Hesperian Health Guides

Maambukizi

Katika sura hii:

Kidonda chochote kinaweza kupata maambukizi.

Dalili za maambukizi

Kidonda kitakuwa kimeambukizwa iwapo kutatokea:

  • kuvimba, kugeuka chekundu na kupata moto
  • kutunga usaha
  • kutoa harufu mbaya


Maambukizi yatakuwa yanaenea sehemu zingine za mwili iwapo itatokea:

  • homa
  • tezi za limfu au mitoki kuvimba na kuanza kuuma kwa ndani
Tezi za limfu —ambazo mara nyingi huitwa mitoki— ni mitego midogo kwa ajili ya vijidudu vinavyosababisha magonjwa ambavyo hujenga uvimbe mdogo chini ya ngozi ya mwili panapotokea maambukizi. Kuvimba matezi au mtoki humaanisha maambukizi yameingia.
Mwili wa mtu ukionyesha sehemu 5 ambapo tezi za limfu hukaa.
Chini ya taya humaanisha maambukizi ya meno au kooni.
Nyuma ya sikio humaanisha maambukizi kichwani au kwenye ngozi ya kichwa na nywele zake, mara nyingi yanayosababishwa na vidonda kwenye ngozi au chawa. Au surua ya rubella inaweza kuwa chanzo.
Chini ya sikio na shingoni humaanisha maambukizi ya sikio,usoni,au kichwani. Au inaweza kuwa kifua kikuu.
Mitoki kwapani, humaanisha maambukizi kwenye mkono, kichwani, au ziwani. Au wakati mwingine saratani ya ziwa (angalia Saratani).
Mitoki kwenye
nyonga
humaanisha maambukizi
kwenye mguu, kikanyagio, ukeeni au umeeni, au unyeo.
Matibabu ya maambukizi

Safisha vizuri kidonda. Inaweza kuhitaji kutoboa au kupasua jipu au kuondoa nyuzi. Kwa taarifa zaidi juu ya majipu angalia Matatizo ya ngozi (kinaandaliwa). Isipokuwa tu kama eneo ambalo limeambukizwa ni dogo na linapata nafuu haraka, kawaida ni bora zaidi kumpa dawa ya antibiotiki. Mpe dikloksasilini (dicloxacillin), sefaleksini (cephalexin), AU klindamaisini (clindamycin). Kama kidonda kimeingia sana ndani, mpe chanjo ya tetanasi (angalia Chanjo – kinaandaliwa) na tetanus immunoglobulin.

Kama maambukizi hayapungui, yanaweza kueneza sumu kwenye damu (sepsisi).