Hesperian Health Guides

Kama una saratani

Katika sura hii:

Kugundua kuwa una saratani kawaida ni jambo la kushtua, kwa maelezo rahisi. Lakini kuna mambo kadhaa ambayo unaweza kufanya kupambana na saratani na kupata unafuu zaidi.

  • Kama unafikiri una saratani, jaribu kutafuta daktari au kiliniki yenye uzoefu wa kushughulikia saratani. Unaweza kuhitaji zaidi ya kipimo 1 kupata uhakika.
  • Kama utambiwa una saratani, muulize daktari juu ya ugonjwa huo. Mambo gani huwapata watu wengi ambao wana aina hii ya saratani? Unaweza kufanya nini ili kuishi maisha marefu zaidi au kunusurika na saratani?
  • Tafuta matibabu haraka. Saratani nyingi zinaweza kutibiwa kwa mafanikio ikiwa zitabainishwa mapema. Kuna njia gani tofauti za matibabu? Njia hizi za matibabu zina madhara gani ya pembeni?
  • Ongea na watu wengine wenye saratani. Kawaida wana ushauri muhimu na ni waelewa na wasikilizaji wazuri hasa kama wamekuwa na saratani kama ya kwako na sasa wanaendelea vizuri.
  • Usiamini maneno ya kupotosha au hadithi zisizo za busara kutoka kwa marafiki na wanafamilia. Mara nyingi hazina ukweli.
  • Kula chakula chenye virutubishi hukufanya uendelee kuwa na nguvu zaidi.
  • Fanya mazoezi kila siku — hata matembezi mafupi. Tafuta njia ya kupumzika, kwa mfano yoga, taamuli (meditation), au kuamua tu kubaki peke yako kwa dakika chache.
  • Tafuta watu ambao wanaweza kukusaidia. Saratani na matibabu yake yanaweza kusababisha uchovu, kichefuchefu, na maumivu. Saratani pia inaweza kulemaza na kufanya vigumu mtu kutembea hapa na pale au kufanya kazi. Mfanyakazi wa afya anaweza kufahamu miongozo, vitabu na machapisho mbalimbali vya kukusaidia.


Juhudi za kuboresha afya na maisha ya mgonjwa lazima zipewe kipaumbele katika matibabu ya saratani.

Kugundua kwamba una saratani, kutibiwa na kuukubali ugonjwa huu ni mambo magumu kisaikolojia. Fikra na hisia za kupoteza matumaini au kujawa na wasiwasi ni kawaida. Hivyo huduma ya kukabiliana na matatizo ya kisaikolojia (kiakili na kihisia) ina umuhimu sawa na huduma zingine za kitabibu. Kuna njia kadhaa za kupata huduma na misaada ya kisaikolojia.

watu wakila pamoja.
  • Pata muda wa kutosha kukaa na watu unaowapenda.
  • Zungumzia hisia na wasiwasi wako na mtu unayemwamini.
  • Omba au shiriki katika shughuli za kiroho na waumini wenzako.
  • Endelea na shughuli ambazo huwa unafurahia.
  • Pumzika na kustarehe kwa muziki, taamuli (meditation), na mazoezi ya kistaarabu.


Kwa taarifa zaidi jinsi ya kusaidia kutuliza hisia za msongo au wasiwasi, angalia sura ya Afya ya akili (inaandaliwa).