Hesperian Health Guides

Kutapika

Katika sura hii:

Kutapika mara moja au mara mbili kawaida siyo hatari na hutoweka bila matibabu.Kama mtu anatapika akiwa na homa au matatizo ya tumbo:

  • Mpe kiasi kidogo (lakini kila baada ya muda mfupi) cha kinywaji cha kuurudishia mwili maji. Baadhi ya watu hupendelea vinywaji vinavyosababisha kucheua kama vile soda kupunguza kuchefuchefu. Kama unatapika kila unachokula, kunywa kijiko kimoja kidogo. Subiri dakika 15, kunywa kingine. Kama hutayatapika, kunywa kijiko kingine baada ya dakika 5. Lengo ni kunywa zaidi haraka kadri uwezavyo bila kuchochea kutapika zaidi.
  • Kupunguza kichefuchefu, tengeneza chai kwa kutumia tangawizi, au tumia aina nyingine ya mmea ambao unaujua.
  • Utakapoanza kujisikia vizuri, kula kidogo kidogo kila baada ya muda, na kuendelea kutumia vinywaji ili kufidia maji ambayo utakuwa umepoteza.

mwanamke akimsaidia mgonjwa kukaa na kunywa

Dalili za hatari
  • Kutapika kunakosababisha upungufu wa maji mwilini.
  • Kutapika kwa zaidi ya saa 24, au kutapika ambako huzidi kuongezeka.
  • Kutapika kwa nguvu matapishi yenye rangi ya kijani kizito au rangi ya udongo, au yakiwa na harufu ya kinyesi (angalia utumbo kuziba).
  • Kutapika damu au matapishi yanayofanana na kahawa iliyosagwa (angalia vidonda vya tumbo na sirosisi katika Madawa, pombe na tumbaku - sura inaadaliwa).
  • Kutapika kunakoambatana na homa, na maumivu ambayo hudumu kwa zaidi ya saa 24. Angalia maumivu makali tumboni (acute abdomen).