokuwa vinapona. Dawa kutoka kundi la antihistamini (antihistamine) zinaweza kusaidia kutuliza mwasho.
  • Vyakula vingi vyenye virutubishi vikiwemo protini ya ziada vinahitajika kusaidia kidonda cha moto kupona. Hata kama utakuwa husikii njaa, kula mara 4 au kula vyakula vyenye nishati zaidi na vingine katikati ya milo wakati unapona. Vyakula vyenye nishati nyingi ambavyo vimeelezewa katika "Lishe bora hutengeneza afya bora” vimesheheni virutubishi.
  • Sehemu zilizoungua zinaweza kukakamaa na kushindwa kutembea, hasa kama jeraha lipo kwenye kiungio. Sehemu hizi zinapaswa kutembezwa kila baada ya saa chache. Kama mtu hawezi kutembeza kiungio chake mwenyewe, taratibu msaidie.


Kama ilivyo kwa majeraha makali, tafuta msaada kama hali ya mgonjwa itazidi kuwa mbaya.