Hesperian Health Guides

Kutokwa damu

Katika sura hii:

Mgandamizo kwenye jeraha kuzuia uvujaji damu

Kugandamiza moja kwa moja, kwa nguvu juu ya sehemu inayovuja damu kunaweza kuzuia karibu uvujaji wote wa damu, hata kutoka kwenye vidonda vikubwa ambavyo vinatoa sana damu. Hata kama mtu atakuwa anatokwa damu kichwani, gandamiza sehemu hiyo ili kuzuia uvujaji.

  1. Inua sehemu iliyojeruhiwa ili iwe juu ya usawa wa moyo wa mgonjwa.
  2. Kamata kitambaa kisafi kilichoko karibu, kunja ili kupata upana unaolingana na ukubwa wa kidonda, na kukigandamiza moja kwa moja na kwa nguvu juu ya kidonda. Muoneshe mtu aliyejeruhiwa jinsi ya kugandamiza kitambaa hicho kwenye jeraha mwenyewe, kama anaweza. Kama kidonda ni kikubwa sana, weka shashi-kitambaa chepesi cha wavu kwa ajili ya kufunika vidonda au kukausha damu (gauze) au kitambaa kingine kisafi. Endelea kugandamiza kidonda hadi uvujaji damu usimame. Usikiondoe kitambaa hata kinapolowa na damu. Badala yake, ongeza kitambaa kingine juu yake. Kwa ajili ya kidonda kikubwa, usiondoe mkono wako hadi zipite angalau dakika 15- usiondoe mkono hata kuangalia iwapo utokaji damu umesimama.


NWTND fa Page 8-1.png


Uvujaji damu utakapokua umepungua au kusimama, unaweza kufunga kwa kukaza kitambaa au kitu chochote kisafi juu ya eneo linalotoa damu. Weka shashi au kitambaa kingine kisafi kilichokunjwa vizuri kulingana na eneo husika juu ya kidonda na baada ya hapo funga bandeji, kwa kukaza, kuzunguka jeraha. Hakikisha bandeji imekaza vya kutosha ili kuweka shinikizo la kutosha juu ya kidonda, lakini usikaze sana kiasi cha kuzuia damu kuzifikia sehemu zilizobaki kwenye mguu au mkono.

Kusimamisha uvujaji damu ni kazi ngumu. Usikate tamaa na kuacha kujaribu!


Kamwe usitumie uchafu, mafuta ya taa, au unga wa kahawa kusimamisha uvujaji damu.

Damu inaweza kuchafua kila kitu sehemu husika na kuonekana kwamba majeruhi amepoteza damu nyingi sana kuliko kiasi halisi alichopoteza. Lakini mwangalie kwa makini majeruhi kuchunguza dalili zifuatazo ambazo zinaonesha huenda amepoteza damu nyingi sana:

Dalili za hatari
  • Kuchanganyikiwa au kupoteza fahamu
  • Mapigo ya moyo kwenda haraka sana
  • Baridi,unyevu au majimaji, na rangi ya ngozi ya mwili kufifia


Kama utaona dalili hizi, inua miguu yote 2 kwa kutumia kitu chochote kinachofaa ili iwe juu ya usawa wa moyo, na baada ya hapo tafuta msaada kwa ajili ya mshituko.

Hata kama hutaziona dalili hizi, kaa na majeruhi au mwangalie kila baada ya dakika 10 hadi 15 kuhakikisha yu salama na kumtia moyo. Endelea kuwa karibu naye hadi atakapoanza kutenda na kujisikia kama kawaida.

Toniketi (Tourniquet)

Tumia toniketi (bandeji au mpira unaofungwa sehemu fulani ya mwili ili kudhibiti mzunguko wa damu) kama njia ya mwisho, iwapo unafikiria kuwa ni bora kupoteza angalau mkono au mguu kuliko kupoteza uhai wa majeruhi.

Tumia toniketi pale tu:

  • Kiungo kimeondolewa au kimeharibika sana kiasi kwamba hakiwezi kuokolewa.
  • Damu inavuja sana kutoka kwenye mguu au mkono na haionekani kupungua hata unapogandamiza kitu. (Umejaribu kugandamiza kwa nguvu zaidi kwanza?)
  • Kuna kidonda kikubwa chenye shimo kwenye paja, kama vile kutokana na risasi, vipande vya risasi au bomu, au vitu vingine vimeingia ndani ya msuli, na majeruhi anaonesha dalili hatari za kupoteza damu mathalan udhaifu mwilini, kuchanganyikiwa, au rangi ya ngozi kupauka au kubadilika. (Ni vigumu kutumia mgandamizo wa kutosha kwenye paja kubwa kuzuia uvujaji mkubwa wa damu.)


Tumia mkanda mpana, au kitambaa kilichokunjwa na kutengeneza kipande bapa kufunga na kutenganisha sehemu inayotoka damu. Usitumie kamba nyembamba au waya. Itakata ngozi na kuingia ndani ya ngozi.

Mpeleke hospitalini haraka kadri uwezavyo. Una saa 2 au 3 kabla ya kiungo kilichojeruhiwa kupotea kabisa.

Hatua 1:
Funga toniketi juu lakini karibu na kidonda, katikati ya kidonda na mwili. (Kosa ambalo hujitokeza sana ni kufunga toniketi mbali sana na kidonda).

Hatua 2:
Funga na kukaza toniketi kuzunguka mguu mara 2. Halafu funga fundo.

Hatua 3:
Weka kijiti kifupi imara juu ya fundo. Funga mafundo 2 zaidi juu ya kijiti.

Hatua 4:
Nyosha kijiti ili kukaza toniketi hadi uvujaji damu utakaposimama.

Hatua 5:
Funga kijiti katika nafasi yake kwa kutumia kitambaa kingine.
Kipande cha ngozi kimeshikiliwa juu kwa kutumia kibanio wakati maji yakitiririshwa kwenye kidonda.