Hesperian Health Guides

Kuboresha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango

Katika sura hii:

Jaribu kufikiria hali ya jamii itakavyokuwa iwapo huduma za uzazi wa mpango zitakuwa zikipatikana kwa ukamilifu. Wanawake na wanaume wote, wakiwemo vijana balehe, watakuwa wanapata taarifa za kuaminika juu ya njia zote za uzazi wa mpango. Huduma za uzazi wa mpango zitapatikana kwa gharama nafuu, na kuwafikia wanawake –walioolewa na wasioolewa-ambao wanataka kutumia huduma hizo. Huduma za uzazi wa mpango zitawezesha upatikanaji wa njia tofauti za kuzuia mimba, ili mwanamke aweze kutumia njia ambazo anapendelea na zinazokidhi mahitaji yake. Mwisho, taarifa za uzazi wa mpango na huduma zenyewe zinaweza kumfikia kila mtu wakiwemo vijana, wanawake ambao hawajaoolewa, na wale waishio mbali na vituo vya afya.

Sehemu hii inatoa mawazo kuhusu uandaaji wa mpango wa kusaidia upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango kwa kila mwanamke katika jamii.

mwanamke akiwambia wenzake 2 jambo.
Njia mbili tu-kondom na vizuizi (daframu ) ndiyo zinapatikana kwenye kliniki, lakini ningependa kutumia vidonge vya majira! Watu wengi zaidi hutumia huduma za uzazi wa mpango wanapopewa fursa ya kuchagua kati ya njia kadhaa.

Jifunze juu ya uzoefu wa wanawake

Katika kusaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango kwenye jamii yako, unaweza kuanza kwa kuwauliza wanawake wana maoni gani au wanatumia njia zipi kuzuia mimba na kupanga uzazi kwa ujumla. Kama baadhi ya wanawake wamepitia uzoefu mzuri, uzoefu huo unaweza kuwasaidia wanawake wengine kujifunza. Kusikiliza shuhuda na taarifa za wanawake ambao wametumia njia tofauti za uzazi wa mpango na kuridhika nazo husaidia kuondokana na fikra potofu na uoga juu ya njia za kuzuia mimba. Hi inaweza kuwatia moyo wanawake wengine kujifunza na kuamua iwapo njia za kuzuia mimba na uzazi wa mpango kwa ujumla unafaa hali zao.

Jifunze juu ya changamoto za wanawake na vijana balehe katika kupata taarifa na huduma za uzazi wa mpango. Unaweza kuanza kwa kukusanya taarifa juu ya vikwazo kwa kuuliza maswali juu ya njia zilizopo na gharama zake. Watu hupata taarifa na huduma za uzazi wa mpango kutoka wapi?

mfanyakazi wa afya akiongea na mwanamke mlangoni mwa nyumba yake.

Yafuatayo ni baadhi ya maswali mengine ambayo unaweza kutumia kuwezesha washiriki kujifunza kutokana na uzoefu wa wanawake:

  • Je huduma za uzazi wa mpango zinapatikana kwa urahisi na ni rafiki kwa mtumiaji?
  • Je ni vigumu kwa mwanamke aliyeoolewa kupata taarifa na nyenzo za uzazi wa mpango? Kwa nini?
  • Je ni vigumu kwa vijana balehe au wanawake ambao hawajaolewa kupata taarifa na nyenzo za uzazi wa mpango? Kwa nini?
  • Je wanaume walio wengi wana mawazo gani juu ya uzazi wa mpango? Je wako tayari kutumia njia za uzazi wa mpango? Kama hapana kwa nini ?
  • Serikali inachangiaje kukuza au kudidimiza uzazi wa mpango? Hakikisha unaongea na watu kutoka makundi mengi tofauti katika kutafuta taarifa hizi.

Jadili vikwazo kuhusiana na upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango

Baada ya kujifunza juu ya uzoefu wa wanawake, inawezekana ukapatikana uelewa mzuri zaidi juu ya sababu nyingi ambazo zinawafanya wanawake kutumia au kutotumia huduma za uzazi wa mpango!

Zoezi la Mti wa Matatizo ni njia nzuri ya kusaidia kikundi kujadili vikwazo vinavyohusiana na na huduma za uzazi wa mpango, na kuchunguza sababu za msingi ambazo zinakwamisha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango kamilifu. Ufafanuzi wa sababu za msingi na mahusiano kati ya sababu hizo, hatimaye hurahihisha ubainishaji wa masuala ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele na njia bora zaidi za kuyakabili.

mwanamke akitafakari kuhusiana na uzazi wa mpango
Mti wa Matatizo unaweza kutumika kwa njia mbalimbali. Unaweza kuwa bango ambalo hutumika tena na tena katika mikutano na mijadala. Unaweza kutolewa kama zana ambayo hukamilishwa na mshiriki mwenyewe. Huwa napendelea kubandika Mti wa Matatizo kwenye ukuta wa kliniki kama kazi ya sanaa ambayo imetengenezwa na wanawake wenyewe. Baadhi ya watu hubuni miti ya ziada; kwa mfano Mti wa Ufumbuzi wa Matatizo. Miti hii huonyesha ufumbuzi kwa matatizo kupitia mizizi, na matokeo mazuri au matunda kupitia majani.

Zoezi Mti wa Matatizo wa kuwezesha mjadala juu ya vikwazo kuhusiana na huduma ya uzazi wa mpango


Jinsi ya kutengeneza Mti wa Matatizo:

Mti wa Matatizo bila maelezo yoyote.

Chora mti kwenye karatasi pana, kitambaa, ubao wa chaki, au hata chini kwenye udongo. Matawi na mizizi yasiwe na maelezo yoyote. Andaa vipande vya karatasi kwa ajili ya kuandika mawazo au maoni yatakayotolewa juu ya visababishi au vikwazo, na pia matokeo au athari za ukosefu wa huduma za uzazi wa mpango. Baadhi ya watu hutumia vikaratasi vya bandika bandua kwa ajili ya kuandika maelezo kwa sababu ni rahisi kuhamisha hapa na pale.

Andika tatizo la afya husika, kwa mfano, "Hakuna Uzazi wa Mpango" kwenye shina.

  1. Toa maelezo ya utambulisho juu ya Mti wa Matatizo na sababu za msingi (mizizi ya matatizo).
    Kama kikundi hakina ufahamu juu ya mizizi ya matatizo, unaweza kutumia mfano wa magugu na umuhimu wa kuondoa magugu na mizizi yake ili kusafisha shamba.
  2. Jadili sababu za msingi.
    Wambie wanakikundi kujadili sababu tofauti na vikwazo walivyogundua ambavyo vinasababisha wanawake kutotumia njia za uzazi wa mpango kwa ajili ya kuzuia mimba zisizotakiwa. (Kama kikundi kitapata ugumu na njia hii, unaweza kuandaa hadithi ambayo inaonesha baadhi ya visababishi au vikwazo katika upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango katika jamii yako, na kuwaomba wanakikundi kutafakari hadithi hiyo.) Andika mawazo ya washiriki juu ya sababu na vikwazo kwenye vikaratasi ambavyo utabandika kuzunguka mizizi kwa kutumia gundi ya karatasi, au viweke chini karibu na mizizi. Mpe kila mtu nafasi ya kutaja jambo ambalo husababisha au kuchangia ukosefu wa upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango.
  3. Panga sababu za msingi kwenye makundi.
    Soma kwa sauti sababu zote au vikwazo ambavyo kikundi kimefikiria. Waombe wanakikundi kujadili mawazo hayo na kuweka yale ambayo yanahusiana sana pamoja kwenye mzizi mmoja. Kwa kuangalia makundi ya vikwazo unaweza kusaidia kikundi kuangalia aina tofauti za visababishi . Weka majina ambayo yanawakilisha aina ya visababishi kwenye mizizi.
    Njia nyingine ya kufanya zoezi hili ni kutoa maelezo mapema. Kadri watu watakapokuwa wanataja vikwazo tofauti kuhusiana na upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango, weka mapendekezo yao karibu na mzizi ambao unahusiana zaidi. (Angalia Sababu msingi za ukosefu wa huduma za uzazi wa mpango kwa ajili ya makundi ya sababu za msingi ambazo unaweza kutumia.)
  4. Angalia matokeo-athari.
    Unaweza kuendelea na zoezi na kuwaomba wanakikundi kutaja matokeo au athari za ukosefu wa huduma za uzazi wa mpango kwa wanawake, familia zao na jamii. Mapendekezo yao yanaweza kuandikwa kama majani na kubandikwa kwenye matawi ya mti. Unaweza kuwaomba washiriki kupanga matawi kwa kuweka mawazo yanayofanana kwa kukaribiana.
    mti wa matatizo ukiwa na maelezo kwenye mizizi yakiwemo "gharama za nyenzo za uzazi wa mpango", "ukosefu wa elimu" na matokeo au athari zikijumuisha "athari za kiafya" na "msongamano nyumbani"

Sababu za msingi za ukosefu wa huduma za uzazi wa mpango

Kupanga vikwazo tofauti au sababu zinazohusiana kwenye makundi(kwa kutumia Mti wa Matatizo au zoezi lingine linalofaa) kunaweza kusaidia wanakikundi kuanza kufikiria njia mbalimbali za kuboresha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango.

Vikwazo vya kisiasa. Kama serikali haitilii mkazo uzazi wa mpango, huduma zinazotolewa mara nyingi zinakuwa kidogo na njia za uzazi wa mpango chache. Vilevile, viongozi wa jamii wasipounga mkono uzazi wa mpango wanaweza kuchangia ugumu zaidi katika upatikanaji wa huduma hizo.

mizizi ya mti ikiwa imeelezewa kama vikwazo vya kisiasa na vikwazo vingine.

Vikwazo vya kiuchumi: Njia za uzazi wa mpango zinaweza kuwa ghali kuliko uwezo wa wanawake. Wanawake pia wanaweza kukatishwa tamaa na kutotumia uzazi wa mpango kama jamii inachukulia watoto-hususan watoto wa kiume-kuwa mtaji wa kiuchumi kwa familia.

Vikwazo vya kijamii: Majukumu ya kijinsia ambayo yameegemea kwenye mila na tamaduni mara nyingi humaanisha kuwa wanawake hawawezi kufanya maamuzi juu ya afya zao, na wanaume wanaweza kuamini kuwa kutumia njia za uzazi wa mpango kunaweza kuwafanya kuonekana siyo wanaume wa ukweli. Vilevile, vijana balehe wanaweza kutokuwa huru kuongea na wazazi wao, walimu, na wafanyakazi wa afya, na hivyo kutopata taarifa za kutosha juu ya afya ya ujinsia, na uzuiaji mimba.

Vikwazo vya kiutamaduni au kidini: Upinzani mkubwa kutoka vikundi vya kidini unaweza kusababisha ugumu kwa watu kupata taarifa za kuaminika na nyenzo za kuzuia mimba. Kwa upande mwingine, wafanyakazi wa afya wanaweza kutoelewa au kutoheshimu imani za kiutamaduni juu ya uzazi wa mpango.

Vikwazo vya kimazingira: Kama huduma za afya zitakuwa mbali au ngumu kufikia, wanawake wanaweza kutopata kuduma za uzazi wa mpango za kuaminika na kadri zinavyohitajika. Na pia katika jamii zenye viwango vikubwa vya vifo vya watoto, wanawake wanaweza kujisikia kutaka watoto wengi zaidi kwa kutumaini kuwa wapo watakaonusurika.

Vikwazo vya kihisia-kisaikolojia: Wanawake mara nyingi wanaweza kukosa uwezo wa kujiamini na kujiheshimu, au uwezo wa kufanya maamuzi ambayo yanahusu maisha yao. Wanaweza pia kutowaamini wafanyakazi wa afya kwamba watawahudumia vizuri na kutunza siri zao.

Vikwazo vya kimaumbile au kibiolojia: Wanawake wenye matatizo ya kiafya, kwa mfano shinikizo la damu la juu (presha), wanaweza kushindwa kupata njia za uzazi wa mpango ambazo zinafaa hali zao.

Kutafuta ufumbuzi wa kuboresha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango

Baada ya kuangalia sababu za msingi, wanakikundi wanaweza kuibua ufumbuzi au mikakati ya kusaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango kwa wanawake wote. Katika kuchagua hatua gani za kupewa kipaumbele wakati wa kupanga, ni muhimu kufikiria hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa katika ngazi ya mwanamke mmoja mmoja, familia zao, na jamii nzima.

Zoezi Zana ya mpira uliofungwa kamba ya katani kwa ajili ya kubungua bongo na kuibua njia za ufumbuzi


Katika kutambulisha zoezi, wambie wanakikundi kuangalia Mti wa Matatizo juu kutambua vikwazo au sababu za msingi ambazo zinachangia wanawake kutotumia huduma za uzazi wa mpango. Eleza kwamba zoezi hili litawasaidia kubungua bongo na kuibua hatua za ufumbuzi ambazo zinaweza kuchukuliwa katika ngazi ya mtu binafsi, familia na jamii( rejea kwenye matawi ya Mti wa Matatizo). Kwa zoezi hili, utahitaji kuondoa "athari au matokeo" ambavyo ni majani kutoka kwenye Mti kwanza ili uweze kuvibadilisha kuwa "ufumbuzi."

  1. Wambie wanakikundi kusimama katika mduara. Mwezeshaji anapaswa kusimama nje ya mduara. Kwa kuanzia, muombe mtu mmoja kushika mwisho wa kamba ya katani iliyofungwa kwenye mpira, na ataje kikwazo kimoja kwa huduma ya uzazi wa mpango. Baada ya hapo, muombe mwanakikundi mwingine kufikiria ufumbuzi kwa kikwazo hicho.
  2. Mpira wa kurusha uliofungwa kamba ya katani (yarn toss)
  3. Mtu wa kwanza hukamata ncha ya kamba hiyo na kurusha mpira kwa mtu mwenye wazo kuhusu ufumbuzi. Mwombe aliyerushiwa mpira kuelezea wazo lake la ufumbuzi na kuona kama linaweza kuchukuliwa katika ngazi ya mtu binafsi, familia au jamii. Uliza kama kuna mtu mwenye wazo lingine la ufumbuzi ambazo linaweza kutumika kushughulikia kikwazo hicho katika ngazi nyingine, ambacho hakijatajwa, (mtu binafsi, familia au jamii ). Mtu wa pili atashika kamba, na kurusha mpira kwa mtu mwingine ambaye pia atachangia wazo lake.
  4. Kadri hatua za ufumbuzi zitakapokuwa zinapendekezwa, ziandike kwenye vipande vya karatasi (ambavyo vinaweza kukatwa kufanana na majani). Bandika vipande hivyo vya karatasi kwenye Mti- katika maeneo ya matawi ambayo yanawakilisha hatua ya ngazi ya mtu binafsi,familia au jamii.
  5. Muombe mwanakikundi mwingine kuibua kikwazo kingine kwa uzazi wa mpango. Baada ya hapo waombe wanakikundi wengine kuchangia mawazo juu ya ufumbuzi wa kikwazo hicho kipya. Endelea na zoezi hadi hapo kikundi kitakapokuwa kimetengeneza utando wa kamba ya katani na kila mtu kwenye kikundi atakuwa ametaja aidha kikwazo au ufumbuzi.
  6. Katika kuhitimisha, tafakari pamoja na wanakikundi juu ya orodha ya hatua ambazo wanaweza kuchukuwa katika ngazi zote 3, na juu ya maana ya utando ambao wametengeneza. Weka utando huo wa kamba ya katani chini na kukusanya njia za ufumbuzi (majani) kwenye mti. Unaweza, baada ya hapo, kuchagua hatua gani za kushughulikia kwanza, na zoezi la Kuandaa mpango kazi (kinaandaliwa).